Wizara ya Nishati, Kilimo waanza kuhamia Dodoma

KATIKA kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kutaka serikali kuhamia Dodoma, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba am...


KATIKA kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kutaka serikali kuhamia Dodoma, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amesema watendaji wa wizara hiyo wataanza kuhamia Dodoma kuanzia wiki ijayo.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa amewataka wakuu wa idara na vitengo wote wa wizara hiyo kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma na kuwa wametekeleza agizo hilo ifikapo mwezi Septemba, mwaka huu.  Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Dk Tizeba alisema tayari watendaji wa wizara hiyo wanaotakiwa kuhamia Dodoma wameanza kufanya maandalizi ya safari.

Alitoa dokezo hilo mara baada ya kutoa taarifa kuhusu Mkutano wa Ushirikishwaji wa Wadau kwenye Sekta ya Uvuvi, unaoishirikisha pia Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wadau mbalimbali.  “Ni kweli hata sisi Wizara tuko kwenye maandalizi wiki hii, kwa sababu wiki ijayo tutahamia Dodoma, tunatekeleza agizo la Rais,” alisema Waziri Tizeba. 

Kauli ya Waziri Tizeba imekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutangaza kuhamia Dodoma ifikapo Septemba mwaka huu, huku akiwataka Mawaziri na Naibu Mawaziri kumfuata.  Waziri Mkuu alisema ameshaagiza ukarabati kwenye nyumba yake ukamilishwe ili ifikapo Septemba aweze kuhamia na kuwataka mawaziri kufanya hivyo kwa sababu kila Waziri ana nyumba na ofisi ndogo mjini Dodoma. 

Nayo Wizara ya Nishati na Madini imetoa waraka ikiwataka wakuu wa idara na vitengo wote wa wizara hiyo kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.  Agizo hilo lipo katika waraka uliotolewa na Kabibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa jana na nakala yake kutumwa pia kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. 

Katibu Mkuu huyo alisema agizo hilo linatokana na kauli iliyotolewa na Rais Magufuli katika Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni, ambapo alisisitiza azma ya serikali yake kuhamia Dodoma.

 Alisema pamoja na kauli ya Rais, watendaji hao wanatakiwa kuanza maandalizi ya kuhamia Dodoma ifikapo Septemba kutokana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuahidi kuhamia Dodoma mwezi huo na kuwataka Mawaziri na Naibu Mawaziri nao kumfuata.

Related

TUJUZANE 6388345859692440715

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item