FOLENI YA MAGARI YAZUA MARADHI MAPYA, SOMA HAPA KUFAHAMU ZAIDI
Dar es Salaam. Wakati kukiwa na ongezeko kubwa la ununuzi wa magari na kusababisha idadi kubwa ya vyombo hivyo vya usafiri, foleni...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/03/foleni-ya-magari-yazua-maradhi-mapya.html
Dar es Salaam.
Wakati kukiwa na ongezeko kubwa la ununuzi wa
magari na kusababisha idadi kubwa ya vyombo hivyo vya usafiri, foleni za
magari nchini, hasa jijini Dar es Salaam, imefikia hatua ya kutisha
huku ikisababisha madhara makubwa kiuchumi, kijamii na kiafya, ikiwamo
magonjwa ya akili.
Misululu ya magari ilikuwa ni ya kawaida kuonekana
nyakati za asubuhi na jioni wakati watu wakielekea na kutoka kazini,
lakini sasa foleni zimekuwa ni za kawaida katikati ya jiji na maeneo
mengine ambayo ukarabati wa barabara unaendelea wakati wote.
Wakati kukiwa na kasi ndogo ya ukarabati wa
miundombinu ya usafiri, kumekuwa na ongezeko kubwa la magari jijini Dar
es Salaam. Pia kumekuwapo na ongezeko kubwa la idadi ya watu hadi
kufikia milioni 4.3 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002 huku vyombo vya
usafiri wa umma (daladala) vikitumia njia zisizo sahihi (kutanua),
kufanya foleni kuwa kubwa hali inayosababisha jiji kuwa kero kwa muda
wote.
Licha ya jitihada za Serikali kutumia treni
kusafirisha abiria ili kusaidia kupunguza msongamano wa magari nyakati
za asubuhi na jioni, bado tatizo hilo ni kubwa. Hivi karibuni Waziri wa
Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuri aliagiza Kampuni ya Strabag, inayojenga
miundombinu ya mabasi yaendayo kasi, kufungua barabara zilizokamilika
ili kupunguza msongamano.
Kutokana na tatizo hilo, wakazi wa Dar es Salaam
na maeneo mengine yanayoathiriwa na foleni, wamekuwa wakilazimika ama
kusitisha safari au kuchelewa kazini na kwenye shughuli nyingine, huku
vyombo vya usafiri vikilazimisha kufanya safari chache na hivyo wamiliki
kupata fedha kidogo kuliko matarajio yao.
“Madereva wanapata magonjwa ya akili kutokana na
kero za barabarani,” alisema Dk. Innocent Godman, ambaye ni mmoja wa
wataalamu wa nyanja tofauti aliyeongea na gazeti hili kuhusu tatizo
hilo.
“Kwanza ni msongo wa mawazo kuhusu uchumi kutokana
na mafuta mengi kupotea njiani; pili barabara mbovu; tatu hasira za
kuchelewa anakokwenda; na nne wanakumbana na askari wa usalama
barabarani ambao wanawakamua fedha,” alisema mtaalamu huyo wa magonjwa
ya akili na mshauri nasaha kuhusu utumiaji wa madawa ya kulevya.
Tanzania inaelezwa ni nchi inayoongoza kwa kuwa na msongamano mkubwa wa magari katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Zatafuna mabilioni ya shilingi
Katika utafiti wake, Wakala wa Mradi wa Mabasi ya
Kasi (DART), Jumbe Katala amebaini kuwa foleni husababisha ajali za
barabarani, upotevu wa nishati (mafuta) na muda wa kukaa barabarani
mambo ambayo husababisha hasara ya zaidi ya Sh655 bilioni kwa mwaka.
Katika utafiti huo, Katala alibaini kuwa foleni
hizo husababisha kudorora kwa uchumi, huku bei ya mafuta ipanda kutokana
na mahitaji ya nishati hiyo kuongezeka.
Alisema kuendesha na kuzima gari mara kwa mara kwa
sababu ya foleni huongeza matumizi makubwa ya gari na kuongeza kasi ya
uchakavu wake, hivyo kusababisha gharama kubwa za matengenezo ya mara
kwa mara.
Madhara kiafya
Kiafya, foleni pia zinatajwa kusababisha maradhi
lukuki yakiwamo magonjwa ya akili, pumu, maradhi ya mfumo wa hewa, mzio
utokanao na mafuta na maradhi ya moyo.
Msongamano wa magari pia husababisha wasafiri hasa
madereva kuvuta hewa chafu itokanayo na mafuta ya magari na maradhi ya
mfumo wa hewa kutokana na kutovuta hewa safi. Dk. Godman alisema
madereva wengi wa Tanzania wana magonjwa ya akili kutokana na sababu
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na foleni.
“Madereva wanapata zaidi ya magonjwa ya akili hata
mara mia moja zaidi,” alisema Dk. Godman. Dk. Godman alisema msongo wa
mawazo unaotokana na adha za usafiri nchini umewaathiri watu wengi na
kusababisha wawe na lugha chafu, hasira za mara kwa mara na uongo.
“Foleni za magari kwa hapa nchini ni zaidi ya janga kwa sababu unaathiri
kila sekta ya maisha,” alifafanua.
Kutokana na utafiti huo, madereva wengi wanaofanya
kazi katika maeneo hayo, hasa katika mabasi ya mijini (daladala) kwa
muda mrefu, wanatajwa kuwa katika hatari ya kupata maradhi ya akili
kutokana na kuwa na msongo kwa kipindi kirefu.
“Wengi wao wanavuta bangi, halafu wakichanganya
foleni ya barabarani na ugumu wa maisha, huo ni ugonjwa wa akili,”
alisema. Wanasayansi wanautaja ugonjwa huo kwa kitaalamu kuwa ni
‘maradhi ya msongo wa foleni’ (Traffic Stress Syndrome).
Kuvunja ndoa
Wataalamu wa masuala ya kijamii wanaeleza kuwa
madereva na abiria wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenye foleni na
kusababisha kupoteza muda ambao wangeutumia kwenye uzalishaji.
Kutokana na hali hiyo, bila takwimu wanasema
abiria hao wengi hulazimika kusema uongo kwa kuchelewa katika mikutano
ya kikazi, elimu, biashara na wakati mwingine watu kuadhibiwa kwa
kuchelewa maofisini na majumbani, jambo linalosababisha kuyumba kwa
ndoa.
Hasara zaidi
Mhadhiri wa Uchumi, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Haji Semboja anachanganua hasara ya msongamano katika
mtazamo wa upotevu wa muda na mafuta.
Anasema, iwapo magari yatachukua muda mrefu kufika
eneo moja, basi hata bidhaa zitapanda bei, kwa sababu mafuta mengi
yanatumika njiani. “Chombo cha moto kilichotumia dakika kumi, si sawa na
kilichotumia saa nzima, ukijumlisha hasara ya mafuta ni sawa na kujenga
barabara zote hapa nchini,” alisema.
Profesa Semboja alisema kuwa msongamano wa magari unachangia
kuwapo uzembe kazini na sasa imekuwa kawaida mtu kusingizia kachelewa
kazini kwa sababu ya foleni.
“Jambo la muhimu ni kutafuta kiini cha tatizo,
mfumo wa barabara ambao hauendani na mfumo wa maji, makazi, biashara,
maisha na ofisi,” alisema.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Greyson Lwenge
alisema hakuna ubishi kuwa foleni zinasababisha hasara, hasa ya utumiaji
mkubwa wa mafuta na muda unaopotezwa kwenye foleni barabarani.
“Kwa hali ya kawaida foleni ni hasara, mahali pa
dakika 10 unatumia nusu saa au wakati mwingine saa nzima. Ndiyo maana
tumekuja na miradi hiyo ili kupunguza msongamano,” alisema Waziri
Lwenge.
Hata hivyo, Waziri Lwenge alisema Serikali
imejipanga vyema na mradi wa mabasi yaendayo kasi, Daraja la Kigamboni,
barabara za juu na upanuzi wa barabara kuu ili kupunguza msongamano wa
magari.
MWANANCHI
MWANANCHI