CUF ITAENDELEA KUSIMAMIA MISINGI YA HAKI NA USAWA

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake kitaendelea kusimamia misingi ya haki na usawa...

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema chama chake kitaendelea kusimamia misingi ya haki na usawa, ili kuhakikisha kuwa kila Mzanzibari anapata haki yake inayostahiki.
 
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara ya chama hicho uliofanyika viwanja vya Kinyasini, jimbo la Chaani.
 
Amesema Chama hicho kitaendelea kuwa mstari wa mbele kudai mamlaka kamili ya Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha kuwa Zanzibar inaongozwa kwa misingi ya haki na usawa, ili  wazanzibari waweze kuamua mambo yao wenyewe bila ya kuingiwa na mamlaka nyengine.
 
Amesifu umakini wa kamati ya Maridhiano yenye wajumbe sita wakiwemo watatu kutoka Chama Cha Mapinduzi na watatu kutoka Chama Cha CUF, na kwamba wajumbe wa kamati hiyo wameonesha uzalendo wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yao.
 
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maridhiano Mzee Hassan Nassor Moyo, amebainisha kuwa mambo yanayodaiwa kutolewa katika orodha ya Muungano sio mageni, kwani yalikuwemo kwenye mamlaka ya Zanzibar kabla ya kuungana na Tanganyika mwaka 1964.
Ameyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na sarafu, mambo ya nje, pamoja na rasilimali ya mafuta na gesi asilia.
 
Mzee Moyo amewasihi  Wazanzibari kuepuka chuki, fitna na ubaguzi, na badala yake waungane kupigania maslahi ya nchi yao.
 
Amepongeza hatua iliyochukuliwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume na mwenzake Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ya kufikia maridhiano ambayo yamewaunganisha Wazanzibari.
 
Nae Mjumbe wa Kamati hiyo ya maridhiano Mansoor Yussuf Himid (CCM), amesema Zanzibar ni ya Wazanzibari wote, na kwamba kila mzanzibari anastahili kupata haki sawa na mwengine.
 
Amesema ataendelea kuungana na Wazanzibari kupigania haki ya Zanzibar ndani ya Muungano, ili iweze kuendesha mambo yake yenyewe, na kuwashajiisha vijana kutorudi nyuma katika kupigania haki hiyo.
 
Akizungumzia kuhusu rasimu ya pili ya katiba inayotarajiwa kuwasilishwa kesho tarehe 30/12/2013 katika viwanja vya Karimjee Dar es Salaam, Mansoor amesema ikiwa rasimu hiyo haitokidhi angalau wastani wa matakwa ya Wazanzibari hawatoikubali, na wataikataa kabisa.
 
“Watu wa mjini huwa tuna wimbo tunasema ‘supu tayari…’ lakini tunasema ikiwa supu hii ya Jaji Warioba itapungua chumvi au pilipili manga tutaiongeza, lakini kama mbaya hailiki tutamuachia mwenyewe supu yake” alidokeza Mansoor.
 
Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ambao wote walikuwepo mkutanoni na kuzungumza ni Abubakar Khamis Bakar (CUF), Ismail Jussa Ladhu (CUF), Eddy Riyami (CCM) na Salim Bimani (CUF).
 
Katika Mkutano huo Mhe. Maalim Seif alikabidhi kadi 459 kwa wanachama wapya walioamua kujiunga cha chama hicho, sambamba na kuweka mawe ya msingi katika matawi matatu mapya ya CUF ndani ya jimbo la Chaani, pamoja na kufungua barza ya vijana, iliyoyopewa jina la barza ya Maalim Seif Sharif Hamad katika kijiji cha Bandamaji Chaani.

Related

OTHER NEWS 29403864276804581

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item