HAYA NDIO MAJIBU YA DKT. KITILA MKUMBO NA ZITTO KABWE BAADA YA KUONDOLEWA KATIKA UONGOZI NDANI YA CHADEMA
1. Katika kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika tarehe 20-22 Novemba 2013, pamoja na mambo mengine, kulijadiliwa waraka wa s...
Waraka huu ulilenga kujenga hoja ya kufanya mabadiliko ya uongozi na kuanisha mikakati ya ushindi kwa mgombea mlengwa katika uchaguzi mkuu ndani ya CHADEMA.
2. Katika mjadala, maudhui ya waraka huu yalionekana kwa wajumbe kwamba yalikuwa na mapungufu na yalikiuka misingi na kanuni zilizoanishwa katika Katiba ya Chama.
3. Kufuatia mkutano wa waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013 ambapo, pamoja na mambo mengine, ilielezwa na viongozi wa CHADEMA kwamba mimi na wenzangu (Samson Mwigamba na Zitto Kabwe) tumehujumu chama na tumefanya uhaini kwa kuandaa mkakati wa ushindi kwa mgombea tunayemtaka, ningependa nieleza mambo yafuatayo:
a. Siamini hata kidogo kwamba kugombea nafasi yeyote iliyo wazi ndani ya chama cha siasa ni uhaini na hujuma. Msingi namba moja wa CHADEMA ni demokrasia na hakuna namna ya kudhihirisha mapenzi kwa demokrasia zaidi ya kuruhusu ushindani katika nafasi za uongozi na hasa uongozi wa juu kabisa. Hiki kinachoitwa uhaini ni wasiwasi wa siasa za ushindani katika chama chetu.
b. Sijawahi na sitarajii kushiriki vitendo vyovyote vya kuhujumu chama changu cha CHADEMA na harakati za mabadiliko hapa nchini.
c. Nasikitika kwamba nimesababisha usumbufu kwa viongozi wangu wa CHADEMA kutokana na dhamira yangu ya kutaka mabadiliko ya uongozi ndani ya chama chetu kwa njia halali za kidemokrasia.
d. Tunaweza kujifunza kutokana na historia. Siasa za ushindani ndani ya vyama katika nchi hii sio kitu kigeni. Enzi za TAA na kabla TANU haijazaliwa wanachama walikuwa wanagawana nafasi za uongozi mezani.
e. Zitto Zuberi Kabwe hajafukuzwa kwa sababu ya waraka huu kwa sababu yeye hakuhusika kwa namna yoyote kuuandaa, ingawa alikuwa ni mlengwa mkuu. Yeye amefukuzwa kwa sababu ambazo yeye atazieleza na ambazo viongozi wa CHADEMA hawakuzieleza katika mkutano na waandishi wa habari.
f. Napenda ijulikane kwamba sikuomba kujiuzulu kwa sababu ya kuogopa aibu ya kufukuzwa. Niliomba kujiuzulu kwa sababu nilitambua kwamba wenzangu katika Kamati Kuu walikuwa hawana imani nami tena, na ni uungwana kujiuzulu mkifika mahala hamuaminiani. Nilitambua vilevile kwamba, kwa mujibu wa Katiba yetu, Kamati Kuu ilikuwa haina uwezo wa kunivua nafasi yangu moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA, Sura ya Sita, Ibara ya 6.3.6 (b), inasomeka hivi “Kiongozi aliyeteuliwa na vikao vya uongozi ataweza kusimamishwa au kuachishwa uongozi na kikao kilichomteua”.
4. Hiki kilichotokea ndani ya chama sio kitu kibaya. Vyama vingi imara hupitia katika migogoro na misukosuko kama hii na zaidi. Naamini tutavuka na tutakuwa imara zaidi. Muhimu ni kwamba ni lazima tuaminiane. Katika kuaminiana sio lazima tufanane kimawazo na kimtazamo kwa sababu hili ni jambo lisilowezekana kibinadamu na zaidi katika siasa.
5. Ninapohitimisha, ninawasihi wanachama wa CHADEMA na wapenzi wa mabadiliko popote walipo wapiganie kwa dhati MISINGI mama ya CHADEMA ikiwemo demokrasia ndani ya chama. Hakuna namna ambavyo chama chochote kinaweza kushawishi umma kwamba kitapigania demokrasia katika nchi wakati kinayahainisha mapambano ya kidemokrasia ndani ya chama chenyewe.
Kukataa siasa za ushindani ndani ya chama ni kuhujumu demokrasia na ni usaliti kwa misingi mama ya chama ambayo ni uhuru wa kweli na mabadiliko ya kweli.
6. Nitafuata taratibu zote za chama kama zilivyoelekezwa na Kamati Kuu na kwa mujibu wa katiba yetu, na nitashiriki kikamilifu katika kutuliza hali ya kisiasa ndani ya chama ili kuhakikisha kwamba tunabaki imara, na CHADEMA inaendelea kuwa tumaini la watanzania.
Mungu ibariki Tanzania.
Dkt. Kitila Mkumbo
Dar es Salaam
Jumapili, 24 Novemba 2013.