BUNGE LA KATIBA: SASA NI KURA MSETO
Hatimaye Bunge Maalumu la Katiba limeridhia wajumbe kupiga kura ya wazi na siri katika kupitia mchakato wa rasimu ya katiba mpya. ...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/03/bunge-la-katiba-sasa-ni-kura-mseto.html
Hatimaye
Bunge Maalumu la Katiba limeridhia wajumbe kupiga kura ya wazi na siri
katika kupitia mchakato wa rasimu ya katiba mpya.
Maamuzi hayo
yalitolewa jana jioni baada ya Kamati ya Maridhiano iliyokutana kuanzia
juzi usiku hadi jana mchana kukubaliana kuwa na kura za aina mbili,
kufuatia mvutano mkubwa ulioibuka baina ya wajumbe hao.
Mwenyekiti
wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, aliamua kuunda kamati hiyo
baada ya mapendekezo kutokana na michango iliyotolewa na wajumbe katika
mjadala wa juzi, ambapo Freeman Mbowe, alikuwa mmoja wa wajumbe waliotoa
hoja hiyo.
Sitta
aliunda kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim
LIpumba, Askofu (mstaafu) Donald Mtetemela na Vuai Ali Vuai.
Kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo, Sitta aliwaruhusu wanakamati hiyo kila mmoja kutoa yale waliyoamua.
Akiongea kwa
niaba ya Mbowe, Johna Mnyika alisema mazungumzo yamesaidia kupiga
hatua moja mbele ingawa ya kukubaliana kutokubaliana.
“Sisi
tulikuwa na mtazamo kuwa kura iwe ya siri lakini wengine walitaka kura
ya wazi. Pamoja na majadiliano yote wenzetu waliona wana uhuru wa kupiga
kura ya wazi, ilibidi tufike hatua ya kuamua kulivusha taifa ili
lisonge mbele.”
Alisema walipendekeza maamuzi haya yafanywe kwa kura ya wazi lakini wao waliamua yafanyike kwa siri.
Alisema
wameamua anayetaka kupiga kura ya wazi apige ya wazi na atakayeamua ya
siri iwe ya siri. Matokeo yatakayopatikana kwa minajili ya kupiga hatua
moja mbele na kulisogeza taifa mbele.
“Wenye
kukubaliana na kura ya wazi watakuwa wengi, na wanaotaka kura ya siri
watasema hapana na kwa vyovyote walio wengi watashinda,”
Alisema utaratibu huu wa mashauriano ni vizuri utumike hata pale ambapo hawakubaliani ili kupiga hatua mbele.
“Sisi hatuna
njama zozote za kuvuruga bunge hili kwa sababu tumepigania sana jambo
hili na kutaka Watanzania wapate Katiba iliyo bora,” alisema.
Alisema wapinzani hawana dhamira ya kukwamisha mchakato wa Katiba. “Kwa sababu kuna magazeti yamemnukuu Mheshimiwa Rais …
PROFESA IBRAHIM LIPUMBA
Alisema
unapofanya mchanganyiko wa kura ya wazi na siri ni kuwafanya wale
wanaotaka kura ya siri kutopata haki yao lakini Ili tusonge mbele na
kuanza kujadili Rasimu ya Katiba, tupige kura ya wazi na siri tufanya
maamuzi.
Lakini hii
si kura nzuri ni kura itakayotupa vikwazo. “Mimi binafsi ntasema hapana
kwa jambo ambalo limeletwa juu ya meza kulifanyia maamuzi. Lakini ili
tusonge mbele tumeona tulifanyie maamuzi hayo.
“Natoa wito
kwa CCM pamoja na kuwa wengi ni vyema kuheshimu mawazo ya wachache “,
alisema na kuongeza kuwa CCM wangekuwa na busara wangeweza kuongeza
idadi ya kamati kwa kuweka mbele ya Watanzania.
VUAI ALI VUAI
Sisi kwa
upande wetu tulikuwa na msimamo wa wazi na wenzetu walikuwa na msimamo
wa siri. Sisi tuliotoka CCM tulikubali twende na mifumo yote miwili.
Wale watakaokuwa tayari kupiga kura ya wazi wapewe haki yao ya wazi bila
vikwazo na siri hivyo hivyo,
CCM itakuwa ya mwisho kusitisha mchakato wa Katiba, matakwa yetu ilikuwa ni kura ya wazi ili tufanye maamuzi tukiwa tunaonekana.
“Tulichotoka nacho kule ndani tunakwenda na kura ya siri kwa wanaotakana na kura ya wazi kwa wanaotaka,” alisema.
ASKOFU (mstaafu) DONALD MTETEMELA
Kila mmoja
ana haki ya kuwa na msimamo au wazo lake ila wananapaswa kuheshimu jambo
lililowaleta hapa ndani ya bunge na kukubali kutoa tofauti zao kwa
mashauriano ili mchakato huo uendelee.
Wajumbe
warudi kwenye azimio la kamati juu ya upigaji kura kwani tumekuwa
tukijadili suala la kanuni hadi sasa ni siku 40 na hatujaanza kazi
ambayo tulikuja kuifanya. Siku zimekwisha tusiongeze nyingine kwa kuleta
hali ya kutofautiana. Tusinga’ng’anie kila kitu ni hapana na
kung’ang’ania misimamo yetu. Tusonge mbele ili kutimiza lengo la kupata
Katiba mpya.
KURA YAPIGWA KUPITISHA AZIMIO
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Pandu Ameir Kificho, alitangaza
wajumbe hao kupiga kura ili kupitisha azimio hilo la kupiga kura ya wazi
na siri.
Kura hizo ndizo zitakazotumika kwenye vikao vya kamati kwa ajili ya kujadili rasimu ya katiba.
Mwenyekiti
wa Bunge Maalum la Katiba, Sitta, alimtaka Katibu wa Bunge , Yahaya
Khamis Hamad, kutangaza utaratibu wa wajumbe kupiga kura ambapo alisema
kila mjumbe ataitwa jina mmoja mmoja, kutamka “ndiyo” au “hapana” kwa
wale waliamua kupiga kura ya wazi.
Aidha, kwa wale walioamua kupiga kura ya siri watakwenda mbele na kutumbukiza kura zao za siri kwenye masanduku ya kura.
Hadi
tunakwenda mitamboni wajumbe walikuwa wanaendelea kupiga kura na baadhi
walipiga ya wazi kukataa wakisema hapana. Wengine walipiga kura ya wazi
kukubali wakisema ndiyo.
Hadi wakati
huo wajumbe wote wa CCM walipiga kura ya wazi kwa kusema ndiyo, wakati
wajumbe wa Chadema na CUF walipiga kura ya wazi ya kukataa wakisema
hapana hali iliyoonyesha misimamo dhahiri ya kichama .
Miongoni mwa
waliopiga kura ya wazi ya hapana ni Waziri wa Sheria na Katiba wa
Zanzibar, Abubakar Khamis, Profesa Ibrahim Lipumba, Juma Haji Duni na
kwa upande wa wajumbe wa CCM waliosema hapana kwa azimio hilo ni pamoja
na Deo Filikunjombe, wakati mjumbe wa Chadema Godbless Lema , hakusema
neno na hakupiga kura kwenye karatasi.