WATU 27 WAMEOKOLEWA AJALI YA MTUMBWI ZIWA TANGANYIKA, 6 WAMEFARIKI
Na Mwajabu Hoza Kigoma. WATU sita wamekufa 27 wameokolewa na wengine 11 kulazwa katika hospitali ya rufaa maweni iliyopo Manispaa ya...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/10/watu-27-wameokolewa-ajali-ya-mtumbwi.html
Na Mwajabu Hoza Kigoma.
WATU sita wamekufa 27 wameokolewa na wengine 11 kulazwa katika hospitali ya rufaa maweni iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma baada ya boti walilokuwa wakisafiria kuzama katika ziwa Tanganyika mkoani humo.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari kamishina msaidizi wa polisi mkoa kamanda Jafar Mohamed alisema tukio hilo limetokea majira ya saa nne asubuhi katika kijiji cha Kalalangabo kilichopo mwambao wa ziwa Tanganyika kwenye halmashauri ya wilaya Kigoma.
Kamanda Mohamed alisema chanzo cha tukio hilo ni idadi kubwa ya watu waliokuwa katika boti hilo na kusababisha kuzama majini mita 200 kutoka nchi kavu na kwamba watu hao walikuwa wakielekea kwenye sherehe ya harusi katika kijiji cha Kigalye kilichopo jimbo la Kigoma Kaskazini mkoani humo.
Alisema watu waliopatikana ambao ni marehemu ni watu sita wakiwemo watoto wawili kati ya hao mmoja ametambuliwa kwa jina la Salama Juakali (37) huku wengine majina yao yakiwa hayaja tambuliwa hadi sasa.
Kamanda amesema hatua za uokoaji zinaendelea sanjari na taratibu za kuhakikisha waliohusika na tukio hilo wanafikishwa katika vyombo vya sheria kujibu tuhuma inayowakabili.
Kwa mujibu wa taarifa ya mwenyekiti wa wavuvi katika mwalo wa Kibirizi uliopo Manispaa ya Kigoma Ujiji Sedwe Ibrahimu alieleza idadi ya watu waliozama majini inasadikiwa kuwa zaidi ya watu 64 ambao walikuwa wakielekea harusini.
Alisema mitumbwi iliyosababisha ajali ilikuwa miwili ambayo ni maalum kwa kuvulia samaki na dagaa hivyo ilitumika kusafirishia abiria baada ya kukodiwa kwa lengo la kuwfikisha maharusi katika kijiji cha Kigalye wakitokea katika kijiji cha Mwandiga jimbo la Kigoma Kaskazini ndipo walipokutwa na janga hilo.
Akifafanua kuhusu tukio hilo baada ya kupatiwa tarifa ya kuzama kwa mitumbwi miwili iliyokuwa imebeba watu waliokuwa katika magari matatu aina ya Hiace pamoja bodaboda tatu kiasi ambacho kinaashiria watu hao walikuwa wengi ukilinganisha na uwezo wa mitumbwi hiyo ambayo hubeba watu 20 tu wakati wa shughuli za uvuvi.
Alieleza eneo ambalo walitumia kupakia abiria hao ilikuwa katika kijiji cha Kalalangabo ambapo si rasmi kwa kupakia abiria kisheria na hivyo kutakiwa kutumia eneo la kibirizi ambalo limetengwa kisheria.
Baaadhi ya wahanga wa tukio hilo akiwemo Zainabu Issa na Mariamu Juma (18) ambaye ni bibi harusi alisema chanzo ni baada ya mitubwi hiyo kukumbwa na wimbi la maji sambamba na idadi kubwa ya watu takribani 80 ambao walikuwa katika mitumbwi hiyo.
Muuguzi wa zamu katika wodi namba tano Haika Masula alisema wamepokea majuruhi 10 na maiti tatu mwanamke mmoja alitambuliwa kwa jina la Salama Juakali na watoto wawili waliochini ya umri wa miaka mitano.
Picha na Michuzi Blog