Balozi Juma Mwapachu awa Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi Airtel Tanzania

     Balozi Juma Volter Mwapachu   KAMPUNI tanzu ya Bharti Airtel inayoongoza katika utoaji wa huduma za simu za mkononi ikifanyak...

     Balozi Juma Volter Mwapachu
 
KAMPUNI tanzu ya Bharti Airtel inayoongoza katika utoaji wa huduma za simu za mkononi ikifanyakazi katika nchi 20 Asia na Afrika, leo imemteua Balozi Juma Volter Mwapachu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Airtel Tanzania.

Balozi Mwapachu ni Katibu Mkuu aliyepita wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, nafasi aliyoishika kati ya Aprili 2006 na Aprili 2011. Kabla ya uteuzi huu, Mwapachu alikuwa Balozi Mwakilishi Ufaransa na UNESCO.

Mwapachu ni mhitimu wa shahada ya sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Pia ni mhitimu wa Diploma ya Juu ya Sheria ya Kimataifa, Masuala ya Diplomasia ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Sheria za Kimataifa na Diplomasia huko New Delhi, India.

Pia ana shahada mbili za heshima katika fasihi na sayansi ya siasa za UDSM na Chuo Kikuu cha Taifa Rwanda.

Akizungumzia uteuzi huo, Christian de Faria, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Airtel Africa, alisema: “Ni faraja kwetu Balozi Mwapachu kuiongoza Bodi yetu ya Wakurugenzi nchini Tanzania. Uzoefu wake mkubwa utaongeza thamani kubwa kwa Bodi yetu na kutoa miongozo bora ya kimkakati katika shughuli zetu nchini Tanzania. Tunaamini pia kuwa atadumisha mahusiano na wadau mbalimbali nchini.”

Kwa upande wake, Balozi Mwapachu alisema: “Ninaipokea kwa heshima kubwa fursa hii ya kujiunga na Bodi ya Wakurugenzi ya Airtel, na kwa pamoja na wajumbe wenzangu wa Bodi hii ya wakurugenzi wa Airtel, tutashirikiana kujenga kampuni thabiti yenye misingi imara ili kuendelea kutoa huduma bora ya mawasiliano nchini Tanzania.

“Sekta ya mawasiliano ina mchango mkubwa katika kukua kwa uchumi wetu ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha wananchi kila mahali. Pia ukuaji wa teknolojia ya hali ya juu na ubunifu katika masoko ikisaidiwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa sekta hii ni dhahiri kutakuwa na uwezekano kwa sekta hii ya mawasiliano kuendelea kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya taifa.”

Balozi Mwapachu ana uzoefu mkubwa katika masuala ya kuongoza bodi mbalimbali kwani amewahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) na Shirika la Reli Tanzania (TRC). Pia alikuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya East African Breweries Limited, Kenya.

Kwa sasa yumo katika bodi kadhaa za taaasisi binafsi ndani na nje ya nchi. Ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Uzoefu wake wa kiuongozi katika mashirika na sekta binafsi Tanzania na eneo la Afrika Mashariki utaleta tija katika uongozi wake wa Airtel Tanzania.

Related

OTHER NEWS 7386847458758476648

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item