MENO YA TEMBO 81 YAKAMATWA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Watu wawili wanashikiliwa na polisi nchini Tanzania baada ya kukamatwa na shehena ya meno ya tembo katika bandari ya Dar es Salaam,...



Watu wawili wanashikiliwa na polisi nchini Tanzania baada ya kukamatwa na shehena ya meno ya tembo katika bandari ya Dar es Salaam, waliyokuwa wakisafirisha kiharamu maafisa wa nchi hiyo wamesema.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa Tanzania, Chikambi Rumisha amesema meno hayo yapatayo 81 yana uzito wa kilo 303.

Kwa mujibu wa maafisa wa Wizara meno hayo ya tembo ni mapya ikiwa na maana yametokana na tembo 41 waliouawa ndani ya mwezi mmoja uliopita.

Naibu Waziri wa Maliasiali na Utalii wa Tanzania Lazaro Nyalandu amesema mauaji ya tembo yameongezeka nchini humo baada ya operesheni ya kupambana na majangili iliyopewa jina la "Operesheni Tokomeza" kusimamishwa kutokana na baadhi ya watendaji kukiuka haki za binadamu.
Mapema wiki hii Naibu Waziri huyo amesema tembo wapatao 60 wameuawa kati ya mwezi Novemba na Decemba ikilingalishwa na tembo wawili waliouawa mwezi Octoba.
Soma taarifa iliyotelewa na mamlaka ya bandari hapo chini.


TAARIFA KWA UMMA

Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na vyombo vingine vya Dola, tarehe 2 Januari 2014 majira ya saa tatu asubuhi kwenye Bandari ya Dar es Salaam, imekamata meno 81 ya tembo yenye uzito wa kilo 303 sawa na tembo 41. Aidha, magamba 120 ya kakakuona na mazao ya bahari nayo yamekamtwa. Hii ni baada ya Askari wa Bandari kutilia shaka mizigo iliyokuwa kwenye gari ikiingizwa bandarini. Meno ya tembo yaliyokamatwa bado ni mapya ikiwa na maana tembo hao wameuawa katika kipindi kizichozidi mwezi mmoja uliopita.

Wizara inasikitishwa sana na vitendo hivi viovu vya ujangili ambavyo vimetokea ndani ya muda mfupi. Tayari watuhumiwa wawili wanashikiliwa na Polisi kufuatia tukio hilo. Majina yao yanahifadhiwa kwa lengo la kutovuruga upelelezi.

Serikali inasisitiza tena kwamba imejizatiti kupambana na vitendo vya ujangili katika mapori yote na maeneo yote ya mipaka ya nchi yetu. Pia, Serikali inapanua wigo wa upelelezi kuhakikisha wote waliohusika wanapatikana na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Imetolewa na:

Chikambi K. Rumisha
Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii
Januari 2, 2014

Related

OTHER NEWS 8037757644056604015

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item