HITIMISHO LA SHINDANO LA ELIMU YA UWEKEZAJI KWA WANAZUONI (DSE SCHOLAR INVESTMENT CHALLENGE) KUFANYIKA AGOSTI 13 2014
Soko la Hisa Dar es Salaam (Dar es Salaam Stock Exchange), kwa udhamini wa benki ya NMB, Selcom na FSDT, linapenda kuwajulisha wana...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/08/hitimisho-la-shindano-la-elimu-ya.html
Soko
la Hisa Dar es Salaam (Dar es Salaam Stock Exchange), kwa udhamini wa
benki ya NMB, Selcom na FSDT, linapenda kuwajulisha wanafunzi wa elimu
ya juu nchini walioshiriki katika shindano la elimu ya uwekezaji kwa
mwaka 2014 (DSE Scholar Investment Challenge 2014) kuwa maandalizi yote
ya kuhitimisha shindano hili kwa sasa yamekamilika.
Mchakato
wa kutambua nafasi ya kila mshiriki wa shindano umemalizika. Majina ya
wanafunzi 50 wanaoongoza katika shindano hilo yamebandikwa katika
mtandao wa DSE (www.dse.co.tz) kwenye kipengele cha Investment Challenge.
Sherehe
za kuwatambua washindi na kuwapatia vyeti na zawadi zitafanyika tarehe
13 August 2014 jijini Dar es Salaam. Mialiko ya kuhudhuria sherehe hizo
inaendelea kutumwa kwa njia ya simu.
Shindano
la elimu ya uwekezaji kwa wanazuoni (DSE Scholar Investment Challenge)
lilianza tarehe 01/04/2014 na kumalizika tarehe 30/06/2014. Wanafunzi
washiriki walipewa nafasi ya kutumia simu zao za mkononi ili kununua na
kuuza hisa zinazouzwa katika soko la hisa (DSE) la Dar es Salaam. Kila
mshiriki alipewa mtaji (virtual capital) wa shilingi milioni moja.
Ushiriki kwa shindano hili ulikuwa ni bure na huru kwa yeyote
aliyependa.
Nia
kubwa ya shindano hili ni kuwapatia vijana walio katika vyuo vya elimu
ya juu nchini fursa ya kuwekeza katika soko la hisa kwa majaribio na
kuangalia mitaji yao ikikua. Elimu hii pia ni muhimu katika kujenga
utamaduni wa utunzaji fedha na uwekezaji miongoni mwa vijana walio
vyuoni (ambao ni viongozi, wawekezaji, wahasibu, wachumi, na washauri
watarajiwa).
Washiriki
walitegemewa kushindana kukuza mitaji waliyopewa kwa kipindi cha miezi
mitatu. Mafanikio ya shindano na elimu hii ni makubwa sana. Mwanafunzi
anayeongoza amekuza mtaji wake kutoka shilingi milioni moja aliyopewa na
kufikisha shilingi milioni nne (kwa kipindi cha miezi mitatu tu).
DSE inawapongeza zaidi ya wanafunzi 5,000 walioshiriki katika shindano na elimu hii muhimu kwao na taifa kwa ujumla.
Shindano
na elimu hii imepangwa kufanyika tena mwakani na kuwahusisha wanafunzi
wengi zaidi ya elfu tano walioshiriki mwaka huu. DSE imepanga
kuwawezesha wanafunzi na vijana nchini kutumia simu pamoja na intaneti
mwakani ili kuwapa uwanja mpana zaidi wa kushiriki. Mipango ya baadaye
ni kuwashirikisha wanafunzi walioko kwenye shule za sekondari pia.