MNUNUZI WA NYUMBA/KIWANJA HII NI NAMNA YA KITAALAM YA KUJUA ENEO UNALONUNUA KAMA LINA MGOGORO AU HAPANA
Na Bashir Yakub Makala zilizopita nilieleza mambo au taarifa muhimu zinazopaswa kuwa kwenye mkataba wako unapokuwa u...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2015/01/mnunuzi-wa-nyumbakiwanja-hii-ni-namna.html
Na Bashir Yakub
Makala
zilizopita nilieleza mambo au taarifa muhimu zinazopaswa kuwa kwenye
mkataba wako unapokuwa unanunua nyumba/kiwanja. Nikasema katika
niliyosema kuwa mkataba lazima uoneshe ukitokea mgogoro utatatuliwa
vipi, ueleze kuwa utapotokea mgogoro muuzaji lazima awajibike
kuhakikisha anakupa ushirikiano mnunuzi ili kumaliza mgogoro huo na
kuwa muuzaji kama ana mke basi mke wake ni lazima aandaiiwe
nyaraka iitwayo ridhaa ya mwanandoa ambayo ni tofauti na mkataba
na aisaini pamoja na kuweka picha yake. Nilieleza mengi lakini
hayo ni baadhi tu.
Kwa
wale ambao hawakubahatika kuyasoma hayo basi waandike neno MAKALA
SHERIA kwenye google watapata makala hizo. Leo tena naeleza hatua
muhimu sana au ya lazima na lazima haswaa kwa mnunuzi wa
kiwanja/nyumba ambayo anatakiwa apitie kabla ya kufanya
manunuzi.Hatua hii kwa jina la kitaalam huitwa OFFICIAL SEARCH kwa
lugha rahisi tu waweza kuiita utafiti,upekuzi, upembuzi au upelelezi
rasmi ambayo hufanywa na wanasheria. Mi napenda niite upelelezi.
( 1 ) AINA ZA VIWANJA/NYUMBA UNAPOTAKA KUFANYA UPELELEZI KUJUA KAMA KUNA MGOGORO.
Nyumba/viwanja
tunavyouziana kila siku vimegawanyika katika hadhi mbalimbali.
Kwanza kuna nyumba/viwanja vyenye hati, vyenye leseni za makazi,
vyenye ofa na ambavyo havina hati, leseni ya makazi wala ofa.
Kutokana
na makuzi ya miji yetu viwanja/nyumba zenye hati mara nyingi huwa ni
chache sana.Zenye leseni za makazi ni nyingi kiasi na haya ni maeneo
ambayo hasa hujulikana kama uswahilini. Zenye ofa huwa ni chache nazo
kwakuwa ofa ni hatua anayopitia mtu anapoelekea kupata hati au
leseni ya makazi.
Pia
maeneo ambayo hayana hati wala leseni ya makazi wala ofa nayo ni mengi
sana pia. Kwa Dar es salaam haya ni maeneo ya pembeni pembeni mwa
mji Tegete,bunju, pugu, chanika, mbagala, baadhi ya maeneo ya kigamboni
n.k. Hata hivyo eneo liwe na hati leseni ya makazi au hapana bado
kisheria linatambulika .
( 2 ) NAMNA YA KUJUA KAMA NYUMBA/KIWANJA KINA MGOGORO
Kama
kiwanja/nyumba ina hati kuna maombi rasmi ya kisheria ambayo huwa
yanafanywa kwenda ardhi wizarani, wizara ya ardhi makao makuu kwa
Dar es salaam na kwa mikoani maombi hayo mara nyingi huenda makao
makuu ya mkoa ambapo katika maombi hayo mnunuzi anaiomba mamlaka
ya ardhi imjulishe mambo yafuatayo;
( a ) KUJUA JINA LA MMILIKI HALALI WA NYUMBA/KIWANJA.
Kwanza
kujua jina la mmiliki. Jina hili linatakiwa kufanana sawasawa bila
tofauti yoyote na yule mtu anayetaka kukuuzia eneo. Hii husaidia
kuthibitisha kuwa anayeuza ndiye kweli mmiliki wa eneo.Kama majina
yatatofautiana basi haraka sana achana na hilo eneo ili kuepuka
mgogoro.
( b ) KUJUA KAMA NYUMBA/KIWANJA UNACHONUNUA KIMEWEKWA KAMA DHAMANA YA MKOPO.
Kitu
kingine unachouliza kwenye hayo maombi rasmi ni kama hiyo
nyumba/kiwanja kimewekwa kama dhamana kwa ajili ya vitu kama mkopo .
Wakati mwingine yawezekana mtu kukuuzia eneo ambalo limewekwa
dhamana kwa mkopo wa hela nyingi tu. Na kisheria kama eneo limewekwa
dhamana yule anayelimiliki kwa dhamana ndiye mwenye nalo kwa muda huo
na wewe uliyenunua sheria iko wazi unakuwa umeliwa.
Ieleweke
kuwa ni vigumu sana kujua kama eneo unalouziwa limewekwa dhamana au
hapana ikiwa hukufanya upelelezi huu. Wakati mwingine mtu huweka
dhamana eneo lake na kubaki na hati . Kwa hati ile wewe mnunuzi ni
rahisi kuhadaika kuwa eneo ni lake lakini kumbe ni eneo lenye deni
kubwa. Ukinunua eneo kama hilo utakuwa umenunua mgogoro mkubwa ambao
wewe mnunuzi kushindwa na kunyanganywa ulichonunua ni lazima tu.
( c ) KUJUA KAMA KUNA MGOGORO WA KIFAMILIA.
Kitu
kingine ambacho utaomba kujua katika yale maombi ni kama kuna
mgogoro wowote wa kifamilia kama migogoro ya mirathi, migogoro ya
kindoa ambapo mwanandoa mmoja anaweza kuwa ameweka zuio kuhusu uuzwaji
wowote wa nyumba/kiwanja hicho. Usipofanya upelelezi huu utanunua
halafu siku ya kubadilisha jina ndio siku utajua kuwa eneo lile lilikuwa
haliruhusiwi kuuzwa.
Aidha ifahamike kuwa mamlaka za ardhi hupata taarifa hizi za viwanja vya watu kupitia utaratibu wa mazuio uitwao CAVEAT.
( 3 ) MNUNUZI WA ENEO LENYE LESENI YA MAKAZ I AKAFANYE UPELELEZI WAPI.
Maeneo
yenye leseni za makazi maombi haya ya upelelezi wa kiwanja/nyumba
yanapelekwa manispaa. Manispaa inayohusika ni ile ambayo lilipo eneo
husika . Kwa mfano ukitaka kununua eneo kinondoni manispaa ya
kinondoni ndiyo inayopelekewa maombi, kama eneo unalotaka kununua lipo
temeke basi manispaa ya temeke ndio ipelekewe maombi. Aidha kuhusu
mpangilio wa maombi na kile unachotaka kujua kuhusu eneo ni kama
nilivyoeleza hapo juu kwenye hati .
( 4 ) MAENEO AMBAYO HAYANA HATI, LESENI ZA MAKAZI UPELELEZI HUFANYIKAJE.
Kwakuwa
maeneo ya namna hii yanakuwa hayana nyaraka yoyote maalum katika
mamlaka za serikali basi wakati mwngine huleta ugumu kidogo katika
kujua ukweli ili kuepuka mgogoro. Lakini kitu ambacho huwa tunashauri
katika maeneo ya hivi ni kuwa kwanza muuzaji akueleze eneo
alilipataje. Kama alilinunua kwa mtu ni vema akaonesha ule mkataba
alionunulia na kama mauzo yatafanyika basi ni lazima mnunuzi apate
kopi ya ule mkataba.
Pili
kama amelirithi ni lazima aoneshe fomu ya usimamizi wa mirathi
ambayo ndiyo itakuwa inampa mamlaka ya kuuza. Na kama alipewa zawadi
basi aonesha waraka wa zawadi ( deed of gift) ambao umesajiliwa.
Jingine la msingi sana katika maeneo yasiyo na hati wala leseni za makazi huwa ni kuuliza majirani.
Eneo
unalonunua kama wapo majirani hebu waulize tu kwa nia njema na mara
nyingi ukiwapata wawili watatu hivi ni rahisi kupata ukweli au
kukuwezesha kujenga shaka. Na majirani usiwaulize kwa pamoja, mtafute
mmoja mmoja kila mtu kwa muda wake ili kuepusha kuoneana haya katika
kusema ukweli. Pia hakikisha wakati wa kuwahoji majirani muuzaji
asiwepo, we tafuta tu muda wako nenda peke yako na pata taarifa.
Uwepo wa muuzaji unaweza kuingilia( influence) ukweli. Usikurupuke
utalia, ni hayo kwa leo.
MWANDISHI
WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA
KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE ,
GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com
Source: Michuzi