SOMA TAARIFA KAMILI ALIYOITOA ZITTO KABWE KWA WAANDISHI WA HABARI
TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA 1. Utangulizi i. Katika...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/11/soma-taarifa-kamili-aliyoitoa-zitto.html
TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA
1. Utangulizi
i. Katika
kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 22 Novemba 2013,
Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi
zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama
iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe
22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk
Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka
unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013.
Ukweli ni
kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za
uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za
kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni
tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa
ndani na nje ya vikao vya chama.
Hitimisho la
tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na
CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama
ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.
ii. Ninatambua
kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka
nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha
CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi
nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na
atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na
chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu
Zipo tuhuma
nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya
vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha
kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama
changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa
1nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.
i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:
● Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
● Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16
katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani,
Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya
kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
● Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
● Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.
ii) Tuhuma
kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni wagombea wetu
kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli
ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga
kura wa Kigoma walivyoamua.
iii) Tuhuma
kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya majimbo
kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM
wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja
na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama nilivyokwisha
kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na
hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba
nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa
tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama
kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila
uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.
iv) Tuhuma
kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli
ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani
na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa
katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa
yote tuliyotembelea. Mwaka 2012
2
baada ya hoja
ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na
operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi.
Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua
matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.
v) Tuhuma
kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama
hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG):
Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa kuwasiliana
kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae. Kwamba
kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na
nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na
nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa
kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:
● Utawala bora
hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama
changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile
zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
● Napenda
kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama
changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu
tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya
siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali
kosa hili ni la nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao Mtakumbuka
kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya
kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa
na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa
kwenye Ilani yetu ya mwaka 20102015. Mtakumbuka kwamba hivi karibuni
Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni
unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma
ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo
kuhusu jambo hili:
● Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge
ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
● Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana
na ukosefu wa
huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama
chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na
kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa,
kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina
mama.
● Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.
3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe Hivi
karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi
ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu
chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu
ya CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa
kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu
haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu
nililalamikia mambo matatu yafuatayo:
i. Kwamba
baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa
chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye
amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu
hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
ii.
Kwa kuwa chama
kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za
kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile
wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
4. Hitimisho
a) Ninatambua
kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na ningewazodoa watu
kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania. Natambua pia
kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya
siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'.
Natambua
kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala
hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na
uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu.
Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue
kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa
mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote
ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.
b) Naomba
wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma
ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi ili
tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania
wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.
c)
Kamamwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi
mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa
niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
d)
Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia.
Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini
wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya
watukuzao siasa majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu
inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima upande wa
demokrasia. Kama alivyopata kunena
mmojayawanasiasamaarufu,'kiwangochajuukabisachauzalendokatika nchi ni
kukubali kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa
chama chetu.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar es Salaam. 24 Novemba, 2013