TUTATUMIA NGUVU YA UMMA KUKWAMISHA KATIBA: CHADEMA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitatumia nguvu ya umma kuikataa Katiba Mpya endapo CCM na Serikali yake: “vitae...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/09/tutatumia-nguvu-ya-umma-kukwamisha.html
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitatumia nguvu ya umma
kuikataa Katiba Mpya endapo CCM na Serikali yake: “vitaendeleza hila na
ubabe katika mchakato unaoendelea.”
Pia chama
hicho kikuu cha upinzani nchini, kimeitaka Serikali kuboresha Daftari la
Kudumu la Wapigakura kabla ya upigaji wa kura ya maoni ya Katiba Mpya
huku kikisema kinyume chake suala hilo litaibua mgogoro mkubwa.
Kauli hizo
zimetolewa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, John Mnyika katika
mahojiano yaliyofanyika Mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.
Mnyika
alisema baada ya CCM kuhodhi muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
na hivyo kulifanya Bunge la Katiba liwe ni hodhi ya chama hicho tawala
karata pekee waliyobakiwa nayo ni kura ya maoni... “Rais Kikwete ambaye
pia ni Mwenyekiti wa CCM, ndiye atakayeteua wajumbe 166 kutoka taasisi
na makundi na kufanya Bunge zima la Katiba kuwa na wajumbe zaidi ya
600.”
Alisema kwa sasa, Tanzania Bara hakuna utaratibu wa kikatiba wa namna ya kuendesha kura ya maoni na kuongeza.
“Wenzetu
Zanzibar katika Katiba yao wanao mfumo wa kura ya maoni, sisi haupo ni
lazima tutengeneze sheria ya kura ya maoni ya Katiba Mpya na Sheria ya
kura ya maoni ya Muungano,” alisema Mnyika.
Mnyika
alisema Kamati ya Bunge la Katiba, Sheria na Utawala inapaswa kuanza
kukutana kwa dharura kupata maoni ya wadau kuhusu kura ya maoni na ianze
na Zanzibar ambayo haikushirikishwa.
“Kamati
ianze sasa, isisubiri Bunge la Oktoba 29 maana kati ya mambo
yaliyoifanya Serikali kuondoa muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni ni
mgongano wa kikatiba kati ya Zanzibar na Muungano,” alisema.
Alisema pia
Tanzania inahitaji kuwa na Katiba ya mpito ambayo itaweka chombo huru
kitakachosimamia upigaji wa kura ya maoni badala ya Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC).
Mbowe
alisema Serikali ya CCM inatumia hila na ubabe kuhakikisha inapatikana
Katiba Mpya itakayobeba masilahi ya chama hicho kwa gharama yoyote.
“Endapo CCM
itaendelea na hila zake hizi niwaambie Chadema tumejipanga… Tutatumia
teknolojia ya kisasa kuwafikia Watanzania hata ikibidi kutumia helikopta
nne ili waikatae wakati wa kupiga kura ya maoni,” alisema Mbowe na
kuongeza: “Hila yoyote itakayotokea kwenye Katiba tutahamasisha
Watanzania kuikataa, wasifikiri wanachokifanya ni salama kwao… Wanageuza
mchakato kuwa wa kichama badala wa wananchi.”
Alisema
msimamo wa CCM kukataa mapendekezo ya muundo wa Serikali tatu si wa
wanachama wake wa kawaida, bali matakwa ya viongozi wake wa juu.
“Tunapozungumzia
kumdhibiti Rais, wao (CCM) wanafikiri tunamzungumzia Rais Kikwete
(Jakaya)… Tunataka kudhibiti madaraka ya Rais yeyote ajaye awe wa
Chadema, CCM au NCCR”.
Alisema
mapendekezo ya wananchi kuhusu Serikali tatu yalianzia wakati wa Rais wa
Zanzibar, Aboud Jumbe mwaka 1984 na baadaye mwaka 1991 wakati wa Tume
ya Jaji Mkuu Francis Nyalali.
Alisema
pamoja na kutotekelezwa kwa mapendekezo hayo ya wananchi, bado wabunge
wa G55 walianzisha vuguvugu hilo lakini likazimwa kwa kutumia nguvu
kubwa.
“Tume ya
Jaji Robert Kisanga nayo ilikuja na mapendekezo hayohayo na sasa Tume ya
Jaji Joseph Warioba na bado CCM haitaki kuamini ni ya wananchi,”
alisema.
Mbowe
alisema ndiyo maana Chadema sasa kimeamua kujitoa mhanga kuwahamasisha
hadi wanachama wa CCM kuikataa Katiba Mpya endapo itapatikana nje ya
matakwa ya Watanzania... “ Nia tunayo, sababu tunayo na uwezo tunao.”
Alisema
matumizi ya polisi hayatalipatia taifa Katiba Mpya na nzuri. “Wajue kuwa
wako Watanzania wenye busara kwa mamilioni walioko nje ya Bunge ambao
wana sauti katika Katiba yao na CCM wasifikiri wao ni alfa na omega
(mwanzo na mwisho),” alisema Mbowe.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema hata kama
Tanzania haitapata Katiba Mpya hadi ifikapo 2015, bado ya sasa haitafaa
kutumika.
“Hata kama
tutashindwa kupata Katiba Mpya hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi na katiba
hii ya sasa kwa sababu katiba mpya ya Zanzibar imejiingiza katika
mgogoro na Katiba ya Muungano,” alisema.
Alisema kama
dalili za kutopatikana kwa Katiba Mpya zimeanza kuonekana, ni vyema
ikatumika busara na hekima katika kuvuka kikwazo hicho na njia pekee ni
meza ya mazungumzo.
“Sisi siyo
tutakaoifanya Tanzania isitawalike, bali CCM… Tunafanya haya kwa nia
njema kabisa, hatutaki damu ya Watanzania imwagike kwa jambo
linaloepukika,” alisema.