MAKAMBA AJIPIGIA DEBE LA URAIS KIAINA
Naibu waziri wa Sayansi na Teknologia , January Makamba Katika kile kinachoonekana kama kujipigia debe katika kinyang’anyiro cha urai...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2013/12/makamba-ajipigia-debe-la-urais-kiaina.html
Naibu waziri wa Sayansi na Teknologia , January Makamba |
Katika kile kinachoonekana kama kujipigia debe katika
kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amewaambia viongozi
wa dini Kanda ya Ziwa kwamba vijana wanapofika kuomba ridhaa yao,
muwaangalie, msiwabeze.
Huku akikataa kuweka bayana nia yake ya kuwania
urais kwa maelezo kwamba muda wa kufanya hivyo haujawadia, Makamba
aliwaambia viongozi hao wa dini kwamba wagombea hao wanapopita wawasomee
sifa za uongozi katika Biblia na kusema kumekuwapo mjadala wa sifa za
uongozi kuhusu kijana na kusema amekuwa akitoa mwito kwa vijana
wasiokuwa na makandokando kushiriki na kujitokeza katika kusaidia nchi
ipone.
Akizungumza juzi usiku mjini hapa katika chakula
cha pamoja na maaskofu na wachungaji kutoka Umoja wa Makanisa ya
Kikristo wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Makamba ambaye pia ni mbunge wa
Bumbuli (CCM), alisema: “Huu ni wakati wa kila mmoja kutafakari hatima
ya nchi yetu. Ndugu zangu… nadhani tuzungumze machache yanayohusu nchi
yetu na Taifa letu, kwa sababu sote ni Watanzania na wote tuna hamu ya
kujua na kutafakari mustakabali wa nchi yetu, umoja wetu, amani yetu na
utulivu wetu.”
Alisema vijana wengi wamekuwa waoga kwa madai
kwamba hawana fedha, uzoefu lakini akasema maaskofu na wachungaji
wanapaswa kuwa mashahidi kupitia vitabu kwani katika Yeremia imeelezwa
jinsi Mungu alivyompatia unabii Yeremia ambaye alidai yeye bado mdogo.
“Yeremia alipopewa unabii alilalamika mimi mdogo
mimi siwezi, lakini Mungu alimwambiaje, ngoja nisome, (Yeremia 1: 4-10)
…. Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako nilikujua, kabla
hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalumu, nilikuweka uwe nabii kwa
mataifa,” alisema na kuongeza:
“Bwana alimwambia usiseme, mimi ni mtoto mdogo.
Utakwenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza,
usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe.”
Alisema Tanzania inapita katika kipindi kigumu,
hivyo viongozi wa dini wanapaswa kuongoza maombi yatakayoiwezesha kupata
kiongozi mwenye sifa ya kuivusha katika kipindi hicho.
Makamba amesema nchi inakabiliwa na nyufa kama
vile rushwa, udini, ukabila, Uzanzibari na Uzanzibara, huku akirejea
hotuba ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya Machi 1995,
ambayo aliyataja mambo hayo kuwa nyufa zinazoweza kuliangamiza taifa.
Alisema Tanzania inahitaji uponyaji na ikibidi
kuanza upya kwa maana ya aina ya uongozi unaohitajika hivi sasa na
kwamba ili kutimiza lengo hilo, viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya
kutafakari na kuielekeza nchi njia sahihi ya kufuata.
“Shughuli za siasa zimeingiliwa na matapeli,
lakini hata shughuli yenu pia imeingiliwa na matapeli. Sasa tunapotafuta
uponywaji wa nchi yetu ninyi mna nafasi kubwa kwani uponyaji
tunaouzungumzia ni wa maovu ya kiroho, uongo, ubakaji na vitu kama
hivyo, ninyi mna nafasi kubwa sana,” alisema.
Alisema viongozi wa kisiasa pia wanayo nafasi yao katika kuponya taifa lakini lazima wanapofanya kazi hiyo wawe wasafi.
Alisema askofu au mchungaji akihubiri anapaswa
kuwa msafi na hata katika uongozi wa siasa anaposimama mtu na kusema
yeye ni jawabu la matatizo ya wananchi ni vizuri kumtazama sura yake
kama ameacha (maovu).
“Tunapoomba uongozi wa kisiasa zipo sifa kwani tunaomba kuongoza
watu wa Mungu ambao ni walewale wanaokuja kanisani ndiyo wanaokuja
katika siasa, kuongoza watu wa Mungu siyo kitu kidogo…… hivyo lazima
vigezo vya kuongoza watu hawa viwe vikubwa sana,” alisema
Rasilimali za nchi
Alisema Tanzania hivi sasa inakabiliwa na
changamoto zinazoweza kuitwa kuwa ni za kidunia na za kibinadamu
zinazojumuisha masuala kama vile upatikanaji wa huduma za afya, maji na
elimu.
“Tunagawanyika ingawa migawanyiko hiyo si ya
kidini, rangi na kikabila... iko ya namna gani, watu wachache
wananufaika na keki (rasilimali) ya taifa kuliko wengine,” alisema
Makamba na kuongeza:
“Sasa Serikali, hili kwetu ni muhimu sana…. hakuna
kitu muhimu kama kuendelea kujenga umoja wa taifa letu, migawanyiko hii
ndiyo changamoto. Elimu anayoipata mtoto wangu ndiyo anaipata mtoto wa
Rwamgasa, Kwimba na Nyarugusu?”
Alisema usawa katika elimu pamoja na huduma
nyingine kama afya na nyingine muhimu, ndiyo msingi wa ujenzi wa taifa
lenye amani na umoja kwani kila mmoja atajihisi kunufaika na rasilimali
za nchi.
Naibu Waziri huyo alisema changamoto nyingine
zinazoikabili nchi ni vitendo vya rushwa, ubadhirifu na wizi wa mali ya
umma, ubakaji, utapeli na kuporomoka kwa maadili.
Alisema taifa halipaswi kusubiri adhabu kutoka kwa
Mungu kama inavyosomeka katika vitabu vitakatifu ambako kuna ushahidi
kuhusu gharika wakati wa Nuhu, pia moto wakati wa Sodoma na Gomora, huku
akiwapa changamoto viongozi wa dini kukabiliana uovu unaoshika kasi.
“Sasa taifa letu lina miaka 52 ya Uhuru wa
Tanganyika na mwakani tunaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Zanzibar. Miaka
50 ni mingi kwa binadamu, lakini ukweli ni kwamba kazi ya kulijenga
taifa letu ndiyo inaanza.”
Shinikizo la maaskofu
Baada ya hotuba yake, baadhi ya maaskofu na
wachungaji walisikika wakimshinikiza Makamba atangaze nia ya kugombea
urais lakini alisema atafanya hivyo wakati mwafaka ukiwadia.
Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa hayo ya Kikristo,
Askofu Charles Sekelwa alisema: “Viongozi wa dini tukubaliane kuwa
walezi na tusimkatae mtu kwa dini yake wala kabila lake. Wakijitokeza
vijana huko mbele tuwaunge mkono, hayo maneno ni ya mtu mwenye hekima”.
Askofu Jacob Lutabija alisema amepokea ujumbe mzito ambao atakwenda kuutangaza kwa waumini wake wa Musoma akisema kwa watu wenye hekima zao wametambua nini wanapaswa kufan
MWANANCHI.
Askofu Jacob Lutabija alisema amepokea ujumbe mzito ambao atakwenda kuutangaza kwa waumini wake wa Musoma akisema kwa watu wenye hekima zao wametambua nini wanapaswa kufan
MWANANCHI.