BALOZI WA KUDUMU WA UMOJA WA MATAIFA AUGUSTINE MAIGA AKUTANA NA RAIS DK.SHEIN
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akibadilishana mawazo na Balozi wa kudumu wa Umoja wa Mat...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/11/balozi-wa-kudumu-wa-umoja-wa-mataifa.html
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
akibadilishana mawazo na Balozi wa kudumu wa Umoja wa Mataifa (Mstaafu) wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, New York, Marekani Mhe. Augustine Maiga
alipofika Ikulu Mjini Unguja leo.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
akibadilishana mawazo na Balozi wa kudumu wa Umojawa Mataifa(mstaafu) wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, New York, Marekani Mhe. Augustine Maiga
alipofika Ikulu Mjini Unguja leo ( Picha na Ikulu Zanzibar)
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
19.11.2014
MAFANIKIO yaliofikiwa katika uimarishaji wa miradi
ya maendeleo hapa Zanzibar sambamba na vivutio vyake vya utalii yote kwa pamoja
yameweza kuijengea sifa kubwa Zanzibar Kimataifa.
Balozi wa Kudumu
wa Umoja wa Mataifa (Mstaafu) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Augustine
Maiga aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo
yake Balozi Maiga, alimueleza Dk. Shein kuwa jina la Zanzibar limekuwa ni
kigezo kikubwa cha mafanikio yaliopatikana katika miradi yake ya maendeleo
ikiwemo kupambana na Malaria, kupunguza vifo vya akina mama na watoto, elimu,
maambukizo ya virusi vya Ukimwi pamoja na sekta nyengine za kimaendeleo.
Akitolea mfano
mafanikio yaliopatikana katika kupambana na Malaria, Balozi Maiga alisema kuwa
Zanzibar imeweza kupata mafanikio makubwa ambayo ni ya kuigwa kwa nchi nyengine
duniani hatua ambayo Umoja wa Mataifa nao unajivunia kwa hilo hasa katika
kufikia Malengo ya Milenia.
Aidha, Balozi
Maiga alimueleza Dk. Shein kuwa utalii wa Zanzibar umeweza kuwa ni kivutio
kikubwa duniani hatua ambayo imepelekea watalii wengi kuwa na hamu ya kuja
kuitembelea Zanzibar kutokana na vivutio vyake zikiwemo fukwe pamoja na sehemu
zake za kihistoria.
Balozi Maiga pia,
alitoa pongezi ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa Umoja wa Mataifa mara
kwa mara kwa Zanzibar kutokana na kufanikiwa kuwepo kwa pamoja mashirikika ya
Umoja wa Mataifa ‘ONE UN’ hapo katika Jengo la ZSTC Kinazini hali ambayo
imeweza kuleta ufanisi mkubwa wa kikazi kwa mashirikika hayo hatua ambayo
imeweza kuigwa na nchi nyengine duniani kama vile Vietnam.
Akimueleza Rais
juu ya juhudi mbali mbali alizozichukua katika utendaji wake wa kazi akiwa New
York, Marekani pamoja na wakati alipokuwa nchini Somali katika mikakati ya kusaka
amani ya nchi hiyo, Balozi Maiga alisema kuwa Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar umewavutia nchi kadhaa ambazo wako tayari kuja kujifunza kutokana na
mafanikio yake.
Pamoja na hayo,
Balozi Maiga alimueleza Dk. Shein kuwa Tanzania imeweza kupata pongezi kubwa na
kuweza kujijengea sifa kubwa ndani ya Umoja wa Mataifa kwa harakati zake za
kuunga mkono harakati za kusimamia amani katika ndani na nje ya bara la Afrika.
Balozi Maiga aliongeza
kuwa kumeshajitokeza Makampuni kadhaa ambayo yana nia ya kuunga mkono sekta ya
elimu kwa lengo la kuanzisha Mradi wa Maktaba kwa kuanzisha maktaba kwa ajili
ya kuwasaida wanafunzi pamoja na wanajamii
sambamba na kuwajengea uwezo vijana kujifunza masomo ya kompyuta kwa
kushirikiana na Wizara husika ambapo kati ya maeneo sita ya Tanzania
yatakayojengwa maktaba hizo, Zanzibar nayo imepata fursa hiyo.
Nae Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa
pongezi zake kwa Balozi huyo wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa (Mstaafu) wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa kuitumikia vyema nchi yake katika kipindi chake
chote alichofanyakazi ndani ya umoja huo.
Dk. Shein alisema
kuwa Zanzibar imeweza kujijengea sifa kubwa Kimataifa kutokana na mashirikiano
mazuri inayopata sambamba na juhudi za makusudi inazozichukua katika kuimarisha
miradi yake ya maendeleo ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Alieleza kuwa mafanikio
yaliopatikana katika kupambana na Malaria pamoja na kupambana na maambukizo ya
virusi vya Ukimwi na kupunguza vifo vya akina mama wajawazito yameweza
kuijengea jina Kimataifa huku akisisitiza kuwa juhudi zitaendelea kuchukuliwa
na Serikali anayoiongoza.
Kwa upande wa
sekta ya utalii, Dk. Shein alieleza kuwa ndani ya miaka mitatu iliyopita idadi
ya watalii imeongezeka kwa kiasi kikubwa huku akieleza mikakati ya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar katika kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia mwaka 2016.
Dk. Shein alisema
kuwa miongoni mwa juhudi zinzochukuliwa hivi sasa ni pamoja na ujenzi wa Jengo
jipya la abiria,njia za kutulia na kurukia ndege pamoja na maegesho ya ndege
ambapo pia alimueleza azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukiimarisha
kiwanja cha ndege cha Pemba ikiwa ni pamoja na kukiweka taa ili ndege ziweze
kuruka na kutua wakati wote.
Akizungumzia
suala la usalama kwa watalii, Dk. Shein alisema kuwa Serikali inachukua juhudi
za makususdi katika kuhakikisha suala la usalama kwa watalii linafanyiwa kazi
kwa kuvishirikisha vikosi vya ulizi na usalama vya Serikali kwa mashirikiano ya
pamoja na Polisi jamii hatua ambayo imeendelea kuipa heshima kubwa Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk