ZITTO AJIWEKA NJIA PANDA
ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe amejiweka katika mazingira magumu zaidi kisia...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/11/zitto-ajiweka-njia-panda.html
ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema, Zitto Kabwe amejiweka katika mazingira magumu zaidi kisiasa
ndani ya chama hicho, kutokana na shaka kubwa iliyougubika mkutano wake
na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam juzi.
Zitto pamoja na viongozi wengine wawili wa
Chadema; Dk Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba walivuliwa nyadhifa zao na
Kamati Kuu ya Chadema baada ya kubainika kupanga mbinu za uasi, kupitia
waraka ambao ulikuwa ukieleza mkakati wa kufanya mabadiliko makubwa ya
kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani.
Leo, uongozi wa Chadema umeitisha mkutano wa waandishi wa habari ambao pamoja na mambo mengine, utajibu baadhi ya hoja za utetezi ambazo zilitolewa na Zitto pamoja na Dk Kitila. Katika mkutano wa juzi, Zitto na Dk Kitila ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, walizungumzia kuvuliwa kwao madaraka, lakini maandalizi na uendeshaji wa mkutano huo yanazua shaka kutokana kuwahusisha watu wanaodaiwa kuwa ni wanachama wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi (UVCCM).
Miongoni mwao, wamo waliowahi kuwa wanachama wa
Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Habib Mchange na Mtela Mwampamba
ambao walitimuliwa kwa makosa yanayofanana na yale yalizosababisha Zitto
na wenzake kuvuliwa nyadhifa zao.
Mchange na Mwampamba pamoja na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Shonza, walivuliwa uanachama wa Baraza hilo Januari 5, mwaka huu baada ya kupatikana na hatia ya kutumia mitandao ya kijamii kukihujumu Chadema na kuwatukana viongozi wake wakuu. Baadaye walihamia CCM wanakoendeleza harakati zao za kisiasa.
Jana, Machange alipotafutwa, alisema: “Mimi
sikuwahi kuondoka Chadema, nilifukuzwa kihuni kama walivyowafanyia Zitto
na Kitila. Nimepeleka malalamiko yangu tangu Januari hadi leo
sijajibiwa, hivyo siwezi kusema nimeondoka.
Nataka nimuunge mkono mwathirika mwenzangu kama ilivyokuwa mimi lakini nitabakia kuwa mwanachama mwaminifu.
“Mimi ni mwanaChadema na sikuwahi kujiunga na CCM
au chama chochote, walioondoka ni Mwampamba na Shonza.” Mwampamba
alisema: “Nilijitokeza pale kuonyesha mshikamano kwa sababu mimi pia ni
mwathirika. Kwa hiyo nilitaka ulimwengu ufahamu kuwa mimi ni kati ya
wanaopinga siasa za aina hii... Chadema ni chama kinachojiandaa kuchukua
dola, sasa kama kila mwenye mawazo tofauti anaonekana mhaini itakuwaje
siku wakichukua dola? Ubaguzi huu haujalishi uko chama gani, hata kama
niko CCM, hilo halinizuii kuungana na mtu aliyepatwa na tatizo kama
langu.”
Kuwepo kwao katika mkutano wa Zitto kunaweza kutumiwa na uongozi wa Chadema kuwa uthibitisho wa kiongozi huyo kushiriki katika uasi na kunaweza kupuunguzia nguvu utetezi unaotolewa na Dk Kitila kwamba hakuwa sehemu mpango wa kuuondoa uongozi wa sasa madarakani. Zitto, Dk Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba wanasubiri kukabidhiwa barua za kuvuliwa kwao madaraka na katika siku 14 wanapaswa wawe wamewasilisha utetezi wao wakieleza kwa nini wasifukuzwe uanachama kutokana na tuhuma zinazowakabili.
Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa alisema
jana kuwa ilikuwa lazima viongozi hao wavuliwe madaraka hasa baada ya Dk
Kitila kukiri kuhusika na waraka ambao anasema ulilenga kushinda
kupitia uchaguzi halali ndani ya chama hicho.
“Hata katika ya nchi ukihusika kutengeneza mbinu
za siri lazima ushughulikiwe.Hakuna Katiba itakayokuruhusu kufanya
mipango ya siri. Kwanza uchaguzi wa Chadema nani katangaza mpaka mipango
ianzwe kutengenezwa sasa hivi?” alihoji Dk Slaa.
Mkutano leo
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene akizungumza jana alisema: “Kamati Kuu ilijadili mambo mengi na hayo ndiyo tunataka umma ufahamu msimamo wetu kama chama.”
Wasomi wanena
Alikiri kwamba watuhumiwa hao hawajapewa barua za uamuzi wa
Kamati Kuu na alipoulizwa sababu, alisema Katiba ya chama hicho haitoi
mwisho wa mtu kupewa barua, huku akihoji: “Wao nani kawaambia waende kwa
waandishi wa habari?”
“Mimi ndiye Katibu Mkuu. Katiba inasema ni lini
barua iandikwe? Utatokaje kwenye kikao alfajiri na wakati huohuo uandae
barua za kuwapa?” alihoji Dk Slaa.
Mkutano leo
Mkutano wa waandishi wa habari ulioitishwa leo
unatarajiwa kujibu baadhi ya hoja za utetezi za viongozi hao
zilizotolewa juzi. Zitto alifichua kile alichokiita tuhuma zilizotolewa
dhidi yake mbele ya Kamati Kuu akimaanisha kwamba tuhuma zilizotamkwa
kwenye vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
hazikuwa kamilifu.
Habari zinasema uongozi wa Chadema utaweka wazi
kile kinachodaiwa kuwa ni “Zitto kujitungia tuhuma, kisha kuzipatia
majibu”, badala ya kujibu hoja ambazo zilitolewa na Kamati Kuu.
Jana, Dk Slaa akizungumzia suala hilo alisema
Kamati Kuu haiwezi kuchaguliwa tuhuma za kusema na za kuacha... “Hiyo
hoja walete kwenye vikao, nani anayeipangia Kamati Kuu ichukue hatua
gani pale inapotaka kufanya hivyo?”
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene akizungumza jana alisema: “Kamati Kuu ilijadili mambo mengi na hayo ndiyo tunataka umma ufahamu msimamo wetu kama chama.”
Habari ambazo zimelifikia gazeti hili zinasema
katika mkutano huo, huenda uongozi wa Chadema ukaweka wazi “makosa
mengine” ambayo Zitto anadaiwa kuwa amewahi kuyafanya na kuonywa katika
vikao vya ndani ikiwa ni pamoja na kiongozi huyo kutofika makao makuu ya
chama hicho kwa zaidi ya miezi sita. “Kuna makosa mengi (Zitto)
ameyafanya yenye sura ya kukiumiza chama chetu na alionywa mara nyingi
tu, tena na vikao vya juu vya chama kuhusu mwenendo wake, lakini
aliendelea na uasi.Sasa Kamati Kuu imechoka,” alisema mmoja wa maofisa
wa Chadema Makao Makuu.
Habari zaidi zinasema katika mkutano wake wa leo,
chama hicho kitatoa ufafanuzi kuhusu mikutano yote ya kichama ambayo
imekuwa ikifanywa na Zitto, huku kukiwa na hoja kwamba alikuwa akifanya
hivyo bila kuwashirikisha maofisa wa makao makuu wala sekretarieti
ambayo kimsingi ndiyo inapaswa kuiandaa.
Wasomi wanena
Akizungumzia mgogoro huo, mtaalamu wa mambo ya
siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda
alisema hali inayoendelea ndani ya Chadema ni matokeo ya vyama vya siasa
kutofanya kazi kama taasisi.
“Misingi ya vyama haiweki wazi misingi ya watu
kuwa viongozi. Kwa mfano, kesho nikitaka kujiunga na Chadema nitaweza
kuwa Mwenyekiti? Misingi ya wazi hakuna,” alisema Mbunda.
Alisema hali ilivyo ndani ya Chadema kwa sasa ni furaha ndani ya
CCM, kwani watu wanaona kuwa chama kilichoonekana kuwa mbadala hakiwezi
hata kushughulikia mambo yake ya ndani.
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo alisema vyama vya siasa ni
watu au kikundi cha watu wenye malengo na mitazamo tofauti.
“Ukisoma huo waraka utaona kuwa unazungumzia
uongozi, upungufu uliopo kwenye uongozi na namna ya kubadili uongozi,
mimi binafsi niseme ieleweke kwamba hata kwenye jumuiya yoyote mambo
haya yapo hasa kwa kuwa walikuwa wanaelekea kwenye uchaguzi,” alisema.
Alisema haoni kwa nini Zitto na Dk Kitila waonekane wahaini kwa kupanga
mikakati yao ambayo walitaka kuitekeleza kupitia uchaguzi.
“Mabadiliko ni jambo la kawaida, hali hii ya
kuwaondoa kwenye nyadhifa zao inawezekana ikawagharimu Chadema na
inaweza kuwagharimu zaidi wakiwafukuza uanachama,” alisema Makulilo.
CREDIT: MWANANCHI
CREDIT: MWANANCHI