UTEKAJI MALORI WASABABISHA MAELFU KUKWAMA NZEGA

Baadhi ya abiria na madereva wakiwa katika mgomo wa kuondoa magari katika kijiji cha Ngonho kata ya Miguwa baada ya magari matatu kutek...

Baadhi ya abiria na madereva wakiwa katika mgomo wa kuondoa magari katika kijiji cha Ngonho kata ya Miguwa baada ya magari matatu kutekwa na madereva wake kujeruhiwa vibaya kabla ya kupelekwa katika hospitali ya Nikinga, Igunga.Takribani abiria 3,000 na magari 1,000 yamekwama katika eneo Picha na na Mustapha Kapalata 

Nzega.
Zaidi ya magari 1,000 yamekwama kwenye Barabara Kuu ya Mwanza - Dar es Salaam katika Kijiji cha Ngonho, Kata ya Miguwa, wilayani Nzega, kutokana utekaji wa malori uliofanywa juzi usiku.
Baadhi ya madereva walisema walikutwa na mkasa huo juzi saa nne usiku wakati magari yao yalipotekwa na watu wanaosadikiwa ni majambazi na kuwanyang’anya mali na kisha kuwatendea ukatili wa kuwajeruhi sehemu mbalimbali za miili yao ikiwa ni pamoja na kuwakata masikio na kuwatoboa macho.
Kutokana na tukio hilo, waligoma kuondoa magari yao na kusababisha mabasi ya abiria na malori ya mizigo kukwama wakati abiria wapatao 3,000 wakitaabika kwa kukosa chakula na maji.
Madereva hao waligoma kuondoa magari yao baada ya kukasirishwa na kitendo cha polisi wa Nzega kushindwa kuwasaidia wakati walipotekwa.
Madereva hao wameapa kutoondoa magari hayo hadi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe au Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa watakapofika kwenye eneo hilo ili kusikiliza kilio chao.
Unyama wa watekaji
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Emmanuel Mihayo alisema watu walijeruhiwa vibaya kwenye utekaji huo kwa kukatwa masikio na kutobolewa macho.
Dk Mihayo aliwataja majeruhi hao kuwa ni raia wa Burundi, Herelina Eddy, ambaye alitobolewa macho na hali yake ilikuwa mbaya na alikuwa kwenye maandalizi ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga kwa matibabu zaidi.
Alisema majeruhi wengine wawili wanaendelea vizuri na matibabu katika hospitali hiyo. Majeruhi hao ni Abraham Ismail na Omary Adrian, ambao wote ni wakazi wa Dar es Salaam.
Alisema Adrian alikatwa sikio na shavu pamoja na mkono wa kushoto wakati Ismail alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili.
Polisi watuhumiwa
Mmoja wa madereva waliotekwa, ambaye aliomba jina lake kuhifadhiwa alisema kuwa polisi wa Nzega waliombwa kutoa msaada lakini walikataa.
Dereva huyo alisimulia kuwa mmoja wa madereva alifanikiwa kutoroka wakati walipotekwa na kwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Nzega lakini askari waliokuwepo kituoni hawakutoa ushirikino.
“Polisi hao walitoa visingizio, wakidai kwamba gari lao halina mafuta na walikataa kutumia lori la dereva huyo kwenda kwenye eneo la tukio,” alisimulia dereva.
Baada ya kunyimwa msaada, dereva huyo alilazimika kurudi kwa wenzake ndio akajikuta akitekwa tena.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Peter Ouma, ambaye alifika kwenye eneo la tukio, aliahidi angewachukulia hatua kali polisi hao.
“Nawaahidi ndugu zangu, hawa waliosababisha hali hii wote nawachukulia hatua kali za kinidhamu mara mmoja na taarifa hizi mtazisikia kwenye vyombo vya habari,” aliahidi Kamanda Ouma, huku akiwaomba madereva wa malori na magari ya abiria waendelee na safari zao.
Hata hivyo, madereva hao waligoma kuendelea na safari na badala yake walisisitiza kuwa wanataka askari waliokuwa doria wachukuliwe hatua za kinidhamu.
“Tunalishangaa Jeshi la Polisi, wameshindwa kutusaidia na matukio kama haya yamezidi hapa Nzega tunataka Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani wachukue hatua... hatuondoki mpaka kieleweke,’’ alisema dereva mwingine, ambaye pia aligoma kutaja jina lake.
Madereva hao walisema vitendo vya utekaji magari katika Wilaya ya Nzega, vimekuwa vikitokea mara kwa mara na kuhatarisha maisha ya watu, magari na mali zao.
“Hivi mbona tukiendesha magari haya na kwenda nchi za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hatupati matatizo haya ya kutekwa,” alihoji dereva mwingine.
Mateso kwa abiria
Kutwa nzima jana, mabasi na magari madogo yalikwama katika eneo hilo na kusababisha foleni kubwa, hivyo kusababisha adha kwa wasafiri, hasa wanawake na watoto.
Kutokana na hali hiyo, wachuuzi wa bidhaa mbalimbali walitumia fursa hiyo kujineemesha kwa kuuza vitu kwa bei ya juu, ambapo chupa ya maji ya kunywa nusu lita iliuzwa Sh1,000 badala ya Sh500 wakati ile ya lita moja Sh2,000 badala ya Sh1,000.

 Aina zote za soda ziliuzwa Sh2,000 badala ya kati ya Sh600 hadi 1,000 wakati sahani moja ya chakula kwa mamalishe iliuzwa kati ya Sh3,000 na Sh5,000.

Mmoja wa abiria alionekana akilalamika na kutoa maneno makali ya kuwashutumu madereva kwa kuwasababisha adha hiyo pamoja na Serikali kushindwa kuwasaidia.
“Sisi tunataabika, hatuna msaada. Watoto wetu wanateseka, wengi wetu tumeishiwa, hatuna fedha,” alilalamika Mariamu Majara, abiria aliyekuwa akisafiria kwenye basi la Kajumulo lililotoka Mwanza kwenda Dar es Salaam.
Taarifa ambazo zililifikia gazeti hili jioni zilisema, mgomo huo ulimalizika na mabasi kuanza kuondoka saa 1:30 usiku.

MWANANCHI.

Related

OTHER NEWS 7674848825524616953

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item