VITUO 304 VYA AFYA VINA HALI MBAYA ZAIDI

MATOKEO ya tathmini ya kuvipatia madaraja vituo vya huduma za afya ya msingi, iliyofanyika katika mikoa 20 nchini, yametolewa yakiones...



MATOKEO ya tathmini ya kuvipatia madaraja vituo vya huduma za afya ya msingi, iliyofanyika katika mikoa 20 nchini, yametolewa yakionesha vituo 304 viko katika hali mbaya zaidi.

Hali hiyo imesababisha vipatiwe fedha kwa ajili ya kufanya maboresho. Vituo hivyo 304 kutoka mikoa ya Tanga, Dodoma, Kigoma na Singida ni sehemu ya vituo 1,932, sawa na asilimia 36, vilivyopangwa kwenye daraja la nyota sifuri.

Kulingana na taarifa ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) iliyowasilishwa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa, vituo vilivyo kwenye daraja la juu; nyota tatu, ni asilimia moja kwa maana ya vituo 67. Aidha, vituo 2,745 sawa na asilimia 52 viko nyota moja na 582 sawa na asilimia 11 ni katika nyota mbili.

Akiwasilisha taarifa hiyo kwa kamati ya bunge, Mkurugenzi Msaidizi, katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Afya) Rasheed Maftah alisema vituo 304 vilivyo katika hali mbaya zaidi, kila kimoja kimepatiwa Sh milioni 10 kwa ajili ya kufanya maboresho. Fedha hizo, Sh bilioni 3.04, zimetolewa na Benki ya Dunia kwenye mradi wa huduma za msingi za afya.

Licha ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya vituo hivyo vilivyo katika hali mbaya, Maftah alisema hatua nyingine zilizochukuliwa baada ya tathimini ni kuelekeza kila kituo, kilichopata chini ya nyota tatu kutengeneza mpango wa uboreshaji.

Maeneo ya kipaumbele ya kuboreshwa ni miundombinu ya maji, nishati ya umeme, vyoo vya kisasa, ukarabati mdogo wa majengo, vifaa vya utakasishaji na vifaa vya tiba ya dharura ikiwemo kuweka masanduku ya maoni.

Mtoaji wa nyota ni wizara yenye dhamana na sekta ya afya na lengo ni kuhakikisha asilimia 80 ya vituo vyote vya kutolea afya ya msingi, vinafikia kiwango cha nyota tatu na zaidi ifikapo Juni 30, 2018. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vigezo vya utoaji alama vilizingatia maeneo 12 kabla ya kuja na madaraja husika.

Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na kuangalia huduma za kitabibu kwa kuzingatia kama kituo kina chumba cha daktari, usiri wa kuhudumia wagonjwa na kuzalisha wajawazito.

Eneo lingine lililoangaliwa ni huduma za dawa, maabara, upasuaji kwa maana ya kuangalia kama kituo kina mtaalamu wa dawa, sehemu stahili ya kuzihifadhi na uwekaji kumbukumbu wa dawa zinazotoka na kupokewa.

Huduma kwa wateja ni eneo lingine ambalo watathimini walilizingatia kwa maana ya mkataba wa huduma kwa wateja, haki na wajibu wa mgonjwa pamoja na sanduku la maoni katika kituo husika.

Kuhusu uwajibikaji, timu ya utathimini iliangalia kama kituo kina kamati ya afya iliyo hai. Vile vile kwa upande wa mpangilio wa huduma, walizingatia kama kituo kina bango la kutambulisha, saa za kuona wagonjwa, taarifa za mapato na matumizi zilizo wazi, mpango wa afya wa mwaka, bei za dawa, ratiba ya elimu ya afya na ratiba ya kliniki maalumu.

Wakichangia taarifa hiyo, wabunge wengi walisisitiza serikali kufanyia kazi tatizo la dawa na upungufu wa watumishi katika vituo vya kutolewa huduma za afya kuanzia zahanati hadi hospitali. Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje alisema Bohari ya Dawa (MSD) imekuwa ikilaumiwa juu ya suala zima la usambazaji dawa wakati tatizo lake ni upungufu wa fedha.

Mbunge wa Mbulu Mjini, Issaay Paulo alisisitiza mapato kuanzia zahanati hadi hospitali yakusanywe kwa kutumia mashine za kielektroniki ili kuziba mianya ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya bunge, Jasson Rweikiza aliitaka serikali iagize wakurugenzi wa halmashauri kwa kuwapa muda wa kuhakikisha kila mzee, anapatiwa kitambulisho kwa ajili ya kupata matibabu bure.

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu), Bernard Makali, alikiri sekta ya afya kukabiliwa na changamoto. Aliwahakikishia wajumbe hao wa kamati kuwa maoni yao wameyapokea na watayafanyia kazi.

Related

OTHER NEWS 2463557195855958669

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item