NAIBU SPIKA ADAIWA KUMPIGA MGOMBEA CCM

Dodoma.  Kampeni za wagombea ubunge wa Jimbo la Kongwa juzi zilikumbwa na tafrani baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kudaiwa ...


Dodoma. 
Kampeni za wagombea ubunge wa Jimbo la Kongwa juzi zilikumbwa na tafrani baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kudaiwa kumchapa fimbo na baadaye kumpiga ngumi mgombea mwenzake aliyeanguka na kuzirai.
Mgombea huyo, Dk Joseph Chilongani, ambaye hivi sasa amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kongwa, alipata kipigo hicho juzi saa 10.20 jioni wakati walipokuwa kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Ugogoni wilayani Kongwa.
Kwa kawaida, wagombea ubunge wa CCM hupelekwa pamoja na chama hicho kwenye mikutano ya kampeni ya kila kata ambako hujieleza kwa wanachama kabla ya siku ya kupigiwa kura.
Mpambe wa Dk Chilongani, Shaaban Chihimba alimwambia mwandishi wetu kuwa Ndugai alimshambulia mpinzani wake kutokana na kukasirika baada ya mgombea mwingine, Simon Katunga kujinadi kwa kuponda utendaji wa mbunge wa sasa wa Kongwa.
“Mgombea huyo alisema fedha zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika halmashauri yetu zimekuwa zikiliwa hivyo akichaguliwa atahakikisha fedha hizo zinatumika kwa mambo yaliyokusudiwa,” alidai Chihimba.
 Alisema kuwa kauli hiyo ilionekana kumkera  Ndugai, hali iliyomfanya kusimama na kutaka kwenda kumpiga mgombea huyo, lakini viongozi wa CCM walimzuia.
 “Akiwa anataka kuketi, alimuona Dk Chilongali akirekodi tukio hilo kwa kutumia simu ya mkononi, ndipo alipomwendea na kumpiga ngumi za usoni na fimbo kwenye tumbo hali iliyosababisha kuanguka chini na kuzirai,” alidai.
Video ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii, inamuonyesha Ndugai akiwa ameshikilia fimbo mkononi huku akisema “embu na wewe usinipige, unanipiga makamera ya nini?”
Chihimba alidai kuwa baada ya mgombea huyo kuanguka, mkutano huo ulivurugika na wagombea wengine wakishirikiana na baadhi ya wanachama walimchukua Dk Chilongani na kumpeleka kabla ya kupelekwa hospitali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema jana jioni kuwa Dk Chilongani alifika Kituo cha Polisi Kongwa na kutoa taarifa za kushambuliwa kichwani na tumboni kwa fimbo.
“Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa kuwahoji watu waliokuwapo na mara baada ya upelelezi kukamilika jalada litapelekwa kwa wakili wa Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa hatua stahiki za kisheria,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Ndugai alijibu kupitia ujumbe mfupi wa simu akisema: “Ni kweli kumetokea mtafaruku, lakini hakuna aliyepigwa ngumi. Na katika maisha yangu sijawahi kumpiga mtu ngumi.”
Mganga mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dk Festo Mapunda alikiri kupokewa kwa mgombea huyo juzi jioni lakini alikataa kuzungumza zaidi.
Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Peter Minja alikiri kutokea kwa tukio hilo lakini akasema si kwa ukubwa huo. “Leo asubuhi (jana), tutakuwa na kikao cha kulijadili na baadaye tutatoa taarifa... tunaendelea na kampeni,” alisema Minja.
Hata hivyo, Minja alikataa kuthibitisha iwapo ni kweli mgombea huyo alipigwa au kukanusha kwa madai kuwa hakuwepo eneo la tukio.
“Tulishamuita mgombea huyo na kumuonya kuhusu kujinadi kwa kukipaka matope chama na halmashauri kwa sababu Halmashauri ya Kongwa imepata cheti safi cha (Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali - CAG), lakini hakusikia aliendelea.
“Tumepata taarifa ya maneno, lakini tunasubiri ya maandishi, taarifa ya polisi na hospitali kwa kuwa utaratibu wa chama unasema kila mwenye malalamiko awasilishe katika vikao husika.”
Minja alisema alikwenda jana hospitalini kumuona mgonjwa huyo, lakini hakuweza kuzungumza naye.
Hata hivyo, alisema jana polisi waliwahoji baadhi ya viongozi, wanachama na wagombea kuhusu tukio hilo.
Alisema tukio hilo limesababisha mchakato wa kampeni za kura za maoni kusimama hadi leo.
“Tulikuwa tumebakiza kata mbili za Sejeli na Kongwa Mjini ambazo zimesalia kwa watia nia kupiga kampeni na hizi tutamalizia kesho,” alisema.
Source: Mwananchi

Related

OTHER NEWS 5956047875255258397

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item