Amani yaanza kutengamaa Sudan Kusini
Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Salva Kiir amemtumia ujumbe Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya y...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2016/09/amani-yaanza-kutengamaa-sudan-kusini.html
Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini
Salva Kiir amemtumia ujumbe Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akimuarifu kuwa hali ya
usalama katika nchi hiyo imeanza kutengemaa.
Rais Salva Kiir
Mayardit amewasilisha ujumbe huo kupitia kwa Mjumbe wake Maalum Mhe.
Aggrey Tisa Sabuni ambaye pamoja na kuwasilisha ujumbe huo amesema
Sudani Kusini imekamilisha nyaraka za azimio la kuridhia mkataba wa
kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao umewasilishwa tarehe 05
Septemba, 2016 katika makao makuu ya Jumuiya Jijini Arusha.
Mhe.
Aggrey Tisa Sabuni amesema Sudan Kusini ipo tayari kushirikiana na nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala mbalimbali yenye
manufaa kwa wananchi ikiwemo biashara na uwekezaji na kwamba ni
matumaini yake kuwa itapata ushirikiano mzuri.
Kwa upande wake
Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na taarifa za kutengemaa kwa
hali ya amani nchini humo na kwamba ni matarajio yake kuwa Sudan Kusini
itajikita katika maendeleo ya wananchi wake.
Katika hatua
nyingine, Rais Magufuli amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya
Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza ulioletwa na Mjumbe Maalum wa Rais huyo
Mhe. Aime Laurentine Kanyana.Katika ujumbe huo Rais Nkurunziza amesema
hali ya Burundi ni shwari na kwamba wananchi wa Burundi wanaendelea na
shughuli zao kama kawaida.
Kwa upande wake Rais Magufuli amesema
Tanzania yenye wakimbizi takribani 200,000 wa kutoka Burundi
inafurahishwa na taarifa za kuwepo hali ya amani nchini humo.