HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA JOSEPH O. MBILINYI (MB) KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015 (Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za Bunge toleo la mwaka 2013)

0.1 UTANGULIZI Mheshimiwa Spika, napenda kuchuku nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema na kwa kunitumia kama chombo ...

0.1 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, napenda kuchuku nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa afya njema na kwa kunitumia kama chombo cha mabadiliko hasa katika kutetea haki za wanahabari, vijana, wanamichezo na wasanii. Namshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Mhe. Freeman A. Mbowe kwa kuendelea kuwa na imani nami katika kuisimamia Serikali katika wizara hii. Aidha, napongeza hatua ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuungana kwa pamoja kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania. Napongeza UKAWA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwaelimisha wananchi nchi nzima. Napenda kuchukua nafasi hii kutoa salamu za rambirambi kwa wasanii nchini kwa vifo vya waigizaji Adam Kuambiana na Rachel Haule vilivyotokea hivi karibuni. Mungu azilaze Roho za Marehemu mahali pema peponi. Amen.
Mheshimiwa Spika naomba kuanza hotuba hii kwa kumnukuu kwa kirefu mmoja wa viongozi wetu ambao wamejipambanua kwa namna ambayo wanastahili sifa za kuitwa ‘statesmen’, mtu huyu si mwingine bali ni Jaji Mark Bomani, ambaye hivi karibuni wakati akitoa hotuba kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo Duniani, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema;
Inasikitisha kuona kuwa hali ya Mtanzania inazidi kudidimia au kubaki pale pale katika sehemu nyingi hasa vijijini katika kipindi cha miaka 40 iliyopita kwa kukosa fursa muhimu za maendeleo na viongozi hawalioni hilo.”
Vyombo vya habari vilimnukuu zaidi Jaji Bomani akisema “nchi itaendeshwa kwa kusimamia haki na ukweli na kuwataka wanahabari wasichoke kuisimamia haki na uhuru wa nchi yao bila woga kwani bila kufanya hivyo nchi itaongozwa kiimla.
“Ni aibu kuona mswaada wa sheria ya habari umekwama kwa zaidi ya miaka 10 kwa sababu ambazo hadi leo hazijaeleweka.”

Akawataka waandishi wa habari,
“wasikate tamaa na badala yake waendelee na kupambana kuhakikisha kwamba harakati za kupata Sheria ya Haki ya Kujua inafanikiwa ili kupunguza matukio ya manyanyaso, kupigwa, kuteswa, kufungwa kwa vyombo vya habari na kuuwawa.”
“Haki haiombwi simamieni haki zenu na songeni mbele.”
2.0          MAENDELEO YA SEKTA YA HABARI NCHINI
2.1 Miaka 10 ya mapambano na ahadi za uongo uliofika ngazi ya kimataifa
Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kuzungumzia vyombo vya habari. Kwanza napenda kuvishukuru kwa kazi kubwa inayofanywa na ‘mhimili’ huu usio rasmi katika kuimarisha demokrasia na kupigania umuhimu wa uongozi nchini kwetu.
Vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele kuibua na kuweka bayana vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na matumizi mabaya ya madaraka licha ya sheria mbaya na kandamizi ambazo zinaendelea kuminya uhuru wa habari na haki ya kupata habari kwa wanahabari na wananchi kwa ujumla.
Mheshmiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Kambi ya Upinzani Bungeni tumezungumza kwa kirefu, tukishauri, kutoa angalizo, kuonya na kuelekeza kwa mapana na marefu kuhusu kufuta sheria kandamizi zilizopo zinazominya uhuru wa habari na kupata taarifa na badala yake zitungwe sheria zingine ambazo zitaimarisha uhuru huo na kusaidia kukomaza demokrasia nchini. Mapambano haya ya wananchi kupigania uwepo wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na Haki ya Kupata Habari si ya leo. Yameanza tangu mwaka 2007.
Mheshimiwa Spika, katika namna ya kipekee ambayo ilipaswa kuungwa mkono na serikali hii kama ingelikuwa ni sikivu, wadau wa habari kwa jitihada za kulisaidia taifa lao, walichukua jukumu la kukusanya mawazo na mapendekezo ya wadau mbalimbali wa habari kuhusu namna ya kuboresha miswada ambayo ilikuwa imeandaliwa na serikali. Mapendekezo hayo yaliwasilishwa serikalini tangu mwaka 2007 kwa sheria ya Haki ya Kupata habari na 2008 kwa sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.
Hatuna haja ya kurudia kusema juu ya danadana ambazo Serikali hii ya CCM imezifanya tangu wakati huo hadi sasa nchi imeshindwa kuwa na sheria nzuri kama ilivyopendekezwa na wadau.  Mwaka jana wananchi walifarijika walipomsikia Rais Jakaya Kikwete akitoa ahadi kwa maneno mazito mbele ya mkutano wa kimataifa kuwa serikali ingeleta muswada wa Sheria wa Haki ya kupata Taarifa ifikapo mwezi Aprili mwaka huu!
Mheshimiwa Spika, Rais Kikwete alikuwa akihutubia Mkutano wa Kimataifa wa Serikali Uwazi ulioitishwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroun ambao ulijadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwazi katika manunuzi ya umma, uwazi katika mikataba, haki ya kupata habari, uwazi katika ukaguzi wa fedha za umma, uwazi wa Serikali na vyombo vya habari, uwazi katika mikataba ya maliasili, uwazi katika maendeleo ya nchi zinazoendelea.
Akizungumza kwenye mkutano huo Alhamis ya Oktoba 31, Rais Kikwete si tu kwamba aliwaahidi Watanzania bali pia alitumia jukwaa hilo la kimataifa kuitangazia dunia nzima kuwa Serikali yake tayari inafanyia kazi utungaji wa Sheria ya Kupata Taarifa, kwa ajili ya kuwapatia wananchi haki ya kupata taarifa kutoka serikalini.
Vyombo vya habari mbalimbali, vya ndani na nje ya nchi, vilimnukuu Rais Kikwete akitoa ahadi hiyo, kwa kusema; 
"Kama watu wanataka kupata taarifa kuhusu namna gani dawa zinagawanywa, kama wanataka kupata taarifa kuhusu bajeti za shule zao za msingi, wanastahili kuwa na haki ya kuzipata. Kama watu wanataka kupata taarifa kuhusu lini watasambaziwa maji wanapaswa kuwa na haki hiyo. Pale watu wanapotaka kupata taarifa, haipaswi kuonekana kuwa wanaingia mahali ambapo hapawahusu.”
Gazeti la The Guardian likiandika kuhusu ahadi hiyo ya Serikali ya CCM, lilisema hivi;
Ahadi hii inawakilisha moja ya hatua kubwa kuelekea haki ya kupata taarifa na suala la Serikali Uwazi nchini Tanzania. Hata hivyo, kama ilivyo ada siku zote, jaribio halisi litakuwa ni katika utekelezaji (wa ahadi hiyo).”
Watu wengi hawajui kuwa kabla ya kutoa ahadi hiyo nchini Uingereza ambako Rais Kikwete aliitangazia dunia kuwa Tanzania itatunga sheria ya uhuru wa habari na kupata taarifa yenye viwango vya kimataifa, pia aliwahi kutoa ahadi ya namna hiyo hiyo kwenye mkutano kama huo, nchini Brazil mwaka mmoja kabla ambako alisema hivi;
“Ninaahidi kuwa tutafanya kadri ya uwezo wetu wote kutimiza matarajio ya ushirikiano huu ili kuhamasisha uwazi na uwajibikaji wa serikali yetu kwa wananchi wa Tanzania. Napenda kuwahakikishia kwamba utashi wetu wa kisiasa kufanikisha malengo ya OGP hayatakwama kwa sababu dhana ya Serikali Uwazi iko kwenye moyo wa mkataba kati ya dola na wananchi.”
Mwandishi katika Gazeti hilo la The Guardian akamalizia kwa kusema
“Je Tanzania inaweza kusimama imara kutekeleza maneno haya mazito?”
Swali hilo linaweza kujibiwa na viongozi wa Serikali hii ya CCM ambao sasa si kwamba wanaweza kutoa ahadi za papo kwa papo za kuwahadaa Watanzania pekee, bali sasa wamevuka mipaka ya nchi na kutoa ahadi za uongo dunia nzima ikiwasikiliza.  Si tu kwamba hawaoni tatizo kuahidi, bali sasa hawaoni shida hata kutotekeleza kila wanachoahidi. Hii ni dalili ya wazi ya ukosefu wa dhamira na uwezo wa kukidhi matarajio ya watu.
Mheshimiwa Spika, katika hali ambayo kwa kweli wadau wa habari nchin wanapaswa kuanza kumjua adui yao halisi kwenye mapambano ya kupata sheria hizi mbili muhimu, ni kitendo cha CCM kupitia kwenye vikao vyake vya ndani kutoa maelekezo kwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na chama hicho na washirika wake, ambayo kwa ujumla yanapingana na dhana nzima ya uwepo wa sheria hizo.
Katika waraka wake wa siri ambao umeripotiwa mara kadhaa na vyombo mbalimbali vya habari, CCM imeamua kujiandikia rasimu nyingine ambayo chama hicho ndiyo kinataka eti Katiba Mpya ya nchi. Katika nyaraka hiyo, vikao vya CCM ambavyo vinaongozwa na Mwenyekii wake Jakaya Kikwete, kimepinga dhana za uwazi, uadilifu na uwajibikaji kama ambavyo zimependekezwa na wananchi ili ziwe sehemu ya tunu za taifa ndani ya katiba.
Mheshimiwa Spika, hali hii si tu kwamba inawachanganya wananchi, lakini inaibua munkari wa kuhoji iwapo Rais Kikwete kupitia serikali yake, wanayo dhamira ya kuheshimu na kutambua mchango wa vyombo vya habari na umuhimu wa wananchi kuwa na taarifa juu ya namna nchi yao inavyoendeshwa! Ni suala linalochanganya na kuibua maswali mengi yasiyokuwa na majibu kuona Rais Kikwete anatoa ahadi kimataifa kuhusu kukuza uwazi na uwajibikaji kwa kuimarisha uhuru wa habari na kupata taarifa, lakini wakati huo huo akiwa hapa nchini bali ya serikali yake kushindwa kutimiza ahadi hiyo, anasimamia vikao vya chama chake ambacho kinapinga maoni ya Watanzania wanaotaka Katiba Mpya izingatie uwazi, uadilifu na uwajibikaji!
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia majibu ya Serikali yaliyotolewa hapa bungeni kwenye mkutano huu wa 15 kikao cha 16 kuhusu miswada ya sheria hizi mbili na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Ubungo John Mnyika na Serikali ikashindwa kutoa majibu ya kuridhisha, inazidi kudhihirisha kuwa hakuna dhamira ya dhati kutekeleza jambo hili. Sasa maelezo ya Mheshimiwa waziri wa Sheria na Katiba, Dr. Asha Rose Migiro katika hotuba ya Makadirio ya wizara yake ni kuwa waraka wa kupeleka kwenye Baraza la Mawaziri wa kupendekeza kutungwa  kwa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa umeandaliwa.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitarajia Serikali ya CCM kutambua umuhimu wa kutekeleza ahadi zake hapa bungeni kwa miaka 7 lakini zaidi ya hapo kutimiza ahadi iliyotolewa na Rais Kikwete ili kumwokoa na aibu ya kusema uongo kwenye mkutano mkubwa wa kimataifa wa Open Government Partnership, mjini London. Tulitarajia Serikali hii ingelikuwa sikivu, ingetambua kuwa sheria hizo ni mtambuka na inahusu wananchi wote katika haki ya kupata na kutoa taarifa kama ilivyoelekezwa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inalaani kwa nguvu zote, sheria kandamizi zinazonyima vyombo vya habari uhuru wa kufanyakazi zake kwa ufanisi, za kufichua maovu kama rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na hujuma za raslimali za taifa. Sheria hizo zinatishia uhuru wa uhariri na kuleta woga wa kushtakiwa kwa makosa ya jinai.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kuleta Bungeni muswada wa sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ambazo zitasimamia utendaji kazi wa vyombo vya habari nchini. Wote tunafahamu kuwa sheria zilizopo zinazosimamia vyombo vya habari ni mbaya, ni kandamizi na hazina nafasi katika nchi inayojinadi kuwa ni ya kidemokrasia.  Sheria hizi zinavifanya vyombo vya habari na wanahabari kutekeleza majukumu yao katika mazingira magumu. Katika vikao vya bunge kwa takriban miaka saba sasa, tumekuwa tukisikia ahadi za serikali ya kubadilisha sheria hizi kandamizi ambazo kwa kiasi kikubwa zinakiuka Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, tunawasiwasi mkubwa wa nia ya serikali ya kufanya mabadiliko stahiki. Tunaona hakuna dhamira ya dhati ya kuleta sheria bora. Hili limedhihirishwa na hatua ya serikali ya mwezi Novemba mwaka 2013 ya kuleta mabadiliko ya sheria mbalimbali (Miscellaneous Ammendement Act) ambayo ndani yake ilikuwa na mapendekezo ya Sheria ya Magazeti 1976, Sheria ya Filamu na Michezo ya Jukwaa na Sheria ya Kanuni za Adhabu ambazo zilikuwa na lengo ya kuongeza adhabu kubwa kwa makosa ya kitaaluma.
Ni muhimu sana kwa Serikali kuacha kutoa ahadi hewa hapa Bungeni na kwingineko na badala yake tudhihirishe utashi wetu kwa kutekeleza kwa vitendo. Ahadi zinazotolewa na mawaziri miaka nenda miaka rudi hapa Bungeni bila kutekelezwa zinashusha hadhi ya Bunge na Taifa letu machoni mwa watanzania na dunia kwa ujumla. Ni jambo lisilopendeza na ni la aibu kwa kweli kwani inaonyesha dhahiri kuwa ama utendaji kazi ni hafifu sana katika serikali hii au la basi Serikali hii haina nia njema ya kufanya marekebisho ya kimfumo ili tuwe na sera na sheria nzuri ambazo zitastawisha demokrasia, uwazi na uwajibikaji.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inawataka mawaziri husika wawe jasiri na watimize ahadi walizotoa kwenye Bunge hili tukufu za kuleta miswada ya sheria za Haki ya Kupata Taarifa na ule wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari.  Wadau wa habari wameshafanya kazi kubwa kwa kutoa mapendekezo yao serikalini. Wayatumie mapendekezo hayo kuandika miswada hiyo na kuileta hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, wenzetu wadau wa habari wamejipanga kuboresha na kuinua hali ya uwajibikaji na maadili katika vyombo vya habari. Tuwaunge mkono kwa dhati kwenye hilo. Kupitia Baraza lao la habari wamepitisha Azimio la Dar es Salaam ambalo linazungumzia haki na wajibu wa vyombo vya habari katika kuimarisha weledi, maadili na uhuru wa uhariri.
Napenda niongeze kwa lengo ya kuweka msisitizo kuwa Haki ya Kupata Taarifa ni muhimu na ya msingi sana, kwani ni sheria mtambuka na inahusu haki ya msingi ya kupata habari ambayo ni haki inayolindwa kikatiba. Ni ukweli wa uhakika kuwa utawala ulioshamiri katika mila za usiri ndio ulioifikisha Tanzania yetu mahali hapa pabaya. Ndio chanzo cha mikataba mibovu na kushindwa kwa uwajibikaji kwa sababu tu watendaji wabovu wanaweza kujificha katika kinga ya usiri. Kambi Rasmi ya Upinzani tunaitaka Serikali kuleta Bungeni muswada wa sheria ya Haki ya Kupata Habari ndani ya mwaka huu kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inasisitiza tena kuwa uwepo wa sheria nzuri za vyombo vya habari ambayo itakuwa kwa manufaa ya wananchi na serikali. Wakati wananchi wanasubiri sheria mpya ya Huduma za Vyombo vya Habari, Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuleta Bungeni Muswada wa kufuta Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 pamoja na kufanyia marekebisho sheria nyingine 17 zenye vipengele kandamizi kwa vyombo vya habari kwa kuwa sheria hizo ni kinyume na Katiba ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Pia sheria hizo zinaendeleza utamaduni wa usiri ambao kama nilivyosema awali unasaidia sana kufanya viongozi wasiwajibike ipasavyo na kufanya mambo yasiyostahili kwa kujificha kwenye kinga ya usiri.
2.2 Uhuru wa uhariri, vitisho kwa waandishi wa habari na utatu hatarishi
Mheshimiwa Spika, katika hali ambayo imezidi kudhihirisha kuwa Serikali ya CCM inawalazimisha Watanzania kuendelea kuishi ‘zama za mawe’, Mwezi Septemba mwaka jana, tasnia ya habari ilipata dhahama kubwa baada ya Serikali kupitia wizara husika na Habari Maelezo, katika hali ambayo hadi sasa haijulikani ilikuwa kwa maslahi ya nani, iliamua kufungia magazeti mawili ya Mtanzania na Mwananchi. Tunasema ni zama za mawe kwa sababu, vitendo vya kufungia vyombo vya habari kwa namna ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali ya CCM ikitumia sheria zilizopitwa na wakati, ikiwa ni sehemu ya kubana uhuru wa maoni na utoaji wa fikra mbadala, vilifanywa enzi zile ambapo dunia ilikuwa inaaminishwa kuwa ina muundo wa meza.
Mheshimiwa Spika, Kwa namna ambayo iliendelea kutuanika namna tunavyokumbatia ‘ukoloni na ukaburu’, Serikali ya CCM ilijigeuza mlalamikaji, polisi (mkamataji), mwendesha mashtaka, hakimu na kisha askari magereza (mfugaji) kisha kulifungia Gazeti la Mtanzania siku 90 na Mwananchi siku 14. Kambi ya Upinzani Bungeni inataka kujua kupitia kauli ya serikali hapa bungeni, mtindo huu wa udikteta unaofanywa na serikali hii inayojiita sikivu inayoshughulikia vyombo vya habari, utaendelea hadi lini?
Mheshimiwa Spika, kwa sasa zipo fikra miongoni mwa wadau wa vyombo vya habari kwamba uhuru wa habari nchini unazidi ‘kuwambwa msalabani’ kwa sababu ya utatu wa hatari ambao umetengenezwa na Serikali ya CCM, kwenye Wizara ya Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni. Utatu huu hatari unaundwa na waziri mwenyewe Dk. Fenela Mkangara ambaye mbali ya kwamba si mwanahabari, si mwanasanaa, si mwanamziki wala si mwanamichezo, taarifa zinaonesha kuwa amekuwa na dhamira ya kupambana na vyombo vya habari, ambao ni wadau wake, tangu alipoteuliwa.
Mheshimiwa Spika, Akiandika kwenye safu yake, mmoja wa waandishi waandamizi nchini, alikuwa na haya ya kusema juu ya Dk. Mukangara;
Waziri mwenye dhamana Dk. Fenella Mukangara kwa muda mrefu amekuwa na nia ovu dhidi ya vyombo vya habari. Julai mwaka jana (akimaanisha 2012) tukiwa Hotelki ya Dodoma mjini Dodoma, wakati tunafanya mazungumzo rasmi na Waziri Mukangara, walikuwepo Theophil Makunga, Pili Mutambalike, Neville Meena na marehemu Alfred Mbogola na wengine, Dk. Mukangara alitoa kauli iliyotushtua wengi na sasa ndipo tunaona inatekelezeka kwa vitendo.”
Mwandishi huyo aliongeza kwa kunukuu maneno ya Waziri Mukangara ambaye amenukuliwa akisema;
“Nikipata fursa Mwananchi nitalifuta, mimi linanikera sana. Tena na Nipashe nao naona wanakuja, ikibidi nitawafungia tu, mimi siogopi kitu.” Hayo ni maneno ya Waziri anayetakiwa kuwa mlezi wa vyombo vya habari!
Mwandishi huyo katika makala yake akaendelea kuandika hivi;
“Baada ya kauli hii tuliendelea na mazungumzo mengine, lakini Meena akatwambia kuwa Dk. Mukangara aliwahi kutoa kauli kama hii ofisini kwake walipokwenda akina Jesse Kwayu, Meena na Absalom Kibanda kuomba Gazeti la Mwanahalisi lifunguliwe. Mwanahalisi alilifungia kwa muda usiojulikana…”.
Mheshimiwa Spika, si Waziri Mukangara mwenyewe wala mtu mwingine yeyote kwa niaba yake, amewahi kukanusha maneno hayo aliyonukuliwa akiyasema hadharani mbele ya wadau ambao yeye anapaswa kuwa kiongozi na mlezi wao.  Kutokana na mwenendo wa Waziri Mukangara wa kupamabana na vyombo vya habari, unaofumbiwa macho na mamlaka iliyomteua, labda kwa bahati mbaya au sehemu ya mkakati wa serikali hii ya CCM. Uhusiano wa waziri na vyombo vya habari ulifikia hatua mbaya zaidi, baada ya wadau wa habari waliokutana Oktoba 9 mwaka jana, kufikia maazimio kadhaa, ikiwemo lile linalosema;
“Kusitisha kuandika, kutangaza na kupiga picha shughuli zozote zitakazowahusisha au kuratibiwa na Mheshimiwa Fenella Mukangara na Assah Mwambene hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo. Adhabu hiyo inaanza mara moja kuanzia leo.”
Mheshimiwa Spika, hapo juu kwenye moja ya maazimio ya wadau wa habari, ametajwa Assah Mwambene, huyu ni Mkurugenzi wa Habari Maelezo. Mkurugenzi huyu ambaye amewahi kufanya kazi kwenye vyombo vya habari kama mwandishi, pamoja na kwamba kwa majukumu yake hayo alipaswa kuwa mtu wa karibu kama mwelekezi na kiongozi kwa wadau wake, kwa kushirikiana na Waziri Fenella Mukangara, amekuwa ni mwiba kwa utendaji wa vyombo hivi, akihusika kuuweka uhuru wa habari na uhariri katika sintofahamu kubwa.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Mkurugenzi wa Habari Maelezo kufanya maamuzi makubwa ya kuyatisha magazeti ya Mwananchi na Rai, kutimiza wajibu wa kuendelea kuhabarisha, kwanza bila kuwa na msingi wowote wa kisheria na pili bila kuwasiliana na wakubwa wake wala wasaidizi wake, kama ilivyotamkwa na aliyekuwa Naibu Waziri Amos Makala, ni jambo ambalo linathibitisha jinsi alivyo sehemu ya utatu huu tunaozungumza hapa.
Mheshimiwa Spika, anayekamilisha utatu unaoweka uhuru wa habari na uhariri kwenye hati hati ni Naibu Waziri Juma Nkamia. Kwa kauli zake mwenyewe hapa hapa bungeni akisikiwa na Watanzania wote, wakiwemo wadau wa habari, alithibitisha jinsi alivyo na chuki dhidi ya waandishi wa habari.
2.3 Kauli za Dharau Dhidi ya Wanahabari
Mheshimiwa Spika, wakati katibu mkuu kiongozi anataja mabadiliko ya baraza la mawaziri Ikulu tarehe 19 Januari Mwaka huu, akiwa amezungukwa na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, wakati akitaja jina la Naibu waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Juma Nkamia, wanahabari hao waliguna na kucheka ikiwa ni ishara ya kutoridhishwa na uteuzi huo. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inaungana na wana habari wote kwa kuguna na kuchekeshwa na uteuzi wa Mhe. Juma Nkamia ambaye ni dhahiri hana maslahi na wana habari bali ameitumia tasnia ya habari kama daraja lake la kufanikisha maslahi yake binafsi ya kisiasa.
Mheshimiwa Spika, tarehe 17 Novemba mwaka 2013, Baraza la Habari la Tanzania lilioneshwa kusikitishwa na kauli za Mhe. Nkamia ambaye alitoa kauli ya kulikashifu baraza hilo wakati akiwa katika vikao vya Bunge wakati yeye akiwa ni mmoja watu walionufaika na Baraza hilo. Akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Nkamia alitamka kuwa , MCT(Baraza la Habari Tanzania) na TEF (Jukwaa la wahariri Tanzania) ni sawa na asasi zisizo za Kiserikali (NGOs) lakini zimekuwa zikijipa kazi ya kusimamia waandishi wa habari nchini.
Mheshimiwa Spika, ni wazi kuwa kauli ya Mhe. Nkamia ilikua ni ya dharau dhidi ya wana habari, dharau dhidi ya tasnia ya habari na dharau dhidi ya vyombo hivyo ambavyo kwa nyakati tofauti, kabla na hata baada ya kupata ubunge, Naibu Waziri alikua akizitambua na kushirikiana nazo. Na kwa kumbukumbu rasmi, ni kuwa MCT na TEF ndizo taasisi zinazoendelea kupigania maslahi ya wana habari dhidi ya uonevu unaofanywa na Serikali hasa kwa wale ambao wana misimamo na misingi ya uadilifu kwani vyombo hivyo ndivyo vilivyounda timu maalum ya uchunguzi kuchunguza mazingira yaliyopelekea kuuawa kwa mwandishi wa habari Daudi Mwangosi Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo, wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa ambapo ripoti yake ilifichua kuwepo kwa mahusiano mabaya baina ya waandishi wa habari na aliyekua kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa ambaye aliulizwa maswali magumu na Marehemu Mwangosi ikiwemo ni kwanini chama tawala cha CCM kiko huru kufanya mikutano ya kisiasa wakati chama cha upinzani kama Chadema kinawekewa vikwazo na polisi kila wakati.
Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri amesahau kuwa anazoziita asasi zisizo za kiserikali, ndizo zilizochangia kwa mapinduzi katika sekta ya habari nchini kwa kufanikisha mambo muhimu ikiwemo kusimamia maadili ya waandishi wa habari, kuandaa mitaala ya kufundishia waandishi wa habari ambayo imepitishwa na Baraza la Elimu la Taifa (NACTE) na pia kutumiwa na viongozi wakuu wa Serikali na wanasiasa kama aliyekua Makamu wa Rais, Dkt. Omar Ali Juma, mawaziri wakuu waliopita Edward Lowassa na Fredrick Sumaye katika kusululuhisha migogoro inayohusiana na tasnia ya habari, inakuaje yeye binafsi avipuuze vyombo hivyo muhimu? Na ndio maana kuteuliwa kwake kuwa Naibu Waziri kuliwashangaza wanahabari na wadau wa habari.
Mheshimiwa Spika, aidha kwa nyakati tofauti Naibu waziri amekua akiwaita waandishi wa habari kuwa ni waandishi makanjanja na yeye kujinasibu kuwa ni mwandishi mwenye weledi na taaluma. Kambi rasmi ya Upinzani, ina ushahidi kuwa Mhe. Nkamia amelidanganya bunge na taifa kwa ujumla kwa kutuaminisha kuwa yeye alikua ni mfanyakazi mwajiriwa wa Shirika la Habari La Uingereza BBC, kitengo cha Propaganga wakati Bwana Tido Mhando ambaye amefanya kazi na Shirika hilo kwa takribani miaka 20, alikana kujua uwepo wa kitengo hicho katika Shirika hilo na zaidi kueleza kuwa Mhe. Nkamia hakua muajiriwa wa Shirika hilo bali aliitwa ili kwenda kusoma taarifa za habari tu kama kibarua jaambo ambalo hajawahi kusema hadharani. Hivyo mbwembwe zote za Naibu waziri zilikua ni kumuhadaa Rais Kikwete ili apate uongozi kwa sifa asizostahili. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inauliza, je wakiitwa waandishi makanjanja, Kiranja wao ama mwalimu wao mkuu ni nani?
3.0          MAENDELEO YA VIJANA
3.1 Baraza la Vijana la Taifa, Benki ya Vijana na Mustakabali wa Maendeleo ya Vijana Nchini
Mheshimiwa Spika; Kifungu 6002 Idara ya Maendeleo ya Vijana ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika mwaka wa fedha 2014/2015 inaombewa jumla ya Sh. 995, 234,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Fedha hizo kwa kiwango kikubwa ni za matumizi yasiyo ya lazima yanayohusiana na Mbio za Mwenge yasiyokuwa na uhusiano moja kwa moja na maendeleo ya vijana nchini.  Ikumbukwe kwamba siku chache zilizopita tarehe 27 Mei 2014 katika kikao cha kumi na tisa kwenye Mkutano huu wa Bunge, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilijibu kwa mfano mwaka 2012 Jumla ya Tsh 650,000,000 zilitengwa kwa ajili ya kuadhimisha Uzinduzi na Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Hali hii inajidhihirisha katika uchambuzi wa kasma za idara hii ya maendeleo ya vijana ambapo kwenye matumizi ya kawaida kasma 210314 kumetengwa posho za vikao Sh 20,100,000 katika mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya “vikao vya uanzishwaji wa Baraza la Vijana, Benki ya Vijana pamoja na tathmini ya Mbio za Mwenge wa Uhuru”.
Mheshimiwa Spika; Hali hii inadhihirisha Wizara haiweki kipaumbele katika kazi muhimu zinazohusu uanzishaji uanzishwaji wa vyombo viwili muhimu kwa ajili ya vijana: Baraza la Vijana la Taifa na Benki ya Vijana ambavyo Kambi Rasmi ya Upinzani imehoji kwa nyakati mbalimbali kutaka utekelezaji uharakishwe. Kitendo cha kutenga rasilimali kidogo kwa ajili ya kazi hizo, huku rasilimali hizo zikielekezwa katika posho za vikao  na vikao hivyo vikiwa na ajenda nyingi nyingine zikiwa tofauti na masuala ya msingi ya maendeleo ya vijana kinaashiria udhaifu mkubwa wa Serikali inayoongozwa na CCM katika masuala yanayohusu vijana.
Mheshimiwa Spika, kwa vyovyote vile, chini ya makada wa CCM posho hizo zitatumika kujadili kuhusu mbio za Mwenge kuliko masuala ya msingi ya uanzishwaji wa Baraza la Vijana la Taifa na Benki ya Vijana kwa kuzingatia namna Serikali ya CCM ilivyojibu bungeni kubariki Mwenge huo kutumika kwa ajili ya propaganda potofu za Serikali mbili kuelekea kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba. Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa mwito kwa uongozi wa Bunge na Wabunge katika mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hii kuhakikisha mamlaka na madaraka ya wabunge kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya Katiba ya Nchi yanatumika vizuri zaidi kuwezesha kuharakishwa kuundwa kwa Baraza la Vijana la Taifa na Benki ya Vijana kwa ajili ya Maendeleo ya Vijana nchini.
Mheshimiwa Spika; Katika Mkutano wa 14 Kikao cha 15 tarehe 21 Disemba 2013 ulisomwa Bungeni Muswada Binafsi wa Mbunge wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013. Baada ya muswada huo, Bunge lilielezwa pia na Mheshimiwa Spika,
“ Waheshimiwa wabunge, muswada binafsi wa Mheshimiwa Zitto Kabwe sasa utaanza kuwepo kwenye website ya Bunge na utakuwa public mpaka utakapopangiwa tarehe ya kujadiliwa na utapelekwa kwenye kamati zitakazohusika wakati muafaka”.
Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa mwito kwa Spika: Mosi, kuweka kumbukumbu sawa kwa kulieleza Bunge kwamba muswada binafsi wa mbunge uliwasilishwa na Mheshimiwa John Mnyika; Pili, kulieleza Bunge sababu ya maelekezo yake ya muswada huo kuwepo kwenye tovuti ya bunge kwa ajili ya kuwa wazi kwa umma mpaka sasa kutokutekelezwa, Tatu, ni lini muswada huo utapangiwa tarehe ya kujadiliwa; Nne, ni kwanini mpaka sasa muswada huo haujapelekwa kwenye kamati zinazohusika;  Tano, ni upi wakati muafaka alioutaja kwenye maelezo yake.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inawahimiza wabunge kuzingatia kwamba kutokuwepo kwa chombo kinachowaunganisha vijana wote bila kujadili itikadi kufuatilia masuala ya maendeleo ya vijana kunafanya Wizara mbalimbali za kisekta kutokuzingatia masuala yaliyokipaumbele kwa maendeleo ya vijana. Mathalani, katika Mkutano huu wa Bunge katika Fungu la 65 la Wizara ya Kazi na Ajira Kitabu cha Nne Cha Miradi ya Maendeleo Kifungu cha 2002, pamoja na wabunge na vijana kupewa matumaini kwamba zimepitishwa bilioni tatu kwa ajili ya mikopo na mitaji kwa vijana ukweli ni kwamba fedha hizo zimepangiwa matumizi ambayo kusipokuwa na chombo cha kuyafuatilia kutakuwa na udhaifu, ufisadi na ubadhirifu kama ilivyojitokeza katika fedha za mifuko ya maendeleo ya vijana  kati ya mwaka 1993/1994 mpaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika; Kwa mujibu wa Kasma za Kifungu hicho cha 2002 cha Bajeti iliyopitishwa ya Fungu 65 Wizara ya Kazi na Ajira, fedha hizo zinazopaswa kuwa za mikopo na mitaji kwa vijana zitatumika milioni 700 kwa ajili ya kulipia utaalamu elekezi (consultancy fees) kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vijana 200 tu; milioni 150 zitatumika kununulia magari Wizarani, milioni 60 zitatumika kwenye matangazo na orodha ndefu nyingine ya  matumizi yasiyo ya lazima ambayo kutokana na ufinyu wa muda sitaendelea kuyataja.  Aidha, katika mjadala wa bajeti hiyo wabunge waliweka bayana kwamba kiwango kinachotengwa katika Mifuko ya Maendeleo ya Vijana iwe ni kwa Serikali Kuu na hata Halmashauri ni kidogo ukilinganisha na uwezo wa nchi, mahitaji ya vijana na mafungu mengine yasiyo na matumizi muhimu yanavyotengewa fedha nyingi katika baadhi ya Wizara.
Mheshimiwa Spika; Hivyo, ili Baraza la Vijana la Taifa na Benki ya Vijana ambavyo ni vyombo muhimu kwa maendeleo ya vijana viweze kuanzishwa kwa wakati, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa mwito kwa Spika wa Bunge kuelekeza muswada binafsi uliokwisha wasilishwa kwa Bunge kwa kamati zinazohusika kwa ajili ya kuanza  kuujadili. Aidha, Spika arejea ratiba ya Bunge ambapo imetajwa bayana kwamba kati ya tarehe 5 Juni 2014 na 11 Juni 2014 ratiba ya Bunge haitahusu uwasilishaji wa Bajeti za Serikali. Ratiba imetaja bayana kwamba “Shughuli nyingine yoyote kama itavyokuwa imeelekezwa na Spika” inaweza kuingizwa kwenye ratiba; hivyo, fursa hiyo itumike kuleta muswada huu Bunge kusomwa kwa mara ya pili.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Bunge kuingilia kati suala hili na kuisimamia Serikali kwa kuzingatia kwamba katika majumuisho ya Bajeti ya Wizara hii kwa mwaka 2013/2014 tarehe 21 Mei 2013 mkutano wa 11 kikao cha 30; Serikali ilitumia kisingizio kwamba ‘ni bunge la bajeti’ kukwepa kuwasilishwa kwa muswda Bunge. Hata hivyo, ahadi ya Serikali ya kuwasilisha muswada haikutekelezwa kwenye mikutano mitatu uliyofuatia ya 12, 13 na 14; hivyo mkutano huu wa 15 ni muafaka kuwezesha maamuzi kufanyika kwa ajili ya maendeleo ya vijana nchini.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaikumbusha Serikali na wabunge kwamba Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa  Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007; hata hivyo Serikali imekuwa ikikwepa kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa pamoja na kuwa suala hilo linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini.  Kambi Rasmi ya Upinzani inakumbusha pia  kwamba katika ilani za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 vyama mbalimbali viliahidi kuhakikisha kwamba Baraza la Vijana la Taifa linaundwa.  Ili kuwahadaa na kujipatia kura za vijana CCM kwa kupitia ilani yake katika kipengele 80 (k)  inasema
“Kuhamasisha ushiriki wa vijana katika ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwa ni pamoja na kukamilisha uanzishaji wa Baraza la Vijana”.
Mheshimiwa Spika; Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inatarajia kwamba wabunge wa pande zote katika suala hili la kuanzishwa kwa Baraza la Vijana la Taifa kuungana kuwa kitu kimoja kuisimamia Serikali na kutumia madaraka ya  Bunge kutunga sheria wakati wa Mkutano huu wa Bunge unaoendelea. Serikali na wabunge mzingatie kwamba  zaidi ya miaka 18 ahadi za kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa baraza  la Vijana la Taifa; bila utekelezaji kamili na wa haraka. Baraza la Vijana litawezesha vijana kuanzia kwenye vijiji/mitaa mpaka taifa kuweza kuwa na vyombo vya kuwaunganisha vijana kwa kike na wa kiume kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa.
Mheshimiwa Spika; Aidha, Baraza hilo litafuatilia pia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya vijana kwenye Halmashauri, Serikali kuu, katika vyombo mbalimbali vya maendeleo na wadau wa maendeleo. Pia, Baraza la Vijana litafuatilia kwa karibu utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuhakikisha kwamba fedha zinatengwa za kutosha na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana kujiajiri, kukuza vipaji vyao na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji ni kwa nini kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 Jumla ya fedha zilizopelekwa kwenye vikundi mbalimbali kwa kupitia mfuko wa vijana ni shilingi milioni 172.6 tu sawa na asilimia 2.8 tu, kati ya Shilingi Bilioni 6.1 ambazo Serikali mwaka jana iliwadanganya vijana kuwa itatenga, huku taarifa ya wizara ikionesha kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 2 sawa na asilimia 32.7 pekee ndizo zilizokua zimepokelewa hadi kufikia April 2014. Je, kiasi cha shilingi milioni 827.4, zimetumikaje tumikaje? Je, Serikali itaacha lini kuwahadaa vijana kuwa wanatenga mabilioni ili kuwanyamazisha katika kudai haki zao huku ikijua kuwa haiwezi kuwasaidia hata kwa kile wanachostahili? 
4.0          UTAMADUNI
4.1          UTAMADUNI: KIELELEZO CHA HISTORIA YA TAIFA
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imekua ikishauri Serikali juu ya umuhimu wa kutunza maeneo na majengo ya kale ili kuweza kuonesha urithi wa utamaduni wa taifa letu. Ni dhahiri kuwa maeneo mengi ya kihistoria yameachwa na kuwa magofu na mengine yanaendelea kubomolewa kwa ujenzi mpya hali inayofanya historia ipotee, jambo ambalo pia linalikosesha taifa mapato yanayotokana na utalii. Kambi Rasmi ya Upinzani, inataka kujua mikakati ya wizara kuhakikisha kuwa maeneo na majengo ya kale yanahifadhiwa na kuachwa katika hali yake kwa mwaka huu wa fedha wa 2014/2015.
4.2 BARAZA LA SANAA TANZANIA (BASATA)
Mheshimiwa Spika, Baraza la Sanaa nchini lina dhamana kubwa kuhakikisha kuwa sanaa ya mtanzania haipoki wala kudhalilisha maadili pamoja na kuiendeleza sanaa hapa nchini. Ni jambo la kushangaza kuona kuwa Baraza hili hufanya kazi kwa kuzinduka tu usingizini huku athari za uporomokaji wa maadili kwa kupitia sanaa katika jamii zinakua kubwa.
Mheshimiwa Spika, ngoma ya Kigodoro haikua maarufu katika sehemu kubwa za nchi kutokana na ngoma hiyo kuchezwa katika sehemu chache. Lakini, baada ya kutolewa kwa filamu ya Kidogoro ambayo kwa kiasi kikubwa ilihamasisha jamii kutaka kujua maana ya kidogoro na hivyo ngoma hiyo kuzidi kupata umaarufu katika sehemu kubwa ya jamii ya watanzania hata kwa watanzania wanaoishi nje ya nchi. Mara baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuelezea athari za ngoma hii katika maadili ya watanzania BASATA ghafla ikazinduka usingizini na kupiga marufuku ngoma hiyo, huku filamu ya Kigodoro ikiwemo katika soko la filamu na ikiendelea kuuzwa huku ikiambatana na ujumbe ambao si tu unahamasisha uvunjifu wa maadili ya kitanzania bali unatoa taswira ya jamii isiyostaarabika. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka wizara hii kuisimamia BASATA ipasavyo pamoja na kuipa uwezo wa kifedha ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kuutunza na kuutangaza utamaduni wa mtanzania kwa kupitia kazi za sanaa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka BASATA kuacha uvivu na kutekeleza majukumu yake kwa ubunifu ili kulinda na kuutangaza utamaduni wa Mtanzania ili hatimaye navyo vitoe mchango katika taifa kutokana na mapato yanayotokana na mauzo ya kazi za sanaa na utamaduni.
4.3 WASANII NA HARAKATI MBALIMBALI
Mheshimiwa Spika, katika mapambano ya kudai haki za wasanii duniani popote, wasanii huongozwa na dhamira ya kutumia sanaa zao ili kuleta mabadiliko ya kweli na si kukubali kutumika kuwa faraja kwa watu wengine kufanikisha malengo yao na mwishowe haki wanazozipigania kuonekana kama kelele za chura.
Mheshimiwa Spika, kila mtu ana uhuru wa kufanya maamuzi yake hasa maamuzi ya msimamo wa kisiasa. Ila kwa muda mrefu sasa, wasanii wa Kitanzania tumeshindwa kuwa mabalozi wa kweli wa haki katika kuhakikisha kuwa tunatumia kazi zetu za sanaa tunapigania haki na usawa ili kulikomboa taifa. Matokeo yake, baadhi ya wasanii wamekua wakitumika kama chambo na baadhi ya wanasiasa ili kuweza kutimiza maslahi ya wanasiasa, ambayo kwa kifupi baada ya kutumika, hata maslahi ya wasanii ambayo wanapigania huwa hayapewi kipaumbele. Mfano mzuri kwetu wasanii ni jinsi ambavyo tumetumika sana katika harakati za kisiasa lakini katika mchakato wa katiba, tumesahulika. This is a wake up call kwa wasanii wote ambao wamekubali kutumika kwa maslahi ya muda mfupi bila kuangalia mustakabali wa sekta ya sanaa katika taifa letu. Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, inawataka wasanii kuacha kutumika na kujenga umoja imara utakaotetea maslahi yao kwa ujumla bila ya kufuata mashinikizo ya kisiasa ili kuleta mapinduzi ya kweli katika sanaa.
4.3.1SANAA NA WASANII KUTUMIKA KWENYE UFISADI NA UFICHAJI WA MGONGANO WA MASLAHI
Mheshimiwa Spika,  Katika Maoni yetu kwa hoja hii ya mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu ilizungumzia kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imeshindwa kulinda haki za wasanii licha ya kuwepo kwa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki tangu mwaka 1999. Tulielezea jnsi ambavyo, licha ya masharti ya Sheria hiyo na licha ya kuwepo kwa Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) tangu mwaka 2007, nyimbo za wasanii nchini zimeendelea kutumiwa kwenye matangazo ya vyombo vya habari, hasa vya Serikali kama vile Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1 na TBC2) bila wasanii waliozitunga au kuziimba nyimbo hizo kupata malipo yoyote.
Mheshimiwa Spika, Ni haki na wajibu kwa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kupiga kelele dhidi ya unyonyaji huu wa wasanii wetu, hasa wanamuziki vijana wa kizazi kipya ambao wanajihangaikia kutafuta maisha na kuendeleza vipaji vyao. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inawaahidi wasanii wetu kwamba itaendelea kutimiza wajibu wake kwa kutetea haki na maslahi yao hadi watakapotendewa haki.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, ni haki na wajibu kwa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kuwakemea na kuwakosoa vijana pale wanapojiingiza katika vitendo vinavyochafua sanaa na sifa zao kama wasanii na wa-Tanzania. Kama inavyofahamika na wananchi na hata kwa Bunge lako tukufu, wasanii kadhaa wa ki-Tanzania wamekamatwa katika nchi za nje wakiwa na madawa ya kulevya. Wasanii wa aina hii, wanaokubali kutumiwa kama punda wa mizigo ya madawa ya kulevya na mitandao haramu ya biashara hiyo, hawastahili chochote kutoka kwa wa-Tanzania zaidi ya dharau na adhabu kali zilizowekwa na sheria za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Kutumia umaarufu wao ili kuficha ushiriki wao katika biashara haramu ya madawa ya kulevya sio tatizo pekee la baadhi ya wasanii wetu. Sasa limejitokeza tatizo la baadhi ya wasanii wetu, hasa wanamuziki maarufu wa Bongo Fleva, kujiingiza – kwa kujua au kwa kutumiwa na wajanja bila ya wao kujua – kwenye ‘dili’ za kifisadi za kuiba fedha za umma. Wajanja hao hujificha katika kivuli cha makampuni yanayotajwa kuwa na malengo ya kuendeleza wasanii na sanaa kumbe ni vichaka vya kuficha ufisadi, mgongano wa kimaslahi na matumizi mabaya ya madaraka ya baadhi ya viongozi wa umma dhidi ya fedha za umma wanazopaswa kuzisimamia.
Utaratibu unaotumika kutekeleza dili hizi za kifisadi unafanana kwa kiasi kikubwa na utaratibu uliotumika kuiba mamia ya mabilioni ya fedha za umma kutoka kwenye akaunti ya madeni ya nje ya Benki Kuu ya Tanzania (EPA) mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 13 Agosti, 2012, Msajili Msaidizi wa Makampuni katika Wakala wa Usajili wa Makampuni na Leseni (BRELA) alitoa Hati ya Usajili (Certificate iof Incorporation) kwa kampuni inayoitwa Leka Dutigite Limited. Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, Leka Dutigite Ltd. ina ofisi zake katika ghorofa ya kwanza ya jengo la City House lililoko katika Mtaa wa Mkwepu, Dar es SalaaM. Mheshimiwa Spika,
Katiba, yaani Memorandum and Articles of Association, ya kampuni ya Leka Dutigite Ltd. iliyosajiliwa BRELA tarehe 13 Agosti, 2012 inaonyesha kwamba mwenye hisa nyingi katika kampuni hiyo ni kampuni nyingine inayoitwa  Gombe Advisors Ltd. ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa za kibenki ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu imezipata, mnamo tarehe 10 Desemba, 2012, Hifadhi ya Taifa ya Saadani ilihamisha jumla ya shilingi 12,200,000 kwenda kwenye akaunti na. 0150357447800 iliyoko CRDB Bank tawi la Pugu Road, Dar es Salaam, inayomilikiwa na Leka Dutigite Ltd. Hifadhi ya Taifa ya Saadani inamilikiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), ambayo ni shirika la umma. Siku moja baadae, fedha hizo zilitolewa kwa pesa taslimu kutoka kwenye akaunti hiyo.
Baada ya hapo, kati ya tarehe 14 Januari na 7 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd. iliingiziwa jumla ya shilingi 28,600,000. Fedha hizi zote ziliingizwa kama fedha taslimu na mtu aitwaye Mchange (shilingi 3,600,000 tarehe 14 Januari, 2013) na Leka Dutigite (shilingi 25,000,000 tarehe 23 Januari na 7 Februari, 2013). Kufikia tarehe 7 Februari, 2013, fedha hizo zote zilikwishatolewa benki.
Mheshimiwa Spika, Tarehe 28 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd. iliingiziwa shilingi 32,367,000 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Kwa mujibu wa taarifa za kibenki, siku hiyo hiyo, fedha hizo zilitolewa kwenye akaunti hiyo. Siku nne baadae, yaani tarehe 4 Machi, 2013, NSSF ilifanya malipo mengine kwenye akaunti ya Leka Dutigite Ltd., kwa mikupuo miwili, ya jumla ya shilingi 46,663,000. Siku hiyo hiyo, fedha hizo nazo zilitolewa kutoka kwenye akaunti hiyo kwa mikupuo miwili. Kwa hiyo, katika kipindi cha miezi mitatu katika ya tarehe 10 Desemba, 2012 na 4 Machi, 2013, Leka Dutigite Ltd. ililipwa shilingi 119,930,000 kwa utaratibu huo huo wa ingiza na toa fasta. Kati ya fedha hizo, shilingi 12,200,000 zililipwa na TANAPA na shilingi 79,027,000 zililipwa na NSSF.
Mheshimiwa Spika, Katika mazingira ya kawaida, sio kitu cha ajabu kwa mashirika ya umma kama NSSF na TANAPA kufanya biashara na watu au taasisi mbali mbali kama makampuni binafsi. Ukweli ni kwamba, kwa upande wa malipo yaliyofanywa na TANAPA, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu imeweza kupata nakala ya mkataba unaohusu Maandalizi ya Filamu (Documentary) kwa Ajili ya Kuhamasisha Shughuli za Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa Kutumia Wasanii Kutoka Kigoma. Mkataba huo umesainiwa tarehe 5 Desemba, 2012, kati ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Leka Dutigite Ltd. na una thamani ya shilingi 12,200,000, kiasi kile kile kilicholipwa na Hifadhi hiyo.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mazingira ya malipo haya sio ya kawaida. Hii ni kwa sababu ya uwepo wa kampuni ya Gombe Advisors Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, kampuni hii ilisajiliwa tarehe 24 Novemba, 2011. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, ofisi za Gombe Advisors Ltd. ziko kwenye jengo la City House, Mtaa wa Mkwepu, Dar es Salaam, ziliko ofisi za Leka Dutigite Ltd. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, wakurugenzi wa Gombe Advisors Ltd. ni Zitto Zuberi Kabwe ambaye kazi yake inatajwa kuwa ‘mchumi’, na Raphael Ongangi ambaye anatajwa kuwa ‘mchambuzi wa fedha na vitega uchumi’ (Financial and Investment Analyst). Bwana Ongangi aliwahi kutajwa na gazeti la kila wiki la Mawio la tarehe 26 Desemba 2013 kuwa ni mmoja wa washauri wa Zitto Zuberi Kabwe na anasemekana kuwa msaidizi wake. 
Mheshimiwa Spika, Zitto Zuberi Kabwe sio ‘mchumi’ anayetajwa katika nyaraka za BRELA zinazoihusu kampuni ya Gombe Advisors Ltd. pekee, bali pia ni Mbunge, tangu mwaka 2005, wa Bunge lako tukufu. Kama Mbunge, Mheshimiwa Zitto Kabwe ni ‘kiongozi wa umma’ kwa mujibu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, 1995. Sheria hii inawalazimu viongozi wa umma, wanapokuwa madarakani, kuwa “waadilifu, wenye huruma, utulivu, umakini na watakaoendeleza viwango vya juu vya maadili ili kujenga na kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa Serikali.”
Aidha, viongozi wa umma “... watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha shughuli zao binafsi kwa namna ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi kwa umma na haitatosheleza kwao kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu.” Vile vile, kuhusiana na maslahi binafsi, Sheria hii inaelekeza kwamba “... viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali wanayoshiriki katika kuyafanya.”
Mwisho, kuhusiana na maslahi ya umma, viongozi wa umma wanatakiwa, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa, kupanga masuala yao “kwa namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi, iliyojificha au inayoonekana kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati ya maslahi binafsi na maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma.” Kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, Mheshimiwa Zitto Kabwe hajawahi kutangaza maslahi aliyonayo kwenye mikataba ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd. na NSSF na TANAPA.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe sio tu ni Mbunge anayebanwa na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, bali pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC). Kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu, mojawapo ya majukumu ya PAC ni kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika Wizara na Mashirika ya Umma yaliyoainishwa katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. NSSF na TANAPA ni baadhi tu ya Mashirika ya Umma yaliyo chini ya usimamizi wa kibunge wa PAC.
Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwa kutumia makampuni yake ya Leka Dutigite Ltd. na Gombe Advisors Ltd., amefanya biashara na TANAPA, shirika la umma analolisimamia kama Mbunge na Mwenyekiti wa PAC. Mheshimiwa Zitto Kabwe na wanamuziki washirika wake, kwa kutumia makampuni ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd., wamelipwa fedha za umma za TANAPA na NSSF.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo juu ya madai ya ukiukwaji wa Sheria uliofanywa na viongozi wa umma na mashirika ya umma katika kashfa hii. Pamoja na maelezo yatayotolewa , Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa na TANAPA na NSSF; msukumo uliofanya fedha hizo zitolewe na matumizi ya fedha hizo kwa kuzingatia  masharti yanayosimamia fedha za umma na utawala bora katika usimamizi wa fedha za umma. Aidha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ifanye uchunguzi juu ya malipo na matumizi husika kwa kurejea masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sheria nyingine zinazohusika.  Kwa upande mwingine, kwa kuwa suala hili linahusu mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na usimamizi wa fedha za umma, Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge nayo ifanye uchunguzi wake juu ya madai ya masharti ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na Kanuni za Bunge juu ya maadili ya kiongozi wa umma ikiwemo yahusuyo utangazaji wa maslahi.
Mheshimiwa Spika; Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inatoa rai kwa wanamuziki na wasanii wengine wote nchini kuwa waangalifu na watu wanaotaka kutumia umaarufu wao kama wanamuziki na wasanii kwa lengo la kufanikisha dili za kifisadi. Bila kuchukua tahadhari ya kutosha, wasanii hao wanaweza kujikuta wakipoteza sifa na umaarufu wao ambao wameujenga kwa jitihada zao wenyewe.
4.4 MCHAKATO BUTU WA VAZI LA TAIFA
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, wakati huo chini ya Waziri Dk. Emmanuel Nchimbi, ilifanya uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Kubuni Vazi la Taifa mwezi Desemba 15, 2011.Kamati hiyo iliyokuwa na watu wanane, Mwenyekiti ni Joseph Kusaga na Katibu ni Angela Ngowi, pamoja na wajumbe wa kamati hiyo ni Habib Gunze, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali, Makwaia Kuhenga, Ndesambuka Merinyo na Absalom Kibanda, ambaye baadaye alitangaza kujiweka kando. Desemba 22, 2011, kamati hiyo ikazinduliwa rasmi na aliyekuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Emmanuel Nchimbi, tayari kuanza kazi ya kubuni Vazi la Taifa, mchakato ambao ulipaswa kukamilika ndani ya siku 75 tangu siku ya kuzinduliwa kwake. Mhe.Nchimbi aliahidi kuwa mara baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi hiyo ikiwamo kuainisha mapendekezo mbalimbali ya vitambaa vinavyoweza kufaa, Watanzania watakuwa wamepata Vazi la Taifa. Siku hiyo Waziri Nchimbi alisema kazi ya kamati hiyo si kuanza mchakato mpya wa Vazi la Taifa, bali ni kumalizia mchakato wa kupata vazi la mwanamume na mwanamke ulioanza mwaka 2004. Hata hivyo, baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri, tarehe Septemba 10, 2012, Kamati ya Vazi la Taifa chini ya Ndugu Kusaga ilikabidhi ripoti kwa Waziri Mukangara aliyekuwa na naibu wake, Amos Makalla. Uwasilishaji wa ripoti hiyo ulifanywa na Katibu wa Kamati ya Vazi la Taifa Angela Ngowi, akiwa na wajumbe wa kamati hiyo, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali na Ndesambuka Merinyo. Angela akasema katika mchakato wa kupata vazi hilo, walipokea zaidi ya michoro 200 kutoka kwa wasanii 88 na kupitisha michoro sita iliyokuwa imekidhi vigezo na kuikabidhi kwa wataalamu wa vitambaa kwa ajili ya kutoa uamuzi wao. Waziri Mukangara alionesha shauku yake ya kuona vazi hilo linapatikana haraka na kwamba lingevaliwa katika maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika ya Desemba 9, mwaka 2012.
Mheshimiwa Spika, ikiwa inakaribia kuwa miaka takribani miwili sasa tangu Waziri Mukangara apokee ripoti hiyo, hakuna vazi lililopatikana wala maelezo mapya juu ya hatima ya vazi hilo. Kwa vile vazi la taifa limekuwa likisubiriwa kwa shauku kubwa na Watanzania tangu mchakato huo ulipoanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka maelezo ya kina kutoka kwa Waziri ni nini kimeukwamisha mchakato huo?
4.5 SANAA NA USANII KUTAMBULIWA KAMA SEKTA YA KIUCHUMI NA ULINZI WA MILIKI BUNIFU KUBORESHWA KUINUA VIPATO VYA WASANII NA MAPATO KWA NCHI
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa juu ya maoni ambayo Wasanii waliyawasilisha mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na baadaye kwa baadhi ya wabunge ikiwemo wa upinzani kutaka wasanii watambuliwe kama kundi maalum katika katiba mpya kama ilivyo kwa wafugaji, wakulima na fani au tasnia nyingine. Aidha, wasanii wamependekeza kwamba rasimu ya katiba mpya itaje miliki bunifu (intellectual property).
Mheshimiwa Spika; Kutokana na umuhimu wa mapendekezo ya wasanii hao waliyoyatoa kupitia mashirikisho yao manne Shirikisho la Filamu, Shirikisho la Muziki, Shirikisho la Sanaa za maonyesho na Shirikisho la Sanaa za ufundi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa maoni kwa Serikali kwamba haipaswi kusubiri mpaka mchakato wa mabadiliko ya katiba  bali marekebisho ya msingi ya kisheria yapaswa kuharakishwa kuwezesha sanaa na usanii kuchangia katika kuongeza ajira, kuboresha maisha ya wasanii na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika mapato ya Serikali na Uchumi wa Nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika; Serikali imekuwa ikitazama sanaa kama suala la burudani zaidi badala ya kuitazama kama ni sekta muhimu ya kiuchumi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuzingatia kwamba Wasanii sio wanamuziki tu, wasanii wapo karibu katika kila kaya Tanzania. Wafinyanzi, wasusi, wapambaji, wanamuziki waigizaji, mafundi mbalimbali wa ushonaji ujenzi na kadhalika, wako wengi wala hata wao hawajitambui kama ni wasanii kutokana na mazingira waliyomo.
Mheshimiwa Spika; Katika ripoti mojawapo ya BASATA ya mwaka 2006, idadi ya wasanii nchini wakati huo ilikuwa ni milioni 6, ni wazi kuwa idadi hiyo kwa sasa itakuwa imepanda.  Katika miaka ya karibuni vijana wengi wamekuwa wanaongezeka kujiunga na kundi hili kwani katika sanaa kumekuwa na uwezekano wa kujipatia ajira, tena isiyokuwa na ukomo. Na hivyo sanaa kwa sasa si utamaduni peke yake bali ni sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika; Wasanii ni sehemu muhimu katika sekta ya Hakimiliki, takwimu za ripoti ya WIPO(World Intellectual Property Organisation) ya mwaka 2010, kuhusu mchango wa sekta ya hakimiliki katika uchumi wa Tanzania, inaonaonyesha  kuwa sekta hii, kati ya 2007-2010 ilichangia kati ya asilimia 3-4.6% ya gross domestic product(GDP). Na kiasi cha kati ya TSH 38.930 bilioni na 86.686 billion kilipatikana kama kipato cha walioajiriwa katika sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika; Kati ya watu 28, 202 na 44, 331 waliajiriwa rasmi, na hiyo ilikuwa kati ya asilimia 4.5 na 5.2% ya kundi zima la waajiriwa wa Taifa hili. Kwa kipimo cha GDP, sekta hii ilikuwa zaidi ya sekta ya madini, ambayo wote ni mashahidi imekuwa katika mazungumzo kila kona ya nchi. Na katika ajira sekta hii ilikuwa juu zaidi ya sekta nyingi zikiwemo madini, usafirishaji, mawasiliano, afya na ustawi wa jamii, maji, gesi, na hata ujenzi. Kwa mchango wa sekta hii wa 3.2% katika GDP kwa mwaka 2009 , umeweka sekta hii kuwa bora kuliko sekta za aina yake katika nchi  kama Croatia 3%, Singapore 2.9%, Latvia 2.9%, Lebanon 2.5%, Kenya 2.3%. Na katika mchango wa ajira sekta hii ilikuwa juu ya Romania, Bulgaria, Lebanon, Jamaica, Colombia, Kenya na Ukraine.
Mheshimiwa Spika; kwa upande wa Tanzania, Takwimu hizi hazijionyeshi katika takwimu za Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kuwa sanaa bado inaonekana ni burudani tu, na thamani yake katika uchumi haitiliwi uzito. Kutambuliwa kwa kundi hili kutawezesha kutungwa sheria na taratibu za kuwezesha Wasanii kuongeza ajira na mapato, na Taifa kufaidika na uchumi wa  raslimali hii.
Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inataka marekebisho makubwa kwenye sheria za nchi yetu kuwezesha kutajwa kwa miliki bunifu katika sanaa, usanii na sekta zote nyingine muhimu za kiuchumi. Ni muhimu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Serikali kwa ujumla ikazingatia kwamba mali ziko za aina tatu. Kuna mali zinazohamishika, mali zisizohamishika na mali zitokanazo na ubunifu. Aina mbili za kwanza zimetajwa katika katiba na ulinzi wake hujulikana na ni wa jadi. Lakini hii aina ya tatu ya mali huwa ni ngumu kuilinda kutokana na mfumo wake kuwa haushikiki hivyo sheria maalumu hutungwa kulinda aina hii ya mali (IP Laws).
Mheshimiwa Spika; Mali zitokanazo na ubunifu kwa sasa ndio mali zenye kipa umbele duniani. Uvumbuzi wa teknolojia mbalimbali, ugunduzi wa njia mbalimbali za kuboresha maisha, sanaa na mengi yanayolindwa na milikibunifu, vimeweza kutoa ajira kubwa na kutoa mchango mkubwa wa kipato kwa wagunduzi na nchi ambazo wagunduzi hao wamekuwa wakiishi au kuzisajili kazi zao. Kama wasanii, haki zetu katika milikibunifu zinajulikana kama Hakimiliki, lakini kama Watanzania tunaona ni muhimu kulinda haki zote za Milikibunifu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika; Nchi zote ambazo zimeweka taratibu imara za kulinda Milikibunifu duniani, zimewezesha wabunifu wake kubuni mambo ambayo yameweza kubadilisha maisha ya binadamu wengine duniani kote. Marekani iliweka kipengele cha Ulinzi wa hakimiliki katika katiba yake tangu mwaka Agosti 1787, na kazi za wagunduzi wa Marekani tunaziona kila wakati katika kazi za sanaa na teknolojia. Korea kusini ilinakiri sehemu ya katiba ya Marekani kuhusu ulinzi wa Milikibunifu kuanzia mwaka 1948, kwa wakati huu wote ni mashahidi wa bidhaa kama Samsung, Ld Daewoo, Hyundai na kadhalika.
Mheshimiwa Spika; Milikibunifu pamoja na kulinda haki katika kazi za sanaa ambazo picha ndogo ya mapato yake zimetajwa hapo juu, Milikibunifu italinda haki za wabunifu wetu, tafiti za wasomi wetu, ugunduzi mbalimbali, taratibu mbalimbali za mambo yetu ya kiasili, dawa za asili za miti yetu, na taratibu za matumizi ya dawa hizo, na mali asili zetu nyingine nyingi tunazozifahamu na ambazo bado hatujazifahamu .
Mheshimiwa Spika; Kuna hasara nyingi ambazo hupatikana kama nchi haina ulinzi wa Milikibunifu, mifano michache hapa Tanzania, ni kupoteza kwa Milikibunifu ya jina Tanzanite, ambayo licha ya kuwa inachimbwa Tanzania tu lakini jina linamilikiwa na kampuni ya Afrika ya Kusini. Vazi la kikoi, pamoja kuwa ni la asili ya Tanzania, milikibunifu imesajiliwa Kenya, staili ya michoro maarufu ya Tingatinga milikibunifu yake iko Japan. Na haya ni machache ambayo yameshtukiwa Milikibunifu ikifuatiwa vizuri ndipo haswa ukubwa wa tatizo utakapojulikana. Kuna ulazima mkubwa wa kutaja Milikibunifu katika sheria zote muhimu na kuanisha ulazima wa kulinda kuendeleza na kwezesha wabunifu wan chi kwa manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.
6.0 SEKTA YA MICHEZO NCHINI
6.1 UENDELEZAJI WA VIWANJA VYA MICHEZO NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imeendelea kuona umuhimu wa taifa kuwekeza katika viwanja vya michezo ili kuweza kupanua wigo wa taifa kujitangaza na kukusanya mapato yanayotokana na viwanja vya michezo nchini. Labda, wizara mpaka sasa haijaweza kujua hasara ambazo kama taifa tunapata kutokana na kutotumia nafasi zinazotokea na kutowekeza vya kutosha katika kuboresha michezo nchini.
Mheshimiwa Spika, enzi za chama kimoja, majengo na maeneo yote ya umma yalikuwa chini ya Serikali. Ujenzi na uendelezaji wa maeneo hayo ulifanya na Serikali kupitia kodi za wananchi, michango, fedha za wafadhili na wahisani mbalimbali. Hata baada ya uwepo wa vyama vingi, uendelezaji wa miradi yote iliyokuwa chini ya Chama kimoja ilifanywa kuwa ni jambo la kitaifa. Kwa namna isiyoeleweka baadhi ya maeneo ambayo CCM imeshindwa kuyarudisha kwa wananchi na kuwa mali ya umma  na kuyafanya ni  mali ya chama ni pamoja na Uwanja wa CCM Kirumba (Mwanza), Samora (Iringa), Sokoine (Mbeya), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Majimaji (Songea), Kaitaba (Kagera) n.k.
Mheshimiwa Spika, pamoja na CCM kuendelea kuhodhi viwanja hivi imeshindwa kuviendeleza na matokeo yake kuwanyima fursa wananchi wa maeneo husika kushuhudia michezo mbalimbali kwa kuwa viwanja hivyo huwa havikidhi viwango vya ubora vya michezo hali inayofanya michezo mingi mikubwa ikiwemo ya kimataifa kufanyika Dar Es Salaam pekee.  Kambi rasmi ya upinzani inarudia tena kuitaka Serikali kuvirudisha viwanja vyote vilivyohodhiwa na CCM kwa wananchi ili viendelezwe kwa kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Michezo nchini kama tulivyopendekeza mwaka jana.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha Mechi ya Taifa Stars na Zimbabwe kuhamishwa kutoka uwanja wa Sokoine Mbeya tarehe 18 Mei na kuhamishiwa uwanja wa Taifa Dar Es Salaam, kwanza kimewavunja moyo mashabiki wa mpira na wakazi wa Mbeya ambao walijiandaa kuonesha uzalendo kwa taifa lao. Kutokana na kitendo cha mechi hii kuhamishwa, Wanambeya walikoseshwa fursa za kujitangaza kiutalii na hatimaye kuchangia katika uchumi kulikosababishwa na Serikali ya CCM kuendelea kuhodhi viwanja vya michezo nchini. Rudisheni viwanja vya wananchi ili viendelezwe na kuwanufaisha wananchi.
6.2 KASUMBA YA MPIRA WA MIGUU KUWA MCHEZO PEKEE WA KIPAUMBELE.
Mheshimiwa Spika, kama Waziri kivuli mwenye dhamana ya kuisimamia Serikali katika masuala ya habari, vijana, utamaduni na michezo. Lakini ni dhahiri kuwa Wizara hii imeshindwa kusimamiwa ipasavyo katika sekta ya michezo,huku soka peke yake ikifanywa kuwa ni mchezo unaopewa kila aina ya msaada na kuidharau michezo mengine. Kwa kifupi ni kuwa, Tanzania ina hazina kubwa ya wanamichezo ambao hawajatumika ipasavyo na wala Serikali haijawekeza vya kutosha katika kuhakikisha kuwa aina nyengine za michezo zinapewa kipaumbele. Kwa mfano, Filbert Bayi ni mwanariadha wa Tanzania ambaye alililetea taifa sifa kubwa kwa kushinda medali ya dhahabu mwaka 1974, tunaye mchezaji wa mpira wa kikapu nchini Marekani Hasheem Thabit anayechezea NBA.
Mheshimiwa Spika, kama taifa kushindwa kuwa na orodha ya wana michezo ambao wamefanya vizuri katika medani ya michezo duniani na kuweza kuwahesabu kwa uchache wao, kunazua maswali mengi sana si kwetu tu bali hata kwa wadau wa michezo nchini ikiwa Serikali ina nia ya dhati ya kuendeleza michezo kwa ujumla.
6.3 MAKOCHA WA KIGENI NA MUSTAKABALI WA MICHEZO NCHINI
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu tumekua tukionesha wasiwasi kwa uamuzi wa Serikali kuendelea kuwaabudu makocha wa kigeni katika michezo. Hali hii si tu kuwa inadumaza soka, bali pia inavunja nguvu makocha wazawa pamoja na kuwakatisha tamaa vijana ambao wamekua na ndoto za kuwa makocha hapa nchini. Hii imekua ni Kasumba ambayo ina athari katika maendeleo ya michezo hapa nchini. Pamoja na makocha wa kigeni kuabudiwa na baadhi ya viongozi wa michezo na wa kitaifa , makocha hawa wamekuwa  na dharau kwa makocha wa nyumbani hali ambayo inadumaza maendeleo haya ya michezo. Imekuwa ni kawaida hata kwa baadhi ya viongozi wa soka wa klabu zetu na hata timu ya taifa kuwathamini na kuwatetemekea makocha kutoka nje pamoja na kwamba tuna zaidi ya miaka 15 sasa na mlolongo mrefu wa makocha wa kigeni, lakini hawajaweza kuleta mafanikio makubwa yanayostahili majina makubwa ya klabu zetu na timu zetu za taifa.
Mheshimiwa Spika, umeshuhudia mara nyingi makocha kutoka nje wakiletwa nchini na kupokelewa na maandamano na shangwe na wanachama na wapenzi wa klabu husika kukifuatwa na kupewa mishahara minono, usafiri wa uhakika na nyumba za kisasa za kuishi. Kuna kocha wa timu mojawapo kubwa ya Tanzania alitaka nyumba atakayopewa kuishi lazima iwe na bwawa la kuogelea, na akapewa. Hii ni sawa na kuwa mtumwa ndani ya nyumba yako mwenyewe. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni inahoji ni nini ambacho makocha wa kigeni wanancho ambacho makocha wazawa hawana kinachofanya Serikali itenge kiasi cha shilingi Bilioni 1.6 kwa ajili ya malipo ya makocha wa kigeni kwa timu za taifa na matumizi ya kawaida ya BMT bila mchanganuo? Je, kwanini Serikali inaendelea kuajiri makocha wa kigeni wakati nchi kuna makocha wenye uwezo wa kufundisha timu za taifa? Je, ni kwanini serikali na wizara hii inasita kuwafadhili kimasomo makocha wazawa nje ya nchi ili waweze kutumikia taifa lao pindi wakimaliza masomo na mafunzo yao?
6.4 MWENENDO WA MCHEZO WA RIADHA
Mheshimiwa Spika; Tanzania imewahi kupata heshima kubwa kimataifa kutokana na mchezo wa riadha.Hata hivyo, katika mchezo huu pia nchi yetu iko katika ‘chumba cha wagonjwa mahututi’.  Hali hiyo, inachangiwa na udhaifu wa kiuongozi, kisera, kimikakati na kioganizesheni kwenye mchezo wa riadha nchini kuanzia ngazi za chini mpaka taifa.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kwamba taifa letu linaweza kutolewa ‘kimasomaso’ na mchezo huu iwapo katika mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2013/2014 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2014/2015 riadha itapewa kipaumbele katika mjadala.
Mheshimiwa Spika; Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imekuwa ikitoa maelezo bungeni kwamba riadha nchini inaendelezwa kupitia wadau mbalimbali ikiwemo Chama Cha Riadha Tanzania (RT). Hata hivyo, Wizara haijawahi kutoa majibu kamili bungeni namna inavyoshughulikia migogoro na matatizo ya kiuongozi na kiutendaji katika chama tajwa hali ambayo inaathiri mustakabali mwema wa mchezo wa riadha nchini.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataarifa kwamba kabla na hata baada ya uchaguzi wa Chama Cha Riadha Tanzania (RT) uliofanyika Morogoro tarehe 20 Mei 2012 kwa nyakati mbalimbali kumekuwepo malalamiko ya wadau wa mchezo huo juu ya uhalali wa uchaguzi huo pamoja na hali tete ya maendeleo ya mchezo huu. Hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ujibu bungeni maswali muhimu yafuatayo kuhusu mustakabali mwema wa riadha nchini:
Mheshimiwa Spika; Mosi, Baada ya kufanya vibaya katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika London 2012 zilitolewa kauli na ahadi mbalimbali na Wizara na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ya kufanya maandalizi bora kuelekea 2016 Rio De Janeiro Olympics; Wizara na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) wanalihakikishia vipi bunge kwamba maandalizi yamekamilika kuondoa ‘ukame’ wa medali na ‘aibu’ kwa taifa?
Mheshimiwa Spika; Pili, Kambi Rasmi ya Upinzani inafahamu kwamba kama sehemu ya diplomasia ya michezo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alilieleza bunge kwamba kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana na Michezo ilipeleka vijana 50 pamoja na walimu wao kwenye makambi ya mafunzo katika nchi mbalimbali ikiwemo New Zeland. Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kwamba mwanariadha Atson Mbugi na Kocha Samwel Tupa nao wapo nchini New Zeland kwenye mazoezi. Hata hivyo, taarifa zilizoifikia Kambi Rasmi ya Upinzani ni kwamba wapo Tanga na Arusha. Je, ni kwanini wameachwa, wakina nani wamepelekwa badala yao na ni kwanini taarifa za uongo zilitolewa kwenye vyombo vya habari? Ni muhimu kwa Bunge kupewa taarifa kwa kuzingatia kuwa kwa nyakati mbalimbali zimekuwepo kashfa za  wanamichezo wasio na viwango kupewa nafasi za wenye vipaji na hatimaye kwenda kulisababishia aibu taifa. Aidha zimekuwepo pia kashfa za wengine kupenyezwa kwenye misafara ya wanamichezo kwa ajili ya kubeba biashara haramu yakiwemo madawa ya kulevya.
Tatu; Wizara na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) walichukua hatua gani baada kupokea tahadhari  ya wanariadha na wataalamu wa riadha juu ya madai ya uchaguzi wa chama hicho kuelekea kufanyika kinyume na Sheria na. 12 ya Baraza la Michezo ya mwaka 1967 kabla ya Mwenyekiti wa BMT Dionis Malinzi na Mkurugenzi wa Michezo Leonard Thedeo kwenda kusimamia Uchaguzi huo?
Mheshimiwa Spika; Nne; mara baada ya uchaguzi huo yapo malalamiko ambayo yaliwasilishwa kwa Waziri yenye kuwasilisha maelezo na vielelezo kuhusu namna uchaguzi huo ulivyokiuka sheria; je, ni sababu zipi zilizoifanya Wizara kutokutoa majibu yoyote juu ya madai hayo?
Tano; Inadaiwa kwamba viongozi wa Chama cha Riadha Tanzania (RT) walisaini Makubaliano ya Maelewano (MOU) mbele ya Viongozi wa Wizara na BMT kwamba marekebisho bora ya katiba ya chama hicho yangefanyika ndani ya siku tisini ambazo zilimalizika tarehe 20 Agosti 2012. Hata hivyo, taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani imeelezwa ni kwamba marekebisho hayo yaliyopaswa kuwezesha mustakabali mwema wa riadha nchini hayajafanyika. Je, Wizara imechukua hatua gani kwa chama hicho na viongozi wake kwa kwenda kinyume na makubaliano hayo?
Mheshimiwa Spika; Sita; Chama Cha Riadha Tanzania (RT) kimekuwa kikipokea fedha za maendeleo ya mchezo wa riadha kutoka Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kwa ajili ya mashindano ya kitaifa na kimataifa. Aidha, Kamati ya Olimpiki (TOC) nayo imekuwa ikipokea fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya pamoja na mambo mengine maandalizi ya wanariadha kwa ajili ya mashindano hayo. Kwa ujumla riadha imekuwa pia ikichangiwa kwa ajili ya maandalizi ya All African Games. Hata hivyo, pamoja na vyanzo hivyo, RT imeburuzwa katika mahakama ya Temeke kwa deni la milioni ishirini ambalo maelezo yake yana utata. Hali hii inaacha maswali kuhusu mapato na matumizi katika RT na TOC. Je, Wizara na BMT wako tayari kuwasilisha nakala ya taarifa zote za mapato na  matumizi yaliyokaguliwa ya RT na TOC ya miaka ya fedha 2012/2013 na 2013/2014?
Mheshimiwa Spika; Kwa hali hiyo tete na tata ya kifedha ambayo inasababisha hata wakati mwingine wanariadha wa Tanzania kukosa vifaa vinavyostahili, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka maelezo kutoka kwa Wizara na BMT, ni nini kilisababisha udhamini wa kampuni ya Lining ya China kwa RT na wanariadha wetu wa toka mwaka 2007 kusitishwa? Je, uamuzi wa TOC kuingia mkataba mwingine na PUMA bila kujadili masharti ya mkataba mwingine uliokuwepo uliathiri vipi mkataba wa awali kwa kuzingatia kwamba yapo madai ya baadhi ya wadau wa riadha kwamba ilikuwa mikataba ya ‘mtaka yote mkosa yote’?
Mheshimiwa Spika; Kwa kuzingatia uzito wa maswali hayo, pamoja na majibu yatakayotolewa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika majumuisho; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ifanye uchunguzi wa masuala haya na mengine yanayohusu RT na TOC ili kuwezesha mustakabali mwema wa mchezo wa riadha nchini. Hata hii italiwezesha bunge kupokea taarifa na kupitisha maazimio yatakayorudisha heshima ya taifa letu kimataifa katika mchezo wa riadha.
7.0 MBIO ZA MWENGE
Mheshimiwa Spika, kwa mufa mrefu Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekua ikipingana na utumiaji wa fedha za walipa kodi na kitendo cha Serikali kuendelea kuwatoza wananchi kwa mashinikizo bila ridhaa zao kuchangia shughuli za mbio za Mwenge wa Uhuru. Ni kweli kuwa Mwenge wa uhuru ni hazina kwa taifa letu jambo ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana nalo na kwa muda mrefu tumependekeza Mwenge wa uhuru uwekwe katika makumbusho ya taifa ili kuweza kuwapatia fursa wananchi kuweza kujifunza hapo.
Mheshimiwa Spika, Suala la kuenzi utamaduni wa Taifa ni la lazima lakini kuendelea kutumia gharama kubwa kwa jambo hili wakati Watanzania wengi hawana huduma muhimu ni dharau kubwa. Aidha, katika kipindi hiki ambacho mwenge wa uhuru unapitishwa katika sehemu mbalimbali za nchi, chama tawala nacho kinapita katika maeneo mbalimbali ya nchi kuangalia utekelezaji wa ilani yake pamoja na kuzindua miradi ya maendeleo ya wananchi. Huu ni usanii mkubwa unaofanywa na Serikali ya CCM kwa dhumuni la kuwanyonya watanzania masikini kwa kigezo cha kuwa wanachangia shughuli za maendeleo wakati ukweli ni kuwa watanzania wanachangishwa mpaka fedha kwa ajili ya malazi na chakula kwa wakimbiza mwenge kama alivyojibu Waziri Mkuu. Na kwa kuwa kumekua na malalamiko kutoka wa wafanyabiashara, wafanyakazi wa Serikali na hasa walimu sehemu mbalimbali nchini kuwa wanalazimishwa kuchangia mwenge bila ridhaa yao. Na kama CCM inataka bado mambo ya mbio za mwenge basi wagharamie wenyewe kwa asilimia 100 na si kuwalazimisha wananchi kuchangia hasa ukizingatia kuwa Waziri Mkuu alitoa kauli wiki hii kuwa kuchangia mbio za mwenge wa uhuru ni hiyari. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kusisitiza kuwa sasa ni wakati muafaka mwenge wa uhuru kupelekwa jumba la Makumbusho ya Taifa. 
8.0 HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, napenda kuhitimisha hoja za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na michezo kwa kulitaka Bunge lako tukufu kuishinikiza Wizara kutekeleza maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo Wizara imekua ikiyakubali kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.
Aluta Continua.
Mheshimiwa Spika, Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, naomba kuwasilisha
…………………………………………..
Joseph Osmund Mbilinyi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo.

29.05.2013

Related

OTHER NEWS 2082315250031718335

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item