WASAFIRISHAJI WA DAWA ZA KULEVYA WAJA NA MBINU MPYA, SOMA HAPA

Dar es Salaam.   Wasafirishaji wa dawa za kulevya wamebuni mbinu mpya baada ya Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ...



Dar es Salaam. 
Wasafirishaji wa dawa za kulevya wamebuni mbinu mpya baada ya Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kukamata kilo 3.5 za heroini zikiwa zimefungwa kwenye vifurushi zikipelekwa Monrovia, Liberia.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Kikosi cha Wanamaji cha Polisi kukamata jahazi likiwa na kilo 201 za heroini wakati likisafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Mkuu wa Upelelezi wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Hamad Hamad alisema jana kuwa kifurushi hicho kilikamatwa Jumatatu saa tisa alasiri, kwenye uwanja huo.

Hamad alisema mmiliki wa kifurushi hicho kilichokuwa kinasafirishwa na Kampuni ya Kusafirisha na Kupokea Mizigo (DHL) hajafahamika.
Kwa mujibu wa Hamad, mmiliki wa mzigo huo alikuwa ametumia jina la bandia pia maelezo ya mzigo ule yalikuwa ya uongo.

Hamad alisema dawa hizo zilikuwa zimeingizwa ndani ya kandambili huku zikiwa na vifurushi vingine kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Liberia.
“Kampuni ya DHL walipewa kazi ya kusafirisha mzigo huo na kujitetea kuwa hawakuelewa kulikuwa kitu ndani,” alieleza Hamad.

Hamad alisema kuwa polisi waliutilia shaka mzigo ule wakati ukipitishwa na kuamua kuukagua, ndipo wakakuta ni heroini.
Katika hatua nyingine, Kamishna wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema bado wanaendelea kuwahoji watu 12 raia wa nchi za Iran na Pakistan waliokamatwa juzi na kilo 201 za heroini.

Alisema pia wanaendelea kumchunguza raia wa Kenya, Abdulrahman Salim, ambaye alikamatwa na kete 142 za dawa za kulevya aina ya cocaine kwenye Uwanja wa JNIA.
Salim alikamatwa akitokea Brazil akiwa amepanda ndege ya Shirika la Ndege Ethiopia.
Mbinu zaidi

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ameelezea mbinu mbalimbali zilizobuniwa na wasafirishaji wa dawa za kulevya, zilizobainika baada ya watu saba walikamatwa katika matukio saba tofauti.
Dk Tizeba alisema hata vitabu vimekuwa vikitumika ambapo wahusika wamekuwa wakikata katikati ya vitabu hivyo na kuweka kete za dawa za kulevya kabla hawajavisafirisha nje ya nchi. Hata hivyo jambo hilo sasa wamelishtukia na udhibiti umeongezwa katika viwanja vya ndege.

“Hivi karibuni tumekamata kitabu cha somo la baiolojia kikisafirishwa kwenda Liberia na kilitiliwa shaka na kilipofunguliwa kilikutwa na kilo mbili za dawa za kulevya,” alisema.
Alisema wameamua kusafarisha kwa njia hiyo baada ya kuona mpango wa kumeza umedhibitiwa na hadi sasa wahusika wa matukio hayo saba wamekamatwa, na mmoja bado ila huenda akatiwa mbaroni wakati wowote.
“Saba tunao kwa mahojiano na mwingine ambaye anahusika na kitabu hicho cha baiologia anafuatiliwa,” alisema.

Related

OTHER NEWS 4829864376374946662

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item