MATOKEO YA MECHI ZA LIGI KUU TANZANIA BARA
Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara imeendelea hii leo ikiwa kwenye mzunguko wake wa pili baada ya kuanza siku ya jumamosi ya wiki iliyopita ...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/08/matokeo-ya-mechi-za-ligi-kuu-tanzania.html
Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Dar young Africans hii leo walikuwa uwanja wa Taifa Dar Es Salaam ambapo walikuwa wenyeji wa Coastal Union toka Tanga . Yanga wamejikuta wakipunguzwa kasi na ‘Wagosi Wa Kaya’ baada ya kulazimishwa sare ya 1-1.
Yanga ndio walioanza kufunga kwenye dakika ya 69 kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi Didier Kavumbagu .
Huku wengi wakitegemea mchezo huo kumalizika kwa ushindi wa mabingwa hao Mwamuzi wa mchezo huo aliwazawadia Coastal Union penati kwenye dakika ya 86 ambapo kiungo toka Kenya Jerry Santo alifunga penati hiyo na kufanya matokeo kuwa 1-1.
Timu zote mbili zilimaliza mchezo huo zikiwa na wachezaji tisa ndani ya uwanja baada ya mwamuzi kuwaonyesha kadi nyekundu Simon Msuva wa Yanga na Crispin Odula wa Coastal Union.
Katika michezo mingine mahasimu wa jadi wa Yanga Wekundu wa Msimbazi Simba Sports Club walipata ushindi wao wa kwanza baada ya kuwafunga JKT Oljoro 1-0 . Bao pekee la Simba kwenye mchezo huo lilifungwa na kiungo mchezeshaji Haruna Chanongo.
Azam Fc waliwafunga maafande wa Rhino Rangers 2-0 huko Tabora ambapo mabao yalifungwa na mshambuliaji Gaudence Mwaikimba na Abdalah Seif Karihe huku Mtibwa wakiwafunga Kagera Sugar kwa 1-0 , Mgambo Jkt waliendeleza mwanzo mbaya wa Ashanti United kwa kuwafunga 1-0 huku Mbeya City wakitumia vyema uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine baada ya kushinda mchezo dhidi ya JKT Ruvu kwa 2-1.
Msimamo wa ligi kuu unaonyesha kuwa timu zote nne zinazotarajiwa kuwania ubingwa msimu huu za Simba , Yanga , Azam na Coastal Union zinalingana kwa pointi zote zikiwa zimejikusanyia pointi nne baada ya michezo miwili zikiwa zimepata matokeo ya ushindi na sare kwa mmoja huku Yanga wakiwa juu ya wenzao kwa tofauti ya mabao kufuatia ushindi mkubwa wa 5-1 walioupata jumamosi ya wiki iliyopita mbele ya Ashanti United huku Coastal Union na Azam zikifuatia kwa tofauti ya mabao zikiwa zimelingana baada ya kushinda 2-0 na kutoka sare ya 1-1 na Simba wanashika nafasi ya nne baada ya sare ya 2-2 na ushindi wa 1-0 .
Matokeo ya Vodacom Premier League kwa mechi za Jumatano Tar 28/08/2013.
Yanga 1-1 Coastal Union.
Jkt Oljoro 0 -1 Simba .
Mgambo Jkt 1-0 Ashanti United.
Rhino Rangers 0-2 Azam Fc.
Kagera Sugar 0-1 Mtibwa Sugar.
Mbeya City 2-1 Jkt Ruvu.