JUKWAA LA KATIBA KUONGOZA UTEUZI WA WAJUMBE WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA
Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata) limesema litaongoza mkutano wa kuchagua majina ya watu 20 kutoka katika taasisi zisizo za kiserikal...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/12/jukwaa-la-katiba-kuongoza-uteuzi-wa.html
Jukwaa
la Katiba Tanzania (Jukata) limesema litaongoza mkutano wa kuchagua
majina ya watu 20 kutoka katika taasisi zisizo za kiserikali katika
makundi yaliyoainishwa kisheria, yatakayopelekwa kwa Rais ili ateue kuwa
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Mkutano huo utafanyika mkoani Dodoma, Jumatano ijayo.
Hatua
hiyo inafuatia taaarifa ya Ikulu wiki iliyopita iliyozitaka taasisi
hizo kuwasilisha majina ya watu wanaowapendekeza awateue kuwa wajumbe wa
Bunge hilo.
Kaimu
Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda, alisema jana kuwa mkutano huo
utahudhuriwa na wajumbe 200 kutoka katika mikoa na wilaya zote za
Tanzania Bara na Zanzibar.
Wajumbe
hao wameteuliwa kutoka katika makundi ya taasisi zisizo za kiserikali,
kidini, elimu ya juu, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, vyama
vya wafanyakazi, vyama vya wakulima na vyama vinavyowakilisha wavuvi na
wafugaji.
Alisema katika kuwapata wajumbe 20 wa Bunge hilo, vigezo vya uwakilishi wa kikanda na kisekta vimetumika.
Mwakagenda
alisema uwakilishi wa wajumbe kijiografia ni kutoka katika mikoa ya
Kanda ya Ziwa, Kusini, Magharibi, Kaskazini, Kati, Pwani, Nyanda za Juu
Kusini, Unguja pamoja na Pemba.
Alisema kwa upande wa uwakilishi wa kisekta, ni katika maeneo yanayogusa jamii moja kwa moja.
Kwa
mujibu wa Mwakagenda, pia kutakuwapo wajumbe watakaowakilisha uchumi na
maendeleo ya jamii, wazee na vijana, jinsia na wanawake, sheria na haki
za binadamu, uwajibikaji na utawala bora.
Pia
kutakuwapo uwakilishi katika haki za watoto, vyombo vya habari, ardhi,
maliasili, elimu, afya, na na kwa watu wenye Virusi vya Ukimwi (VVU) na
Ukimwi pamoja na dawa ya kulevya.
“Tukishachagua
majina 20 ya ‘wajumbe’ hao tutamwandikia barua Rais ili ateue wajumbe
tisa kutoka kwenye uwakilishi wa kijiografia yaani kikanda na 11
kuwakilisha sekta mbalimbali,” alisema Mwakagenda.
Alisema
kutokana na mchakato wa kuwapata wajumbe na kuchelewa kuanza kwa Bunge
hilo, itakuwa ni miujiza kupatikana kwa katiba mpya ifikapo Aprili 26,
mwakani.
Mwakagenda
alisema katika masuala ya kidemokrasia na sheria ni lazima yawepo
makubaliano ya pamoja na kupendekekeza uitishwe mjadala wa kitaifa kabla
wananchi hawajapiga kura ya maoni, kwani bila kufanya marekebisho hayo
katiba ikikataliwa itakuwa ni hasara kwa Taifa kutokana na gharama kubwa
zilizotumika kuendesha mchakato huo.
Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa mwisho wa kupeleka majina ya wajumbe hao ni Januari 2, mwakani.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013, Bunge Maalumu la Katiba litakuwa na jumla ya wajumbe 635.
Kati
ya wajumbe hao, wanaotoka katika mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na
taasisi za kidini ni 201, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni
358 na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ni 76.
Kwa
mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, kati ya wajumbe
201 kutoka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini, nusu
watakuwa wanawake na nusu nyingine watakuwa wanaume.
Waziri Chikawe aliliambia Bunge katika Mkutano wake wa 13 kuwa kati ya wateuliwa 201, wanawake watakuwa 101 na wanaume 100.
Bunge
Maalumu la Katiba, ambalo litafanyika kwa siku zisizozidi 70,
linatarajiwa kuanza rasmi Februari, mwakani, kwa ajili ya kujadili na
kuipitisha rasimu ya pili ya katiba iliyopendekezwa.
Rasimu
ya pili ya katiba itakabidhiwa kwa Rais na baadaye itachapishwa katika
Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine ndani ya siku 31.
Katika kipindi hicho, Rais ataitisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kwa ajili ya kupitisha rasimu iliyopendekezwa.
Tume
itakabidhi rasimu ya pili ya katiba kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein, Desemba 30, mwaka huu.
Rasimu
hiyo ya pili inatolewa ikiwa imepita miezi saba tangu tume hiyo
ilipotoa rasimu ya kwanza ya ambayo ilijadiliwa katika Mabaraza ya
Katiba yaliyokaa kuanzia Julai 12 mpaka Septemba 2 mwaka huu.
Rasimu ya kwanza ilizinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Juni 4, mwaka huu.
Baada
ya rasimu ya pili kupitishwa na Bunge Maalumu la Katiba, itaitishwa
kura ya maoni, ambayo itatoa fursa kwa wananchi kuamua ama kuikubali au
kuikataa.
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji
Joseph Warioba, yenye wajumbe 30; wakiwamo 15 kutoka Tanzania Bara na 15
kutoka Zanzibar, ilitangazwa na Rais Jakaya Kikwete, Aprili 6 na
kuapishwa Aprili 13, mwaka jana.
Ilianza
rasmi kazi ya kukusanya maoni ya wananchi Mei mosi, mwaka jana. Baada
ya kukamilisha kazi hiyo, iliyachambua na kuandika Rasimu ya Katiba.
Kazi
ya kukusanya maoni hayo iliwahusisha wananchi mmoja mmoja kupitia
mikutano ya hadhara na ilikamilishwa na Tume Desemba, mwaka jana.
Baadaye
Tume ilikutana na makundi maalumu na watu mashuhuri, wakiwamo viongozi
wakuu wastaafu na waliopo madarakani Januari 7-28, mwaka huu.
Baadaye,
mabaraza ya katiba yaliipitia Rasimu ya Katiba kuanzia Julai 12 hadi
Septemba 2, mwaka huu na kutoa mapendekezo yake, ambayo yaliwasilishwa
kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume
inaendelea kuyachambua kabla ya kukabidhi rasimu ya pili ya katiba kwa
Rais Kikwete na Rais Dk. Shein mwishoni mwa mwezi huu.