SHEHENA YA KEMIKALI YAZUA TAHARUKI, NI BAADA YA TRENI YA MIZGO KUPINDUKA KIJIJI CHA KIFURU MKOANI PWANI.

Mafundi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) wakikarabati kipande cha reli mwishoni mwa wiki kilichoharibika baada ya treni...

Mafundi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) wakikarabati kipande cha reli mwishoni mwa wiki kilichoharibika baada ya treni ya mizigo iliyokuwa imebeba shehena ya madini ya salfa kuanguka katika Daraja la mto Mpiji, kijiji cha Kifuru, wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani. 
(Picha na Fadhili Akida). 

SHEHENA ya kemikali ya salfa iliyoachwa Kijiji cha Kifuru, wilayani Kisararwe na Mamlaka ya Reli ya Tazara na Zambia (Tazara) baada ya treni yake ya mizigo kupata ajali, huenda ikawa tatizo kubwa kwa taifa kama itachelewa kuondolewa. 
Tayari moshi uliotokana na moto uliozuka baada ya mabehewa hayo kupinduka umeshaanza kuleta matatizo kwa wakazi wa eneo hilo.

Baadhi ya wananchi ambao walizungumza na gazeti hili kijijini hapo walisema kuwa kuungua kwa shehena hiyo kumewatia hofu kubwa kutokana na kutambua kuwa kemikali hizo zina madhara makubwa kwa binadamu hasa zinapoingia kwenye maji na kusambaa kwenye hewa. Kijiji hicho kina watu 571.

Aidha katika kipindi hiki ambacho mvua zimeanza kunyesha, wananchi hao wanahofu kwamba kemikali hiyo itaingia Mto Mpiji, ambayo maji yake yanakutana na maji ya Mto Msimbazi ambayo yanatumiwa na wakazi wa Dar es Salaam.

Baadhi yao walidai kupata madhara ya kiafya na kwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe na kuelezwa kuwa hewa chafu ya kemikali hiyo ndio iliyowasababishia madhara hayo na hivyo wakashauriwa kunywa maji mengi pamoja na maziwa ili kuondoa sumu ya kemikali hiyo mwilini.

“Baada ya moshi wa kemikali hiyo kutapakaa kijijini hapa, nilijisikia vibaya mbavu zikaniuma, nilienda pale Kisarawe nikalazwa siku moja, lakini madaktari waliniambia , tatizo langu limetokana na kuvuta hewa chafu,” alisema Latifa Ramadhani.

Naye Mtendaji wa Kijiji cha Kifuru, Mohammed Kaudunde alisema baada ya treni hiyo ya mizigo kuanguka wiki moja iliyopita alisema kijijini hapo wananchi wengi walilalamika afya zao jambo ambalo liliwalazimu kumuita daktari wa wilaya.

“Alikuja daktari wa wilaya hapa na timu yake wakatutangazia tu kwamba tusisogee eneo la tukio na kwamba wananchi wanywe maji mengi pamoja na maziwa,” alisema Kaudunde.

Alisema pia Katibu Tawala wa Wilaya na viongozi wengine wa halmashauri ya wilaya walifika kijiji hapo na wananchi zaidi ya 20 wakalalamika kuathirika na moshi huo kiafya.

Mkuu wa Usalama wa Tazara, Elisha Mhoka alisema tayari Tazara imeshawasiliana na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) ili kusafisha eneo hilo.

Mhoka alisema NEMC walikuwa wanasubiri mafundi wa Tazara wamalize kazi ya kutengeneza reli iliyokuwaimeharibika katika eneo hilo, kazi ambayo wameikamilisha Ijumaa usiku ili waanze kazi hiyo ya kuondoa shehena hiyo ya salfa.

“Wametuambia wakishaiondoa shehena hiyo na kwenda kuiteketeza, pia udongo wa sehemu hii utachimbwa wote kuhakikisha udongo wote ambao umemwagikiwa na kemikali hiyo unaondolewa eneo hili ili kulinda mazingira ya sehemu hii,” alisema.

Alisema ajali hiyo imetokea eneo la mto na akaongeza kuwa kuna haja ya kufanya usafishaji huo haraka kuhakikisha kuwa mvua zitakaponyesha zisije zikasafirisha kemikali hiyo na kuipeleka kwenye visima vya asili vya wananchi.

Daktari Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, Paschal Nkii alipoulizwa na gazeti hili kama kuna wagonjwa ambao wamepelekwa hospitalini hapo kutokana na tatizo hilo la kemikali, alikiri kulifahamu tatizo hilo lakini akagoma kuzungumza kwa kuwa si Mganga Mkuu wa Wilaya.


CHANZO: HABARI LEO

Related

OTHER NEWS 3438731842597336809

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item