SIKU YA MABAHARIA 2014 YAADHIMISHWA
Kila mwaka ifikapo tarehe 25 Juni, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Mabaharia Duniani. Hawa ni watu wanaofanya kazi kwa muda ...
Lakini inasikitisha kuona kwamba, Mabaharia wapatao millioni 1. 5 wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kila siku, lakini hawa ndio injini ya uzalishaji na ukuaji wa uchumi kimataifa. Ni watu wanaoishi na kukabiliana na hatari kwa kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, katika hali mbali mbali za hewa, ni kundi ambalo linapata fursa kiduchu ya kukutana na kuchanganyikana na watu wengine katika Jamii. Kazi ni ngumu inayohitaji uwajibikaji makini.
Mabaharia wanajikuta kwamba, kwa muda mrefu wanatengana na familia zao; wanatishiwa maisha kutokana na vitendo vya kiharamia vinavyofanywa huko Baharini. Siku ya Mabaharia Duniani ni mwaliko kwa wananchi sehemu mbali mbali za dunia kuonesha mshikamano na Mabaharia pamoja na kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na uchumi wa dunia.
Bwana Koji Sekimizu anasema, Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia kwa Mwaka 2013 yalipata mafanikio makubwa kwani vyombo vingi vya mawasiliano ya jamii, vilishiriki katika kuunga mkono kampeni ya maadhimisho ya siku hii. Hata mwaka huu, watu wanahamasishwa kushiriki katika kampeni ya kuunga mkono juhudi za maboresho ya maisha ya Mabaharia sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu ambao wamewaonjesha mamillioni ya watu huduma mbali mbali kwa njia ya bidhaa zinazotumika, kumbe kuna haja ya kusema, asanteni Mabaharia.