PINDA KWENDA KITETO KUTAFUTA SULUHU YA MAPIGANO
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda leo anakwenda Wilaya ya Kiteto, Arusha kutafuta suluhu ya mapigano baina ya wakulima na wafugaji katika Hif...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/01/pinda-kwenda-kiteto-kutafuta-suluhu-ya.html
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda leo anakwenda Wilaya ya Kiteto,
Arusha kutafuta suluhu ya mapigano baina ya wakulima na wafugaji katika
Hifadhi ya Embroi Murtangosi yaliyosababisha vifo vya watu 10.
Mwandishi wa Habari wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Irene
Bwire alisema jana: “Ni kweli Waziri Mkuu atakwenda kutembelea wilayani
Kiteto ili kuongoza juhudi za kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.”
Polisi waanzisha msako
Maofisa wa Polisi kutoka Makao Makuu ya jeshi hilo
wanaongoza operesheni ya kuwasaka wahusika wa mapigano hayo kwa kutumia
helikopta.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Akili Mpwapwa
alisema msako huo unaongozwa na Kamishna wa Operesheni wa Polisi, Simon
Sirro... “Operesheni inaendelea porini lakini hadi sasa hatujakamata
mtu. Mapigano yanayoendelea Kiteto ni ya kuviziana.”
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Martha Umbulla amezitaka
pande zote kuacha vita na kuwataka waliovamia ardhi ya Kiteto kuondoka
kwa hiari.
Chadema waibana Serikali
Waziri Kivuli wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Rose Kamili ameitaka Serikali kuchukua hatua za haraka kumaliza mgogoro huo.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Kamili alisema
licha ya Bunge kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza migogoro ya
wakulima na wafugaji nchi nzima, hali bado ni tete katika eneo hilo.
Alisema Serikali inatakiwa kujitafakari juu ya
uwezo wake wa kushughulikia matatizo ya haraka, badala ya kuwa mabingwa
wa kushughulika na matokeo ya tatizo.
Mgogoro
Mgogoro huo ulioanza mwaka 2006, unatokana na wafugaji na wakulima kugombea ardhi kwenye eneo la Hifadhi ya Embroi Murtangosi.
Mapigano kati ya pande hizo mbili yamesababisha watu wanaokadiriwa kufikia 30 kuuawa.
Hifadhi hiyo yenye hekta 135,000, ina vyanzo vingi
ya maji na madini ya aina ya chumvi, haitakiwi kuguswa kwa shughuli za
kilimo wala ufugaji.
Wafugaji wanashinikiza utekelezaji wa amri ya
Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, ambayo mwaka 2009 iliwaamuru wakulima
kuondoka katika eneo hilo.
Mwaka 2006, wakulima waliishtaki Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto katika Mahakama ya Wilaya na kushinda kesi.
Halmashauri ilikata rufaa Mahakama Kuu lakini
wakulima waliibuka washindi tena. Ilikata rufaa Mahakama ya Rufani
ambako ilishinda na wakulima walitakiwa kuondoka.
MWANANCHI
MWANANCHI