UKAWA WATISHIA KUANDAMANA NCHI NZIMA

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umemtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha mara moja shughuli za Bunge Maalum la Katiba ili lisiende...


Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umemtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha mara moja shughuli za Bunge Maalum la Katiba ili lisiendelee kufuja mali za Watanzania na kupuuza maoni ya wananchi yaliyomo katika rasimu ya Katiba mpya.

Viongozi wa umoja huo wameonya kuwa, endapo Rais Kikwete hataitikia wito huo, Ukawa utawaongoza wananchi kupaza sauti zao kwa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima kupinga najisi inayotiwa kwenye maoni yao.

Aidha, viongozi hao wamemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalum kwenye matumizi ya fedha za Bunge hilo kwani Tangu Bunge la Bajeti lililopita walibainisha kuwapo kwa ufisadi.

Tamko hilo la Ukawa lilitolewa na viongozi wa umoja huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, wakati wakizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.

Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Mbatia alisema endapo Rais Kikwete atashindwa kusitisha Bunge hilo, umoja huo utawaongoza wananchi kufanya maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima kupinga kuchakachuliwa maoni yao kwenye Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa katika Bunge hilo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

“Tunamtaka Rais Kikwete asitishe shughuli za Bunge Maalum la Katiba mara moja lisiendelee kuvuruga na kuharibu mchakato wa Katiba na kuiweka nchi katika sintofahamu juu ya jambo hili nyeti, tunamtaka alisitishe ili lisiendelee kufuja fedha za Watanzania maskini wanaopigania Katiba hiyo iwape matumaini ya kuongozwa na kujitawala wanavyotaka,” alisema na kuongeza:

“Iwapo Rais atashindwa kutumia mamlaka yake kusitisha Bunge hilo na hivyo likaendelea kinyume cha matakwa na maslahi ya wananchi kama lilivyofanya awali na linavyofanya sasa, Ukawa tutaongoza Watanzania kupaza sauti zaidi kupinga najisi inayotiwa kwenye maoni yao kupitia maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima.”

Mbatia alisema unajisi huo wa maoni ya wananchi unafanywa pasipo kujali kilio cha wananchi kinachopazwa kutoka kila kona ya nchi kutaka maoni yao yazingatiwe kwa kujadiliwa, kuboreshwa na kisha kupitishwa na Bunge hilo kabla ya wao kupigia kura.

Alisema wabunge wanaotoka Chama Cha Mapinduzi(CCM) pamoja na makada wengine wapatao 166 wa chama hicho waliteuliwa kuingia kwenye Bunge hilo kusimamia maslahi ya CCM kupitia kundi la 201.

“Wameamua bila aibu mbele ya umma si tu kupuuza rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi, bali hata kuingiza mambo yao waliyodhamiria  tangu mwanzo kwa kadri ya maamuzi na maelekezo ya vikao vya chama hicho,” alisema Mbatia na kuongeza:

“Bila kujali wala kuguswa na miito ya Watanzania mbalimbali wanaotaka jambo hilo liongozwe na maridhiano kwa ajili ya mwafaka wa kitaifa badala ya kuweka matamanio ya watawala mbele, CCM na mawakala wao katika mchakato huu wameendelea pia kufuja fedha na kutumia vibaya fedha za wananchi kwa kujadili na kuingiza vitu visivyokuwamo au visivyotakiwa kuwa sehemu ya rasimu hiyo.”

Mbatia alisema hali hiyo imefanyika kwa namna kadhaa ikiwa ni pamoja na kutofuata sheria inayosimamia mchakato mzima, kubadili kanuni za uendeshaji wa Bunge hilo hasa katika taratibu za kujadili na kupitisha ibara ikiwamo kuingiza masuala ya Tanganyika kwenye Rasimu ya Katiba ya Muungano.

“Kimsingi masuala wanayoyajadili  na kuchomeka kinyemela kwenye rasimu hiyo ya pili, hususani ya ardhi, elimu, maji, kilimo, uvuvi, mifugo, serikali za mitaa na mengine yanapaswa kuandikwa kwa kina ndani ya Katiba ya Tanganyika na siyo Jamhuri ya Muungano” alisema.

Alisema ni vema kukumbuka kuwa hata Zanzibar nao walijadili wenyewe mambo yao ya ndani na kutengeneza Katiba yao, na kwamba katika hilo hawaoni mantiki ya kuruhusu wajumbe toka Zanzibar kujadili na kuamua mambo ya Tanganyika, huku akisema Bunge hilo halina sifa ya kujadili yasiyo ya Muungano.

Aidha, akijibu maswali ya waandishi wa habari, Mwenyekiti mwingine Mwenza wa Ukawa, Mbowe, alisema ni jambo la kushangaza kuona mchakato huo nyeti unaendeshwa pasipo na kuwapo kwa mwongozo kutoka kwa watu walioko madarakani ambao walitarajiwa wangetumia mamlaka yao na dhamana ya uongozi ili kulipitisha taifa salama wakati huu mgumu na kupatikana Katiba mpya.

Mbowe alisema nchi inaongozwa kama ndege isiyo na rubani ambayo haina mwelekeo maalum ambayo  inaweza kuanguka mahali popote.
Alisema kwa namna mchakato huo unavyopelekwa, mtu yeyote makini anaweza kubaini kuwa ni matokeo ya kukosekana kwa uongozi wa kisiasa kwa chama kinachoongoza serikali.

“Vipo viashiria vingi vinavyoweka wazi kuwapo kwa ombwe  kubwa la uongozi kisiasa katika mchakato huu, ikiwa ni pamoja na kauli kinzani za viongozi wa serikali na CCM wenyewe, wakati Waziri Mkuu Pinda akizungumza kama vile kunahitajika mazungumzo zaidi na kwamba suala la muundo wa serikali lilipaswa kupigiwa kura kabla, lakini Mwenyekiti wa Bunge hilo naye anaendelea kuongoza Bunge kama vile ni mali binafsi,” alisema na kuongeza:

“Wakati baadhi ya viongozi wa serikali wakitoa kauli za kuhitaji kuwa makini na taratibu za kuendesha mchakato huo, CCM nayo inatoa kauli za kuzidi kuharamisha na kutia najisi mchakato mzima, mchakato unakwama, nchi inayumba, Watanzania wako katika sintofahamu kwa sababu tu tumekosa uongozi wa kisiasa katika jambo hili.”  alisema Mbowe.

Kuhusiana na baadhi ya wajumbe wa Ukawa kuhudhuria vikao hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi(CUF), Prof. Lipumba, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Umoja huo, alisema mpaka sasa wajumbe wa Ukawa  wameonyesha msimamo wa kusimamia upande wa wananchi kwa kuwa zaidi ya asilimia 95 wote wako nje ya Bunge hilo.

Alisema  wanapongeza wajumbe hao kuwa na msimamo mmoja wa kutetea maslahi ya wananchi kwa kutohudhuria vikao vya Bunge hilo ambavyo maoni ya wananchi yamekiukwa.

Kadhalika,  Mbowe akifafanua kuhusu baadhi ya wajumbe wanaotoka chama chake kuhudhuria vikao hivyo, ambapo alisema ni mjumbe mmoja tu anayemtambua kushiriki katika Bunge hilo na kwamba wengine wawili walienda kusaini posho.

Hata hivyo, alisema kamati ya maadili ya chama hicho itawachukulia hatua wajumbe hao.

Katika suala la taarifa za Mbowe kukutana katika kikao cha siri na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulhaman Kinana, zilizotolewa kwenye vyombo vya habari hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa alisema kikao hicho hakikua cha siri.

Alisema kikao hicho hakikuwa cha viongozi hao wawili, bali kiliandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania(TCD)  na kushirikisha viongozi wakuu wa vyama vilivyo na wawakilishi bungeni.

Alisema kikao hicho kilifanyika Agosti 2, mwaka huu na kati ya mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi, kufanya marekebisho ya daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na suala la kuwapo kwa maridhiano juu ya mchakato wa Katiba.

Jingine alilotaja kuzungumzwa katika kikao hicho ni endapo Katiba itashindikana kupatikana kwa sasa,  nini, suala la mgombea binafsi, na suala la mgombea wa Urais kupata kura asilimia 50+1.

Dk. Slaa alisema katika mkutano huo walikuwa wanazungumza mambo ya kawaida na kwamba walikubaliana  mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho yatakuwa ni siri, lakini kinachotokea hivi sasa baadhi ya viongozi wa CCM wameamua kuanza kuyaweka wazi taratibu.

Alisema licha ya wao kukubali kuendelea kufanya mazungumzo hayo ya maridhiano lakini wenzao wamekuwa wakikiuka masharti ya mazungumzo hayo na kwamba endapo hali hiyo itaendelea uvumilivu utawashinda.

Bunge hilo lililoanza Februari 18, mwaka huu kwa awamu ya kwanza, lilitumia takriban siku 21 za mwanzo kujadili na kupitisha kanuni za kuliongoza, ikiwamo kuunda kamati 16, kati ya hizo, 12 za kujadili sura za Rasimu ya Katiba. Kamati hizo zilijichimbia katika kumbi mbalimbali mjini Dodoma na kujadili sura ya kwanza na ya sita, huku mjadala mzito uliosababisha Bunge kuingia kwenye mvutano mkubwa ni sura ya sita inayozungumzia muundo wa Muungano.

Kundi la wajumbe wengi, wakiongozwa na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatetea muundo wa sasa wa serikali mbili uendelee kwa maelezo kuwa ndiyo utakaodumisha Muungano.

Kundi la Ukawa linaloundwa na vyama vya upinzani, vikiwamo Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na baadhi ya vyama vidogo lilisimamia serikali tatu kwa hoja kwamba, rasimu ilipendekeza serikali tatu kutokana na maoni ya wananchi.

Aidha, baada ya kamati hizo kumaliza kazi na kurudi kama Bunge Maalumu, wenyeviti wa kamati hizo waliwasilisha taarifa ya wengi, huku wengine wakiwasilisha ya wachache.

Hata hivyo, mjadala huo ulijikita katika kurushiana vijembe, maneno yasiyo na staha, matusi, kudhihaki waasisi, kumshambulia Jaji Warioba kwamba alichakachua takwimu na kupendekeza serikali tatu kwa maslahi yake binafsi.

Hata hivyo, wakati mjadala wa sura hizo ukiwa katikati, kundi la wajumbe wanaounda Ukawa walitoka nje ya ukumbi Aprili 16, mwaka huu, kususia mchakato huo kwa madai kwamba, CCM imeliteka Bunge na mjadala huo kutokana na kufuta mapendekezo ya tume ya sura hizo mbili na kupenyeza rasimu yake.

Hadi Bunge hilo linaahirishwa, ngwe yake ya kwanza Aprili 25, mwaka huu, wajumbe wa Ukawa walikuwa nje ya Bunge kwa takriban siku tisa, huku wakianza kuzunguka maeneo kadhaa ya nchi kuwaeleza wananchi juu ya mwenendo wa Bunge kupitia mikutano ya hadhara.

Bunge hilo liliahirishwa kupisha Bunge la Bajeti, Mei, mwaka huu na kuendelea tena Agosti 5, mwaka huu kwa siku 60 zilizoongezwa na Rais Kikwete pasipo kundi hilo la Ukawa.

Aidha, mara baada ya mchakato wa kuunda Katiba mpya ya Tanzania, kuingia hatua ya Bunge Maalum liloloundwa chini ya kifungu cha 22 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Watanzania na dunia kwa ujumla imeshuhudia mambo mengi ambayo ni vyema yakarejewa.

Mojawapo ilikuwa ni  kubadili mtiririko wa matumizi ya kanuni, uliyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, kuhutubia Bunge Maalum kabla Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ni moja ya mambo yaliyoibua malalamiko kabla na baada ya kutokea.

Baada ya Rais Kikwete kuhutubia, yakaibuka malalamiko hasa kutoka upande wa kundi linalounga mkono maudhui yaliyo ndani ya Rasimu ya Pili ya Katiba, iliyotokana na maoni ya wananchi kwa uratibu wa Tume ya Warioba.

Walio wengi wanaona kuchachamaa kwa Ukawa hakuna mantiki kwa sababu ni haki na wajibu wa Rais kutoa maangalizo, hasa katika tukio zito la kitaifa kama hilo.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Rais Kikwete, akihutubia Taifa kupitia vyombo vya habari alikaririwa akizungumzia hotuba yake aliyoitoa wakati akizindua Bunge Maalum Hii ni mara ya kwanza kuzungumzia suala la mchakato wa Katiba, tangu alipolizindua na kuacha gumzo ndani na nje ya Bunge hilo.

Rais Kikwete, alieleza kazi tatu anazopewa na Sheria husika, kuzifanya baada ya Tume kumaliza kazi zake kuwa ni kupokea Rasimu na Ripoti, kusaini tangazo la gazeti la serikali na kuitisha Bunge Maalum.
SOURCE: NIPASHE

Related

OTHER NEWS 1979502756781929599

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item