TAMKO LANGU KWA UMMA KUHUSU MCHAKATO WA KUANDIKA KATIBA MPYA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Ndugu wanahabari na wa Tanzania wenzangu, Nimekuwa nikilazimika kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa wanahabari, ndugu, jamaa na ma...
https://gabriellabridalsolution.blogspot.com/2014/02/tamko-langu-kwa-umma-kuhusu-mchakato-wa.html
Ndugu wanahabari na
wa Tanzania wenzangu,
Nimekuwa nikilazimika kujibu maswali mbalimbali kutoka
kwa wanahabari, ndugu, jamaa na marafiki kuhusiana na namna mchakato wa kuandika
katiba mpya ya Taifa letu unavyoenda; wengi wakipenda kujua nini mtazamo wangu
kuhusu mambo mengi, haswa hili la serikali mbili ama tatu kwenye muungano wetu.
Mara nyingi nimekuwa nikikwepa kusema msimamo wangu ni nini kwa sababu niliona
ni vema nikajipa muda wa kutafakari kabla ya kuamua kujenga msimamo yangu. Ila
kwa kuwa wakati wa kwenda Bungeni umefika na mimi nimepata bahati ya kuwa
miongoni mwa wajumbe wa Bunge hili la kihistoria nimeona leo nitoe mtazamo
wangu.
Kwanza, nianze kwa kuonesha wasiwasi wangu kama tutaweza kufika
salama huko tuendako. Si kwa sababu za kitabiri kama mnajimu, la, ni kwa sababu
za kisayansi, ambazo nitaziweka wazi hapa kama ifuatavyo:
(i.) Pamoja na
kwamba tume imefanya kazi nzuri ya kukusanya maoni na kuyaweka katika nyaraka
ambayo tutapaswa kuifanyia kazi, napata shida kama walikuwa makini katika
kuendesha zoezi hili. Kivipi, binafsi napata shida na methodology iliyowawezesha
kufikia ‘conclusion’ madhubuti kwamba watanzania asilimia 61 walitaka serikali
tatu. Kwa sababu za kisayansi naona tume ya Mhe. Jaji Warioba imepotoka na
kwamba kusema hivyo ni kutaka kulazimisha uhalali wa hoja hii nyeti kwenye
dokumenti ya Rasimu ya Katiba tunayopaswa kuipitisha bila kuwa na msingi wa
kitakwimu unaotokana na njia (methodology) za kisayansi za kukusanya ‘data’ na
kutafuta ‘validity’ na ‘generalizability’ ya taarifa husika.
(ii.) Kwa
jinsi mchakato ulivyo ni ngumu kusema kuwa leo tutaweza kubadili jambo nyeti
kama la ‘Muundo wa Muungano’ kuwa uwe ni wa Serikali mbili, ama moja, wakati
mapendekezo ya Tume, ambayo ‘yanaelezewa’ na Tume kuwa yanatokana na ‘maoni’ ya
wananchi walio wengi, 61% na pili mabaraza ya katiba [cf. Muundo katika mchakato
huu ni wa pyramid, kwamba unaanza na maoni ya wengi huku chini kwenye kitako,
baadaye mabaraza ya katiba hapo katikati na mwisho Bunge la Katiba, kabla ya
kura ya maoni]. Hivi inawezekana wapi Bunge Maalum la Katiba, kwa hapa
tulipofikia, likafanya mabadiliko kwenye mambo yanayohusu ‘muundo’ (structure)
wa Katiba? Yaani, kwamba inawezekana vipi wajumbe hawa 640 wabadilishe jambo
zito la kimuundo kama hili? Kimantiki haingii akilini. Uhalali huo unatoka wapi?
Lakini pia hapa hatuwezi kuondoa ukweli kwamba malalamiko na manung’uniko ya
baadhi ya watu yana mashiko, kuwa hivi kama hoja ya Chama Cha Mapinduzi ilikuwa
ni kuilinda ‘status quo’ ya muungano wa serikali mbili na kama walifanya kazi ya
kuwaelimisha wanaCCM nchini, na wanaCCM walikuwa wengi zaidi kwenye mabaraza ya
katiba ya wilaya [walishinda kwa zaidi ya asilimia 65, inatokeaje asilimia 61
watake muungano wa serikali 3?]
Nini tafsiri ya haya yote? Kwamba ukisema
unabadili leo muundo wa Muungano ukaleta wazo tofauti na lile linalotokana na
mapendekezo ya tume, kama yanavyosomeka kwenye Rasimu (sura ya 6), mfano
ukasema, ziwe serikali mbili tu badala ya tatu zinazopendekezwa, maana yake
unaongelea kuanza upya kutengeneza vifungu vipya vya ‘kimuundo’ vya serikali za
mitaa, wawakilishi wa wananchi, mambo ya wakuu wa mikoa ama majimbo(provinces) –
jambo ambalo litakuwa cumbersome! Vurugu mechi bila uwepo wa rasimu! Swali la
kujiuliza hapa ni kwamba – hivi tume hawakuliona hili? Pengine wangeweka chaguzi
(option) pembeni, maana maoni yote haya wanayo, ila kwa sababu ya muundo wa
Muungano ‘waliouchagua’ hawakupenda kuelezea mambo binafsi ya serikali hizi
‘mbili’ za ‘iliyokuwa Tanganyika’ na Zanzibar kwa madai kwamba jukumu lao ni
kuandaa rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kinachoonekana hapa
ni kwamba walikwishaamua kuwa ziwepo serikali tatu kwa madai kuwa ndiyo maoni ya
wananchi na kwa kuzingatia msingi wa hoja kwamba Bunge la Katiba haliwezi kuwa
na uhalali wa kubadili mambo ya msingi ya kimuundo wa katiba, kama hili la
Muundo wa Muungano, bali ‘kuboresha’ tu yale yaliyomo. Mtu makini atahoji kuwa
ni kwa nini wamekwepa kuzungumzia ukweli kwamba ‘Tanganyika’ hayupo? Na nini
itakuwa hatma ya Katiba yake? Na ni lini wabia hawa wa Muungano walikaa
wakakubaliana washirikiane kwenye mambo yapi kwenye huo muungano wa Shirikisho?
Sasa wabunge wa Bunge maalum la katiba tukiukataa huu muundo wa serikali
tatu nini kitatokea? Maana yake sehemu kubwa ya rasimu hii italazimika
kubadilishwa.
(iii.) Jambo lingine ambalo litatusumbua ni kuwa, vipi kama
wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba tukiamua tujenge msimamo kwenye hoja ya
Serikali Moja itakuwaje? Maswali mengi yataibuka bila kupata majibu hapa, kuwa
ni nani atakuwa ‘Mpatanishi’ kwa niaba ya Tanganyika (ama Tanzania bara)? Maana
Zanzibar yupo na ana uhai wake kamili, Tanganyika yuko wapi hapa?
Mhe.
Jaji Joseph Warioba na wenzake wanapaswa wajibu maswali haya:
1. Ni njia
(methodology) ipi ya kisayansi na kitakwimu walitumia kufikia ‘conclusion’ hiyo
madhubuti kabisa kuwa 61% ya watanzania walitaka Muundo wa Serikali Tatu?
Watueleze watanzania sample size, sampling technique, sampling frame na namna
walivyowafikia na kuwahoji watu hao.
2. Watueleze ni nani aliyewatuma
kwenda kubadilisha Muundo wa Muungano?
3. Ni nani sasa atakuwa na
mamlaka ya kuandika Katiba ya Serikali ya Tanganyika (ama Tanzania Bara – ambaye
aliishakufa?), kama tukiamua kwenye Bunge la Katiba kupitisha Rasimu hii yenye
Muundo wa Muungano wa Serikali tatu? Tunaanzia wapi kumfufua Tanganyika?
Maoni yangu: Mtu yeyote mpenda demokrasia ataona wazi kwamba kuna utata
uliogubikwa na ukungu wa presha za kisiasa za kuona zoezi hili linakamilika.
Utata wa uhalali wa Bunge la Katiba kubadili hoja za msingi kwenye rasimu ni
jambo zito, na mashaka kwamba pengine Jaji Joseph Warioba na wenzake walikuwa na
ajenda yao ya siku nyingi ya kuleta serikali tatu kinyume na matakwa ya Chama
Tawala, CCM, ni jambo zito zaidi. Hivyo, kuondoa mamlaka na madaraka ya wananchi
(kama kweli yapo kama inavyosema tume) kwenye jambo zito la kimsingi kama Muundo
wa Muungano ni jambo linalotishia usalama wa mchakato na ni jambo lisilokubalika
kwa kuwa linaondoa haki, wajibu, mamlaka na madaraka ya wananchi kufanya maamuzi
kuhusu katiba yao (an act of popular sovereignity). Mkanganyiko huu unatia
mashaka zaidi ya kuleta mwangaza wa mabadiliko ya kutokea kwa maridhiano. Jaji
Warioba na wenzake walilijua hili na wameleta ‘chaos na frustration’ kwa maksudi
kwa kujificha chini ya kivuli cha ‘uhalali’ wa Bunge la katiba (yaani
‘legitimacy of rule or of law is based on the consent of the governed’) na
nadharia pana ya demokrasia yenye msingi kwenye kanuni za ‘popular sovereignity’
wakijua kabisa wabunge tutashindana, tutatofautiana!
Mimi nina maoni
kwamba, ili mchakato uishe salama, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Jakaya Kikwete aingilie kati, atumie mamlaka yake kusitisha mchakato huu
mpaka itakapoundwa tume nyingine ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu suala la
Muundo wa Muungano na kisha ipigwe kura maalum ya maoni kuhusiana na jambo hili
ili watanzania washiriki kikamilifu na waamue na siyo kufanya maamuzi ya
kubadilisha Muundo wa Muungano bila kutupa fursa ya kujadiliana na kushiriki
kufanya uamuzi kuhusu jambo hili. Ni jambo lisilo na busara hata kidogo kwenda
kujadili Rasimu ya Katiba bila kuwa na suluhu inayokubalika kuhusu Muundo wa
Muungano wetu.
Kama kuna presha ya muda wetu wa miaka mitano kuisha kuna
dirisha la kutokea; tusogeze mbele muda wa uhai wa Uongozi wa awamu hii ama
turudi nyuma tufanye mabadiliko ya sehemu za katiba zinazohusiana na Tume ya
Uchaguzi tu. Hatuna namna ya kukwepa moja kati ya mambo haya kwa sababu hata
tukifanikiwa kufunika kombe mwanaharamu apite, tukapitisha Katiba hii, bado
tutahitaji kufanya mabadiliko makubwa ya Sheria mbalimbali nay a kitaasisi
kutokana na Katiba mpya itakayokuwa imepatikana, zoezi ambalo kwa kila namna
litahitaji muda wa kutosha na sioni kama upo! Demokrasia ni gharama na
haikwepeki!
Maswali ni mengi zaidi ya Majibu. Wasiwasi ni mwingi kuliko
uhakika. Tutafika salama kwenye kupata Katiba hii kweli? Ni bora tukawie kuliko
kuvurunda. Tusikimbie kwa kasi bila kutazama tuendako, tutambae lakini macho
njiani na mbele tunakoelekea.
Tamko hili limetolewa na Ofisi ya Mbunge,
Jimbo la Nzega.
HK (Nimesaini)
Dkt. Hamisi Kigwangalla,
MB.
Posted by
MAPOCHISIDE BLOG