Kadhalika,
ipo miradi iliyobuniwa ambayo tayari imeanza kutekelezwa. Miradi hio ni:- Mradi wa kuimarisha huduma za
mama na mtoto, Mradi wa ujenzi wa jengo la wodi ya watoto, Mradi wa upasuaji wa
maradhi ya kichwa na uti wa mgongo (Neurosurgical unit), Mradi wa kitengo cha
“Gastro-Enterology”, Mradi wa kuimarisha kitengo cha kisasa cha wodi ya
wagonjwa mahututi (ICU) na Mradi wa elimu ya utafiti. Vile vile, maandalizi ya utibabu wa matatizo
ya maradhi ya haja ndogo na figo yameanza.
Hospitali
ya Wete imefanyiwa matengenezo katika wodi ya wanaume pamoja na vyoo vyake,
kliniki ya watoto pamoja na kupatiwa vifaa vya kisasa. Aidha, imejengwa Maabara
mpya kubwa na ya kisasa kwa kushirikiana na “International Center for Aids care and treatment Programme” ( ICAP)
katika hospitali ya Micheweni.
Kwa
kupitia mashirikiano yaliyoanzishwa baina ya hospitali ya Kivunge na mradi wa HIPZ, hospitali
imefanikiwa kuanzisha kitengo cha huduma
za dharura (Emergency Unit)
kitakachotoa huduma za haraka kwa wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapo
pamoja na kufanyiwa matengenezo kwa kituo cha elimu ya kujiendeleza (Resource Centre) iliyopo hospitalini
hapo.
Katika kutekeleza mpango wa kuifanya Hospitali ya
Abdalla Mzee kuwa hospitali ya Mkoa, mchakato umeanza ambapo Hospitali hii
itajengwa kwa msaada mkubwa kutoka Jamhuri ya Watu wa China na itakuwa ni ya
kisasa yenye uwezo wa kutoa huduma za wagonjwa wa maradhi mbali mbali na
wagonjwa mahututi (ICU), huduma za dharura (accident
and emergency) na huduma za uchunguzi wa CT Scan.
Katika kipindi hiki huduma za
matibabu ya macho zimefanyika na uchunguzi na utibabu wa macho kwa wafanyakazi
na wanafunzi 69 wa Jeshi la Polisi umefanyika. Askari 51 walipatiwa miwani na 18 walipewa dawa za
macho. Huduma za uchunguzi na utibabu wa macho zimetolewa kwa wananchi katika
maeneo mbali mbali Unguja na Pemba.
Kwa kushirikiana na Kitengo cha Elimu Mjumuisho na
Stadi za Maisha cha Wizara ya Elimu, na Timu za Afya za Wilaya, kitengo cha
maradhi ya macho kimeweza kufanya uchunguzi na utibabu wa macho kwa jumla ya
wanafunzi 2,665 wa skuli mbali mbali ambao
kati yao, 587 walipatiwa matibabu ikiwemo dawa za macho, ushauri wa
kiafya na utoaji wa miwani.
Serikali iliahidi kukiimarisha Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya pamoja
na watumishi wa sekta ya afya kwa kuwapatia mafunzo ya ndani na nje ya nchi.
Utekelezaji wa ahadi hii umekwenda vizuri ambapo wafanyakazi 226
wamepelekwa mafunzo ya muda mrefu na ya muda mfupi katika vyuo mbali
mbali.
Chuo
cha Taaluma za Sayansi za Afya sasa kitaunganishwa na SUZA katika kukiendeleza,
uamuzi huu hivi sasa unafanyiwa kazi na Serikali.
Katika kuziimarisha afya za wanawake,
Serikali imeondoa ada ya Tsh. 40,000 kwa akinamama wanaokwenda kujifungua kwa
operesheni. Kadhalika, huduma za bohari kuu ya dawa zimeimarishwa ili
kurahisisha upatikanaji wa dawa nchini.
Bohari Kuu mpya ya dawa ilifunguliwa rasmi huko Maruhubi katika
shamrashamra ya Sherehe za Maadhimisho
ya miaka 49 ya Mapinduzi mwezi Januari, 2013.
UTAWALA BORA
Ndugu Waandishi wa Habari
na ndugu Wanachi,
Suala la Utawala Bora hivi sasa nimeliweka
katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kufuatia mabadiliko
ya Wizara niliyoyafanya hivi karibuni.
Katika kutekeleza dhamira yetu ya kupambana na
rushwa, Serikali ya Awamu ya Saba imeanzisha Taasisi ya Kuzuia Rushwa na
Uhujumu wa Uchumi kwa kupitisha sheria namba 1 ya mwaka 2012. Kuanzishwa kwa
Taasisi hiyo ambayo imeshaanza kufanya kazi kutaisaidia Serikali kupambana na rushwa nchini kama
Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010 ilivyoagiza.
Serikali inaendelea kuimarisha Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar ili iweze kuendesha mashtaka katika ngazi zote
za mahakama. Aidha, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inazidi
kuimarisha kwa kuwapa mafunzo wafanyakazi wake kwa lengo la kuimarisha
ukaguzi na uhakiki wa mali za Serikali. Asilimia 88 ya wafanyakazi katika ofisi hii
wameweza kupatiwa elimu ya juu. Aidha, mazingira ya kufanyia kazi yameimarishwa
ikiwa ni pamoja na kuipatia Ofisi kwenye majengo ya kisasa na vitendea kazi vya
kisasa.
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
imepata sifa ndani na nje ya nchi kama vile katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
pamoja na SADC kwa ufanisi katika utendaji wake. Baadhi ya nchi zinaleta
wataalamu wao kuja Zanzibar kujifunza
hasa Computerized Auditing. Kadhalika, nchi kadhaa zimekuwa
zikitaka ushauri kutoka Ofisi hii.
Utekelezaji wake umefikia asilimia 67 kwenye lengo la ukaguzi.
Ndugu Waandishi wa Habari
na Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha utoaji wa haki, Serikali
inaendelea kuimarisha Mahakama Kuu na Mahakama ya Kadhi kwa kufanya ukarabati
wa majengo yake. Ndani ya kipindi cha miaka mitatu mahakama ya watoto imeweza
kuanzishwa kwa lengo la kulinda haki za watoto nchini.
Vile vile, idadi ya majaji imeweza kuongezeka
kutoka watatu hadi kufikia 6 wakiwemo majaji wanawake kwa mara ya kwanza.
Kadhalika, Mahakama inaendeleza mapitio ya sheria mbali mbali ili kuweza kuimarisha utoaji wa huduma katika
sekta hiyo.
Kuhusu kuanzishwa kwa mahakama ya biashara,
sheria imeshapitishwa na sasa kanuni zinaendelea kutayarishwa hivyo, mahakama
hiyo itaanza kufanya kazi hivi karibuni.
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
Suala la Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaaa
na Idara Maalum za SMZ nimeziweka kwenye Ofisi ya Rais, katika mabadiliko ya
wizara niliyoyafanya hivi karibuni.
Kuwepo kwa serikali za mitaa ni mafanikio
makubwa yanayotokana na demokrasia na utawala bora nchi. Ndani ya kipindi cha
miaka mitatu Serikali imeanza kuifanyia mapitio Sheria za Serikali za Mitaa na
Tawala za Mikoa ambapo Mpango wa Mageuzi ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, umeandaliwa na Sera yake imeshapitishwa na karibuni inatarajiwa kuanza
kufanya kazi. Serikali za Mitaa zimeanza
kuimarishwa kwa kuajiriwa watalaamu wa fani mbali mbali, vifaa vya kisasa na
vitendea kazi ili kutoa huduma bora kwa wananchi. Jitihada kubwa inafanywa katika kuwahamasisha
wananchi kuunda Kamati za Maendeleo yao ili kusukuma kasi ya maendeleo. Vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa kupitia
mfumo wa Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii.
Suala la usafi wa miji na hifadhi ya mazingira nalo linashughulikiwa.
UTUMISHI WA UMMA
Katika kipindi hiki cha miaka mitatu
nimeanzisha utaratibu wa Watendaji na Mawaziri kubainisha utekelezaji wa bajeti
za Wizara zao na jinsi wanavyosimamia mipango iliyoandaliwa kwa kila robo mwaka
hapa Ikulu. Aidha, Serikai imeandaa miundo ya Utumishi ya Wizara na Taasisi zake kwa lengo
la kuleta uwiano wa kimaslahi kwa
kuzingatia viwango vya elimu na uzoefu wa utumishi wa wafanyakazi.
Utekelezaji wa miundo ya utumishi utaanza hivi karibuni. Masuala ya Kazi na Utumishi wa Umma nayo
nimeyaaweka katika Ofisi ya Rais katika mabadiliko ya Wizara niliyoyafanya hivi
karibuni.
Ndugu Waandishi wa Habari
na Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya
Saba, imefanya jitihada ya kuimarisha mishahara na stahili nyengine za
wafanyakazi mara mbili katika kipindi cha miaka mitatu. Vile vile, Serikali
imeongeza nafasi za mafunzo kwa watendaji wa Serikali ndani na nje ya nchi.
Chuo cha Utawala wa Umma kimezidi
kuimarishwa kwa kupatiwa jengo jipya huko Tunguu ambalo lilizinduliwa tarehe 5
Januari, 2013.
WAZEE, WATU WENYE ULEMAVU NA WATOTO
Ndugu Waandishi wa Habari
na Ndugu Wananchi,
Katika
jitihada za Serikali za kuanzisha makundi maalumu, Serikali ya Awamu ya Saba
imeweza kuzimiimarisha huduma za wazee kwa kuwaongeza posho hadi Tsh. 40,000
kwa mwezi, kuwapatia chakula cha uhakika kwa kila siku, kuimarisha huduma za
maji pamoja na kuimarisha ulinzi kwa wazee wanaoishi kwenye nyumba za Sebleni,
Limbeni na Gombani Pemba. Vile vile, Serikali imeimarisha juhudi za kulinda
haki za watoto kwa kuanzisha sheria mpya
ya kumlinda mtoto ya mwaka 2011, kuongeza vituo vya Mkono kwa Mkono hadi
kufikia vinne pamoja na kuanzisha mahakama ya watoto hapa Zanzibar kwa lengo la kuzilinda haki zao.
Katika
kipindi hiki cha miaka mitatu,huduma za watu wenye ulemavu zimeimarishwa. Zoezi la usajili kwa ajili ya kuimarisha
huduma na haki zao, likiwemo suala la elimu kwa watoto limefanyika. Tarehe 28 Septemba, 2012 Serikali iliizindua
Mfuko wa kuwasaidia watu wenye ulemavu na
hadi sasa jumla ya Tsh. 198 milioni zimepatikana.
HABARI, UTAMADUNI NA
MICHEZO.
Ndugu Waandishi wa Habari
na Ndugu Wananchi,
Katika
eneo la vyombo vya Habari, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka
2010-2015 inaelekeza Serikali kusimamia utekelezaji wa Sera ya Habari na
kuendeleza uhuru wa vyombo vya habari nchini. Katika kutekeleza agizo hili, Serikali katika kipindi cha
miaka
mitatu imetoa vibali vya kuanzishwa Redio nne (4) za FM na Televisheni tano (5). Sambamba na
hatua hizo, Shirika
la Magazeti ya Serikali limeweza
kuwafikia wasomaji wengi zaidi kwa kuongeza maeneo ya usambazaji Unguja na
Pemba na Tanzania Bara.
Ndugu Waandishi wa Habari
na Ndugu Wananchi,
Katika
kipindi hiki Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) lilianzishwa na Serikali
ililazimika kuchukua hatua kadhaa, kama vile kununua vifaa na mitambo ya kisasa, ili viweze
kuyarusha matangazo yake kwa ufanisi, kuonekana na kusikika katika sehemu mbali
mbali ndani na nje ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Katika kipindi hiki
Serikali ilifanya uamuzi wa kuingia katika utaratibu wa kisasa wa digitali kwa
kununua vifaa na mitambo mipya, kwa ajili ya kuimarisha shughuli za utangazaji
Zanzibar na mafunzo ya kuwaendeleza wanahabari mbali mbali yalitolewa kwa lengo
la kuyatekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa. Katika kipindi hiki jumla ya
waandishi 38 wameweza kupatiwa mafunzo katika viwango vya stashahada, shahada
ya kwanza na shahada ya pili. Vile vile, Serikali iliyaimarisha matangazo ya redio kwa
kuuhamisha mnara wa masafa ya kati (medium waves) kutoka Chumbuni na kuupeleka
Bungi, ambako Ofisi na Studio mpya na nyumba mbili (2) za kisasa za familia nne
za wafanyakazi zimejengwa. Aidha,
ukarabati wa mnara wa mawimbi mafupi (short
wave) nayo umefanyika. Ukarabati huo umefanywa kwa ushirikiano wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Ndugu Waandishi wa Habari
na Ndugu Wananchi,
Chuo
cha Uandishi wa Habari nacho kimeimarishwa kwa lengo la kujitosheleza kwa
wanahabari. Vifaa vya kufundishia
vilinunuliwa na walimu wenye ujuzi waliajiriwa.
Katika kuimarika kwa chuo hicho, hivi sasa wanafunzi wanaosomea cheti na
stashahada wameongezeka kutoka 75 mwaka 2009/2010 hadi kufikia 122 kwa mwaka
2010/2011.
Kwa upande mwingine, Serikali
imelishughulikia tatizo la uingizaji wa vifaa vya utangazaji vilivyopitwa na
wakati TV na redio ili kuepusha Zanzibar kugeuzwa jaa. Serikali ilitekeleza kwa mafanikio makubwa
Mkakati wa Mageuzi
ya Teknolojia
ya Utangazaji kutoka analogi kwenda dijitali nao umetekelezwa vyema.
Vile vile, jengo la Utangazaji la
zamani liliopo Rahaleo limefanyiwa ukarabati mkubwa ili liweze kutumika kwa
ajili ya studio za kurikodia nyimbo za wasanii wetu. Hivi sasa Serikali tayari ishachukua hatua ya
kununua vifaa vya studio hio.
Ndugu Waandishi wa Habari
na Ndugu Wananchi,
Katika
kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Serikali imechukua hatua za kuifanyia
mapitio marekebisho sera ya Utamaduni na Michezo na sheria zinazoongoza taasisi
zinazosimamia utamaduni ili ziweze kuenda sambamba na wakati huu wa kuihusisha
sekta ya utamaduni na utalii kwa wote.
Katika
kuufanya utamaduni uwe na tija zaidi, wizara imeweza kukamilisha mchoro wa
ramani ya Utamaduni katika shehia za Unguja na Pemba pamoja na Utafiti wa
Urithi wa Utamaduni katika mikoa mitano ya Zanzibar na hatimaye ihifadhiwe na
itangazwe nchi za nje kwa kuingizwa katika orodha ya “UNESCO” ya tamaduni
zinazohifadhiwa. Hivi sasa Serikali imo katika mchakato wa kuifanyia
marekebisho makubwa sheria ya sanaa inayokusanya mambo yote ya utamaduni. Mswada huo wa sheria hivi sasa unaandaliwa.
Kuhusu ujenzi wa kiwanja cha kisasa cha michezo na
sherehe za kitaifa, Serikali imeuchagua uwanja wa Mao Tse Tung uliopo mjini Unguja utumike kwa shughuli hizo. Hatua
iliofikiwa hivi sasa ni
kukamilika michoro ya awali. Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imekubali
kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi huo na mkataba
wa makubaliano tayari umetiwa saini na pande mbili.
Ndugu Waandishi wa Habari
na Ndugu Wananchi,
Uwanja
wa Gombani Pemba tayari ulifanyiwa marekebisho kwa kuweka nyasi bandia na hivyo
kukidhi haja ya mashindano ya kimataifa ya mpira wa miguu. Halikadhalika,
matengenezo ya taa za uwanja yamekamilika ambayo yanauwezesha uwanja kutumika
hata wakati wa usiku. Serikali hivi sasa imeanza utaratibu wa kuezeka paa jipya
na ujenzi wa njia ya kukimbilia ili kutoa fursa ya michezo ya riadha kufanyika
kukidhi viwango vya kimataifa. Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Japan
ujenzi wa kiwanja cha michezo ya ndani umeanza na unategemewa kukamilika
mwishoni mwa mwezi wa Disemba 2013.
Kwa
upande wa Uwanja wa Amaan, ukarabati mkubwa unafanyika kuimarisha eneo la
kuchezea ambapo utawekewa nyasi bandia. Kazi hii inatarajiwa kukamilika
katikati ya mwezi wa Disemba na utatumika kwa ajili ya mashindano ya
maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi.
Ndugu Waandishi wa Habari
na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya Uongozi wangu,
Serikali imechukua hatua mbali mbali kuzilinda, kuzihifadhi na kuzidumisha mila, silka na
maadili mema ya Wazanzibari. Hatua
zimechukuliwa za kuzikagua kazi za sanaa na kuchukuliwa hatua za kuilinda na
kuhifadhi mila na silka kulingana na matokeo ya ukaguzi huo. Kukamilika kwa kamusi la
Kipemba, Kimakunduchi, Kitumbatu kutapelekea wananchi kuyatumia makamusi hayo
ili kuulinda utamaduni wetu.
Aidha,
kumekuwa na uhakiki wa Matamasha, Matangazo
ya kibiashara, Video
za nyimbo, Tenzi
zenye maudhui mbali mbali
na Filamu tofauti katika
maduka ya kukodishia
kanda Unguja na
Pemba. Bodi imekagua pia vikundi vya ngoma, michezo ya kuigiza jukwaani,
tenzi na mashairi ya kughani ili kuhakikisha mila, silka na utamaduni wa
Kizanzibari hauathiriwi na mambo hayo.
Hatua hizo zimekwenda sambamba na hatua za
kuhifadhi kumbukumbu za kihistoria na Mambo ya Kale. Utafiti wa uchimbaji wa eneo la Ngome
Kongwe, Forodhani Unguja kulingunduliwa vigae vya vyungu, ‘Kwale pottery’ vya
karne ya kwanza. Aidha, matengenezo yamefanyika kwa jengo la makumbusho la
Mahodhi ya Hamamni (Hamamni Baths) ili kulirudisha katika hadhi yake ya awali
na kuweza kuongeza idadi ya vivutio kwa wageni. Serikali imeyafanyia
matengenezo majengo ya Mangapwani kwenye Mahandaki ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia
pamoja na mnara wake na magofu ya Kizimbani na Hamamni na jengo la Beit el
Ajaib.
MAZINGIRA
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Serikali
imeweza kutekeleza majukumu muhimu ya kuyalinda na kuyahifadhi mazingira ya
nchi yetu kwa kulingana na Sheria, Sera na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2010- 2015.
Mambo makuu yote
yaliyozingatiwa kwenye Ilani na kwenye MKUZA II yameweza kutekelezwa kwa
mafanikio makubwa. Serikali imeweza kufanya mapitio ya Sera ya Mazingira ya mwaka 1992 na
kuzindua Sera ya Mpya ya Mazingira ya mwaka 2013 ambayo inatoa muongozo kwa
shughuli za uhifadhi wa mazingira nchini kwa kuzingatia hali halisi ya
kimazingira ilivyo na kwa kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi. Mapitio
ya Sheria ya Mazingira ya mwaka 1996 yamelenga katika kuongeza nguvu za
kisheria katika kuyahifadhi na kuyasimamia mazingira nchini. Sambamba na hatua hizo, Serikali imepitisha
kanuni mbili za usimamizi wa mazingira.
Kanuni
ya kwanza ni ya usimamizi wa maliasili zisizorejesheka, ambayo inatoa miongozo
ya uvunaji endelevu wa maliasili hizo na kupunguza wimbi la uchimbaji kiholela
wa mawe na mchanga. Kanuni ya pili ni ya
kupiga marufuku mifuko ya plastiki, ambayo inakataza kuingiza, kutumia,
kusafirisha na kuhifadhi mifuko ya aina yote ya plastiki hapa Zanzibar. Jumla ya tani 288 za plastiki zimekamatwa na
kuteketezwa na wanaohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.
Hivi
karibuni Serikali ilianzisha na kuzindua Kikosi kazi cha udhibiti wa uharibifu
wa mazingira katika visiwa vya Zanzibar.
Uanzishwaji wa Kikosi kazi hicho ni hatua muhimu na ya lazima ya kulinda
mazingira yetu, dhidi ya vitendo vyote vibaya vinavyoathiri mazingira. Tangu kilipozinduliwa kikosi kazi hicho watu kadhaa wameshakamatwa
na taratibu za kisheria zimechukuliwa dhidi yao.
Ndugu waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Sera mpya ya Mazingira ya 2013 inaelekeza kutoa elimu kwa
wananchi juu
ya umuhimu wa utunzaji na hifadhi ya mazingira na kuimarisha ukaguzi katika
maeneo ya makaazi, viwanda na
mahoteli. Elimu imesisitizwa juu ya
umuhimu wa kuhifadhi misitu,umuhimu wa mikoko, maliasili
zisizozalishika,uhifadhi wa bioanuwai, na kadhalika.
Ndugu Waandishi wa Habari na Ndugu Wananchi,
Kwa
upande mwingine Serikali imefanya mapitio ya Uchaguzi ya miradi ya vitega
uchumi ili kujua athari za mazingira na kupendekeza hatua za utekelezaji.
Katika kipindi hicho jumla ya miradi 160 imefanyiwa ukaguzi na kupewa miongozo
na ushauri wa kimazingira. Vilevile miradi ya maendeleo na vitega uchumi 51
imefanyiwa tathmini ya athari za kimazingira na kutolewa vyeti vya mazingira
kwa miradi hiyo.
Masuala mengine yaliyotekelezwa katika kipindi hicho ni
kushughulikia suala la mabadiliko ya tabianchi kwa kufanya utafiti, kuangalia
athari za mabadiliko ya tabianchi kwa uchumi wa Zanzibar na kuorodhesha maeneo
yanayoingia maji ya chumvi ambapo jumla ya maeneo 148 yameathirika Unguja
(maeneo 25) na Pemba (123).
Aidha,
Serikali imeandaa ramani ya mazingira na kuanzisha mfumo wa kuweka taarifa za
kimazingira kwa njia ya ramani kwa kutumia kompyuta yaani Zanzibar Environmental Information Management System (ZEIMS).
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
NA WAZANZIBARI
WANAOISHI NCHI ZA NJE (DIASPORA)
Ndugu Waandishi wa Habari
na Ndugu Wananchi,
Serikali
ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba imeanzisha
Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wanzanzibari Wanaoishi
Nje (Dispora) kwa lengo la kurahisisha
na kushajishisha ushiriki wao katika
harakati za maendeleo ya nchi yao. Kwa
kupitia idara hii, Wazanzibari walioko nje wanaendelea kutoa michango mbali
mbali ikiwemo ya fedha na kitaalamu katika sekta mbali mbali za kiuchumi na
kijamii. Aidha, Idara imekuwa ikifanya kazi ya kuwahamasisha Wazanzibari
walioko nje kuja kuwekeza nchini.
Kupitia
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Idara
ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wanzanzibari Wanaoishi nje imeimarisha ushiriki wa Serikali yetu katika
masuala na mikutano mbali mbali ya Kimataifa.
Vile
vile, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imeimarisha
mashirikiano na nchi mbali mbali, Taasisi za Kimataifa na washirika wote wa
Maendeleo.
MWISHO
Ndugu Waandishi na Ndugu Wananchi,
Napenda
nitoe shukurani zangu za dhati kwa wananchi wote kwa kushirikiana na Serikali.
Ni matumaini yangu kwamba wananchi wataendelea kushirikiana na Serikali na vile
vile wafanyakazi wote wa Serikali wataendelea kuongeza juhudi zao ili tuweze
kutekeleza malengo yetu ya DIRA YA MAENDELEO 2020. Hivi sasa tumebakiwa na miaka sita tu hadi
kuyafikia malengo hayo. Pindi kama tukiyafikia, hapana shaka tutaitoa nchi
katika kundi la nchi za kipato cha chini na kuwa katika kundi la nchi za kipato
cha kati (Middle income).
Bila
ya shaka yoyote, hali hiyo tutaifikia tu tukiwa makini, watiifu wa amani na
utulivu nchini. Utiifu wa sheria ni hatua moja muhimu katika kuyafanikisha
hayo. Ni jukumu la viongozi wote wa Serikali,
wanasiasa, viongozi wa dini na viongozi wengine katika jamii, sote kwa
pamoja tutekeleza wajibu wetu kwa kuhakikisha kwamba amani na utulivu
unadumishwa na sheria za nchi zinafatwa.
Ilivyokuwa Serikali inaongozwa kwa misingi ya Katiba na Sheria zake,
basi vyama vyote vya siasa, taasisi zisizokuwa za Serikali na zile za jamii
nazo ni lazima ziongozwe kwa kuzingatia katiba za nchi, katiba zao na kanuni
zao na kuzifuata sheria za nchi. Sura ya
Tatu ya Katiba yetu imeelezea kuhusu Kinga ya Haki za Lazima, Wajibu wa Uhuru wa
Mtu Binafsi, kuanzia kifungu cha 11 hadi kifungu cha 25. Lakini kila mtu ana wajibu wa kufuata na
kuitii Katiba ya Zanzibar na Sheria zake. Hili ni jambo muhimu na ni lazima
tuyaenzi na tuyadumishe Mapinduzi yetu na tuudumishe na tuuendeleza Muungano wetu
kwani ndio nguzo yetu kubwa ya maendeleo
na vilivyotufikisha hapa tulipofika hivi sasa na tunakokusudia kufika katika
miaka mingi ijayo. Katika kipindi hiki
tumeshuhudia Muungano wetu umeendelea kuwa imara zaidi tangu pale ulipoanzishwa
na nchi yetu imepata heshima kubwa sana katika Jumuiya ya Kimataifa. Tumepata mafanikio makubwa ya kisiasa,
kiuchumi na ustawi wa jamii, ingawa zimekuwepo baadhi ya changamoto lakini
zitaendelea kushughulikiwa hatua kwa hatua.
Napenda
niwahakikishie wananchi wote kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika
kuendeleza Muungano wetu, kuimarisha na kuwatumikia wananchi. Katika kuuimarisha Muungano wetu, sote
tumetimiza wajibu kwa kutoa maoni yetu kwa ajili ya kuandaliwa Katiba Mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume ya
Kuratibu Maoni ya Katiba Mpya umefanya kazi nzuri na itaendelea kuifanya kazi
hio kama vile sheria inavyoiongoza.
Hatua zilizobakia nazo zitakamilishwa kwa kuzingatia sheria iliyopo ili
hatimae tupate Katiba Mpya itakayoliongoza Taifa letu na kuimarisha Muungano
wetu. Napenda nimshukuru na nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusimama imara katika kuutetea na
kuuendeleza Muungano wetu na kwamba siku zote yuko tayari kuzizungumzia
changamoto zinazoukabili Muungano wetu na kutafuta njia za kuzipatia ufumbuzi
kila zinapotokea.
Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza na kuudumisha Muungano kwa manufaa ya
nchi zetu mbili.
Hivi
sasa tumemaliza miaka mitatu tangu SMZ yenye Mfumo wa Umoja wa Kitaifa imeingia
madarakani. Hata hivyo, bado ipo kazi
kubwa mbele yetu ambayo inahitaji jitihada zetu sote. Tuendelee kushikamana na kupendana,
tushindane kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa bila ya kugombana,
kukashifiana, kulaumiana, kutukanana na kudharauliana. Zanzibar haitajengwa kwa
mambo hayo yasiyokuwa na tija wala faida.
Huu ni wakati wa kuongeza kasi na kuijenga nchi yetu, ili tusije
tukaachwa nyuma.
Napenda
kuwahakikishia wananchi wote kuwa serikali kwa upande wake itaendelea
kutekeleza wajibu wa kikatiba na sheria kwa kuilinda amani, utulivu, mali na
maisha ya watu. Hakuna atakayedhulumiwa wala kuonewa, lakini pia hakuna
atakayevumiliwa kwa kuvunja sheria.
Tukiwa
tumo katika kipindi cha shamrashamra ya kusherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya
Zanzibar, natoa wito kwa kila mmoja wetu awe ni sehemu ya kuzifanikisha sherehe
zetu kwa furaha, salama, amani na utulivu. Tushirikiane sote kwa pamoja na
tuendeleze umoja na mshikamano katika kuzifanikisha sherehe zetu, ili tuioneshe
dunia mafanikio yetu ya miaka 50, utamaduni wetu na kwamba tunauthamini umoja
wetu, amani na mshikamano.
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.