WAHAMASISHAJI JAMII KUONGEZA NGUVU YA KAMPENI MPYA YA UZAZI WA MPANGO KIGOMA

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la World Lung Foundation Dk.Nguke Mwakatundu (katikati) akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari,wag...

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la World Lung Foundation Dk.Nguke Mwakatundu (katikati) akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari,waganga wakuu wa wilaya mkoani Kigoma na wahamasishaji jamii kuhusu uzazi wa mpango ikiwa ni sehemu ya  kampeni ya uzazi wa mpango ijulikanayo thamini uhai Jitofautishe.


*Wahamsishaji jamii waliofuzwa watafanya kazi na kampeni ya Thamini Uhai kuhamasisha faida za uzazi wa mpango*
Mkutano na waandishi wa habari mkoani Kigoma umeainisha nafasi muhimu ya wahamasishaji jamii katika kuelimisha wananchi kutumia uzazi wa mpango.
Wahudhuriaji wa mkutano huu uliyoandaliwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma na World Lung Foundation, walipata kusikia ni jinsi gani wahamasishaji jamii 20 waliopewa mafunzo maalum wanaongeza ufahamu wa jamii kuhusu faida za muda mrefu za uzazi wa mpango katika jamii husika.
Kampeni hii inayotumia njia mbalimbali ya mawasiliano imeandaliwa na kusimamiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikishirikiana na Engender Health na World Lung Foundation (WLF) chini ya nembo ya “Thamini Uhai”.
Wahamasishaji jamii hawa watacheza nafasi muhimu kupunguza mahitaji makubwa ya jamii kuhusu uzazi wa mpango kwa kuunganisha watumiaji watarajiwa na huduma hizi katika vituo vya afya husika.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kampeni, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dr Leonard Subi alisema, “Wahamasishaji jamii ni sehemu muhimu ya kampeni za afya kama Thamini Uhai.
Wanawaunganisha wateja wanaohitaji huduma muhimu kama vile uzazi wa mpango, na wafanyakazi wa vituo vya afya wanaotoa huduma hizi.
Bila shaka, mafanikio ya kampeni hii yatategemea pia ubora wa huduma zitolewazo katika vituo vya afya.
Hivyo, kampeni hii inawahusisha pia watoaji wa huduma wa afya na pia tutaandaa mikutano katika vituo na katika jamii ili kuzingatia huduma bora na mahitaji ya jamii.” Kampeni hii mpya iliyozinduliwa Mei 25 inajumuisha matangazo ya redio, mchezo wa kuigiza wa radio, mtandao wa kijamii, mabango na majarida pamoja na uhamasishaji jamii.
Kampeni imewalenga wanaume na wanawake wenye umri wa kuzaa. Ujumbe wa kampeni utaonyesha manufaa ya kupanga uzazi au kupunguza idadi ya mimba, kwa mfano elimu bora na ongezeko la ajira kwa wanawake, afya bora zaidi kwa mama na mtoto, matumizi mazuri zaidi ya rasilimali katika familia na jamii iliyo imara zaidi.


Dr. Nguke Mwakatundu, Mkurugenzi wa Taifa – Tanzania, World Lung Foundation, alisema: “Wahamasishaji katika sekta ya afya, serikali na taasisi za dini nchini kwa pamoja wamekubali kuwa uzazi wa mpango ni jambo jema kwa familia na taifa.

Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma, Dk.Leonald Subi (kushoto) akitoa tathmini ya hali ya uzazi wa mpango mkoani Kigoma  katika kikao cha pamoja cha waandishi wa habari, waganga wakuu wa wilaya na wahamasishaji wa kampeni za uzazi wa mpango ijulkanayo kama Thamini uhai Jitofautishe.
 Ukosefu wa mpango wa uzazi, ikiwemo kuacha nafasi kati ya mimba moja na nyingine, inachangia kuongeza vifo vya akina mama na watoto wachanga nchini.
Ukosefu huu pia hupunguza uwezo wa wanawake na familia zao kufanya maamuzi  yatakayolinda afya zao, uchumi wao na ubora wa maisha yao. Hali hii imekithiri Kigoma, ambapo wanawake huzaa watoto wengi zaidi kuliko wastani wa nchi.” Kiwango cha uzazi kwa Kanda ya Magharbi ikiwemo Kigoma ilikuwa ni watoto 7 ikilinganishwa na wastani wa watoto 5 kwa Tanzania na wastani wa watoto 2.5 duniani.
Katika kanda ya Magharibi 30% ya wanawake wenye umri wa miaka 15-19 wamekwisha anza uzazi ikilinganishwa na 16% katika kanda ya Kaskazini.
 Kwa mujibu wa Tafiti za Viashiria vya Demografia na Afya (Tanzania Demographic and Health Survey TDHS) 2010, 25% ya wanawake walioolewa nchini na kiasi cha 41% ya wanawake walioolewa Kigoma wana mahitaji yasiyokidhiwa ya uzazi wa mpango.
 Hii ina maana ya kuwa hawataki kupata ujauzito (wanahitaji kuacha nafasi ya kutosha kati ya mimba au kupunguza idadi ya mimba) lakini hawatumii njia yoyote ya uzazi wa mpango. Zaidi ya haya, 34% ya wanawake walioolewa nchini, ingawa ni 25% ya wanawake walioolewa Kigoma, hawataki kupata ujauzito na wanatumia uzazi wa mpango kuzuia mimba isiyopangwa.
 Data hizi zinaashiria kuwa kuna umuhimu wa kuongeza matumizi ya uzazi wa mpango. Vitu vinavyopelekea uzazi wa mpango kutowafikia wanawake ni pamoja na imani za dini, kabila au utamaduni; ufahamu mdogo kuhusu faida za uzazi wa mpango; dhana potofu kuhusu athari za uzazi wa mpango; na pia matumizi madogo ya njia za kisasa za uzazi wa mpango kwa upande wa vijana – vyote hupelekea ujauzito usiopangwa na uzazi hatarishi.
Upatikanaji wa huduma pia huzoroteshwa na uhaba wa fedha katika kumudu kununua bidhaa za uzazi wa mpango na vifaa tiba. Uzazi wa mpango ni mkakati muhimu katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuboresha afya ya mama na mtoto nchini.
Mtaalam wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ya mkoa Kigoma ambaye pia Mratibu wa kampeni ya Thamini Uhai Jitofautishe inayoendeshwa na Shirika la world Lung Foundation mkoani Kigoma, Dk.Kalist akitoa maelezo kuhusiana na njia za kuzuia uzazi wa mpango na faida zake.

Mpango mkakati wa kitaifa wa kupunguza vifo vya akina mama, wachanga na watoto (The National Road Map Strategic Plan to Accelerate Reduction of Maternal, Newborn and Child Deaths in Tanzania) ya 2008–2015 (Sharpened One Plan) umepanga lengo la kuongeza matumizi ya uzazi wa mpango kutoka 27%1 mpaka 60% ifikapo 2015.
Ongezeko la matumizi ya uzazi wa mpango limetambulika kuwa na uwezo mkubwa wa kusaidia kufikia lengo hili la Mpango wa Sharpened One la kupunguza uwiano wa vifo vya uzazi (MMR) kutoka 578 kufikia 193 kwa kila uzazi 100,000 mpaka kufikia 2015.
Awamu hii ya pili ya kampeni ya Thamini Uhai imelenga kusaidia kufikia malengo haya. . Taarifa muhimu kwa wahariri Kuhusu Thamini Uhai Thamini Uhai ni kampeni ya afya ya mama iliyoanza mwaka 2014 inayotilia mkazo umuhimu wa kujifungua katika kituo cha afya.
Kampeni hii mpya inapanua Thamini Uhai kuhusisha uzazi wa mpango, kwa kuandaa matangazo ya redio na michezo ya kuigiza ya redio yenye ujumbe wenye hisia. Matangazo matatu ya redio yameanza kurushwa Radio Kwizera, Tanzania Broadcasting Corporation (TBC), na Clouds FM, kwa wiki 15 kuanzia Mei 25.
Mfululizo wa mchezo wa kuigiza wa redio, Jitofautishe, inarushwa hewani kupitia TBC na Radio Kwizera. Mchezo huu wa kuigiza unatilia mkazo umuhimu wa wenza na familia katika uzazi wa mpango ili kunufaisha wanawake na familia. 1 The CPR, which is the percentage of couples using contraception, was measured at 27% in 2010 (TDHS 2010).
 Pamoja na matangazo ya redio na mchezo wa kuigiza, kampeni pia ina jarida, mabango na uhamasishaji jamii. Pia kampeni imelenga kuwafikia wananchi wengi zaidi kipitia mtandao wa kijamii wa intaneti kwa kutumia hashtag #ThaminiUhai kusambaza ujumbe.
 Kuhusu Programu ya Afya ya Akina Mama WLF Data iliyotolewa karibuni na Shirika la Afya (WHO), UNICEF, UNFPA na Benki ya Dunia2 inakadiria kuwa ingawa mwaka 2010 idadi ya vifo vya akina mama nchini Tanzania ilikuwa asilimia 3 ya vifo vyote vya uzazi duniani, hata hivyo Tanzania imefanikiwa kupunguza kiwango cha vifo vya uzazi kwa asilimia 55 kati ya mwaka 1990 na 2013.

Mwenyekiti wa mkoa Kigoma wa wahamasishaji jamii kuhusu matumizi ya njia za uzazi wa mpango katika kampeni ya thamini Uhai Jitofautishe, Benjamen Kulinjie akitoa ushuhuda namna kampeni hiyo ilivyoweza kupata mafanikio katika kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto na matumizi ya njia za uzazi wa mpango.
Tokea mwaka 2006, WLF imefanya juhudi kubwa kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga nchini Tanzania kwa kutekeleza mradi unaotumia teknolojia na vifaa vya kisasa.
Mpango huu unaofadhiliwa na Bloomberg Philanthropies, Fondation H&B Agerup’, Merck For Mothers na Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA), umelenga kuimarisha upatikanaji wa huduma bora ya uzazi kwa akina mama hususan wale walio vijijini na maeneo yaliyopo pembezoni mwa nchi.
World Lung Foundation inaweza kuonyesha mafanikio yaliyopatikana nchini katika vituo muhimu vya afya na hospitali katika wilaya saba katika mikoa ya Kigoma, Morogoro na Pwani.
*Tokea 2008:World Lung Foundation imeimarisha vituo 10 nchini Tanzania ili vituo hivi viweze kutoa huduma bora na salama ya afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na upasuaji.
*Kabla ya uboreshaji huu, wagonjwa walisafiri masaa 3-4 kufikia hospitali ya karibu. Sasa, huduma ya dharura ya uzazi inapatikana katika jamii.
*Zaidi ya wafanyakazi wa afya 100 wasio madaktari wamepewa mafunzo katika huduma ya dharura ya uzazi au upasuaji na utoaji wa nusu kaputi.
* Matumizi ya vituo vya afya kwa ajili ya uzazi umeongezeka kwa kiwango kikubwa. Kabla ya mradi katika vituo vyote tisa huduma ya uzazi ulitolewa kwa wagonjwa 3,500 kwa mwaka. Hadi kufikia mwaka 2011 idadi hii iliongezeka na huduma ilitolewa kwa wagonjwa 12,300 mwaka 2014 baada ya mradi wa WLF kutekelezwa.
* Zaidi ya upasuaji 2,500 umefanyika katika vituo hivi, jambo ambalo lisingewezekana kabla ya maboresho yaliyofanywa na mradi wa WL.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la World Lung Foundation Dk.Nguke Mwakatundu (Mwenye tai aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na Waganga Wakuu wa wilaya za mkoa Kigoma na waratibu wa kampeni za uzazi wa mpango na wahamasishaji jamii juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango  kwenye halmashauri za mkoa Kigoma wakati wa mkutano wa tathmini ya kampeni ya thamini Uhai Jitofautishe.


Related

OTHER NEWS 2189741411623217482

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item