TANZANIA YASISITIZA NYONGEZA YA POSHO KWA WALINZI WA AMANI WA UMOJA WA MATAIFA

Na Mwandishi Maalum, New York Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  imesema, posho ya dola 1.28  kwa siku wanayolipwa walinzi wa amani wan...

Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  imesema, posho ya dola 1.28  kwa siku wanayolipwa walinzi wa amani wanaohudumu katika Misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa,  hailingani na  mazingira magumu  na hatari ya utekelezaji wa mamlaka wanayokabidhiwa na Umoja wa Mataifa.  

Na kwa sababu hiyo na kwa zingatia hali halisi,  Tanzania  imesisiza kwamba,  wakati umefika sasa wa kuangalia upya posho hiyo ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 20.

Balozi Tuvako Manongi, Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania katika Umoja wa mataifa,  ametoa rai hiyo  mwanzo mwa  mkutano wa Kamati   Maalum  ya      Usimamizi wa  Operesheni za Ulinzi wa Amani maarufu kama C-34.

Kamati hii ambayo wajumbe wake ni kutoka nchi zinazochangia walinzi wa Amani katika misheni mbalimbali za kulinda  amani,  imeanza mkutano wake wa  mwezi mmoja hapa  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo  wajumbe watajadili  mambo yote yanayohusu sera za ulinzi wa Amani  chini ya Umoja wa Mataifa.

Balozi Manongi amewaeleza wajumbe wa mkutano huo  kwamba   Kamati   ilikuwa inaanza mkutano wake,  wakati ambapo ,  operesheni za ulinzi wa amani  zinakabiliwa na  changamoto mbalimbali zikiwamo za malipo duni.

“ Tunaposhindwa kukubaliana kujadili hoja ya  kuongeza kiwango cha posho ya kila siku kwa walinzi wa amani,  posho  ambayo  imebaki  dola 1.28 kwa zaidi ya miaka 20, siyo tu kwamba tumewaangusha walinzi wa amani,  bali pia tunawavunja moyo na kuwakatisha tamaa katika utekelezaji wa majukumu yao”. akasisitiza Balozi  Manongi.

Akasema waeleza wajumbe    licha ya  malipo duni na mazingira magumu, walinzi hao wanajitolea uhai wao kwaajili  ya watu wengine na kwamba,kutokana  umuhimu wao , Umoja wa Mataifa  umejikuta  ukilazimika kuwapeleka katika Misheni ambazo ama hakuna amani ya kulinda au  mahali ambako kuna  vikundi vingi vyenye silaha vinavyokinzana.

“Hii ndiyo hali halisi inayozikabili Misheni zetu zote  katika  utekelezi wa mamlaka  tunazokabidhiwa na Umoja wa Mataifa. Inasikitisha  na kukatisha tamaa pale baadhi yetu tunaposisitiza kwamba Misheni mpya inayoundwa au kuongezewa mamlaka itekeleze mamlaka hayo kwa kuzingatia rasilimali zilizopo, ili hali tunafahamu wazi kwamba rasilimali zinazozungumzwa  ama hazipo au hazikidhi hali halisi ya  Misheni hizo”. Akabainisha Balozi Manongi.



Na kuongeza. “Ni vema tukaunganisha nguvu zetu kukabiliana na  changamoto hizi na nyingine nyingi ili  walinzi wa amani  ambao wanategemewa  sana waweze kusaidia katika ulinzi wa amani kwa raia wasiokuwa na hatia, lakini pia  kujihakikishia usalama wao wenyewe.

Akaeleza kwamba  ni matumaini ya Tanzania kuwa  hoja ya  kuongezwa kwa posho  hiyo   pamoja na nyongeza ya  malipo ya vifaa itapewa umuhimu na kujadiliwa ipasavyo katika mkutano ujao wa Kamati ya Tano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya   Utawala na Bajeti ya Umoja wa Mataifa.

Pamoja na  changamoto hizo,  Muwakilishi  huyo wa Tanzania, ameuhakikishia  Umoja wa Mataifa  kwamba,  Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuwajibika kwa kushiriki katika operesheni za ulinzi wa Amani  kwa  mujibu wa Mamlaka inayokabidhiwa na  Umoja wa Mataifa.

“ Tumedhamiria na tunajivunia ushiriki wetu wa ulinzi wa Amani katika  maeneo mbalimbali ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako  tunashiriki  kupitia Misheni ya Kulinda Amani katika DRC ( MONUSCO). Misheni ambayo ndani yake  kuna  Force  Intervention Brigade ( FIB)”.

Vile vile  akabainisha kwamba  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  itaendelea  kushiriki kikamilifu katika  utekelezaji wa  Mpango  Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa, kuhusu Ulinzi, Usalama na   Ushirikiano wa  Ki- maendeleo katika DRC na  eneo la  Maziwa Makuu.

Akizungumzia  zaidi kuhusu Misheni  ya MONUSCO na mchango wake katika  usimamizi wa amani  katika DRC. Balozi Tuvako Manongi amesema, Tanzania inaamini   kwamba utendaji kazi wa Misheni hiyo  unasimama katika  misingi ya  Misheni Moja,  Jeshi Moja,  Nguvu  Moja ya Mamlaka,  kuwa  ndiyo  mweleko sahihi na wenye tija  katika ngazi zote  kiutendaji.

Misheni ya MONUSCO  inaundwa na walinzi wa Amani  kwa upande mmoja kutoka Pakistani, India na  Bangladeshi pamoja na  Tanzania,  Afrika ya Kusini na Malawi kupitia FIB.

Aidha,   Muwakilishi wa  Tanzania katika Umoja wa Mataifa,  amezitaka Mamlaka za Jamhuri ya  Kidemokrasia ya Kongo,  kutumia  mafanikio yaliyopatikana hivi karibuni, kuimarisha  taasisi zake za  kisiasa, kiulinzi , kiuchumi   pamoja na kuongeza kasi ya  majadiliano na  maridhiano.


 Baadhi ya  Waambata wa Kijeshi wanaoziwakilisha nchi zao
 Katika Umoja wa Mataifa, wakiwa  katika  picha ya pamoja muda mfupi kabla ya  ufunguzi wa Mkutano wa Mwezi mmoja wa Kamati Maalum ya Usimamizi wa Operesheni za Kulinda  Amani.    Katika Mkutano huu wajumbe ambazo ni kutoka  nchi ambazo zinachangia walinzi wa amani watajadili sera zote zinazohusu ulinzi wa amani chini  ya  Umoja wa Mataifa.

Related

OTHER NEWS 1234740917991929307

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item