JAJI MKUU AISHUKIA TUME YA MAREKEBISHO YA SHERIA TANZANIA

  DAR ES SALAAM . JAJI Mkuu Mohamed Othman Chande ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuharakisha mchakato wake wa kuandaa...

 
DAR ES SALAAM.
JAJI Mkuu Mohamed Othman Chande ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuharakisha mchakato wake wa kuandaa ripoti inayohusu migogoro ya ardhi nchini ili kutoa nafasi ya kufanyiwa marekebisho Sheria ya Ardhi.
Jaji Chande ametoa kauli hiyo wakati ambao maeneo mbalimbali nchini yamekumbwa na migogoro mikubwa ya ardhi na kusababisha wananchi kupoteza mali,mifugo,makazi na wengine kuuawa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu sherehe ya Siku ya Sheria Nchini itakayofanyika Februari 3, mwaka huu, Jaji Chande amesema, “Ukiondoa idadi kubwa ya kesi za jinai, zinazofuata wa wingi ni kesi za migogoro ya ardhi, hasa za madai, mfano Mahakama Kuu ya Tanzania pekee kuna kesi za ardhi zaidi ya 6,000.”
Alisema asilimia 60 ya kesi hizo zinatoka kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya.“Mfumo wa kutatua kesi za ardhi uko chini ya mamlaka tatu. Ngazi ya chini kabisa ni Baraza la Ardhi la Kijiji ambalo lipo chini ya Serikali za Mitaa na Halmashauri. Pili, ni Baraza la Kata,” alisema na kuongeza.
“Na tatu ni Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ambalo mamlaka yake ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Baada ya hapo ndiyo kinafuata Kitengo cha Ardhi cha Mahakama Kuu” alisema.
Alisema tatizo lililopo sasa ni kwamba ili uweze kutatua migogoro ya ardhi ni lazima uangalie kesi husika ipo katika ngazi gani na kusisitiza kuwa migogoro mingi ipo katika ngazi za chini ambazo zipo katika mamlaka nyingine.
“Hivi sasa mfumo wa migogoro ya ardhi na mashauri ya ardhi unaangaliwa upya na Tume ya Kurekebisha Sheria ambayo imetembelea mikoa yote nchini na kukutana na wadau wote ikiwamo, mahakama, Wizara ya Ardhi, wananchi na wanasheria hivyo ripoti hiyo ikitolewa itasaidia kuboresha sheria,” alisema.
Mahakama za mwanzo
Akizungumzia mahakama za mwanzo, Jaji Chande alisema, “Tanzania tuna mahakama za mwanzo 960 lakini zinazofanya kazi ni 803, kati ya hizo zinazofanya kazi mahakama 487 ndiyo zina mahakimu wa kudumu na nyingine 316 hutoa huduma kwa kutembelewa na mahakimu mara moja au mbili kwa wiki kutokana na mahakimu kutoishi maeneo hayo.”
Alisema kwa sasa kuna uhaba wa majengo zaidi ya 296 ya mahakama za mwanzo, kwamba kuna majengo 157 ya mahakama za mwanzo ambayo hayafanyi kazi kwa sababu ya uchakavu.
Alisema mahakama hizo zinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kuwapo katika majengo chakavu na nyingine zikiwa ndani ya majengo yanayomilikiwa na taasisi mbalimbali na Serikali, jambo ambalo alisema linazifanya mahakama hizo kuonekana kutokuwa huru.
Alisema miundombinu ya mahakama nyingi ni mibovu na kutolewa mfano mahakama za mwanzo zilizopo katika Wilaya za Bagamoyo, Mkuranga na Kisarawe mkoani Pwani kuwa hazina umeme na kusisitiza kuwa hali hiyo inachangia kuchelewa kutolewa kwa hukumu na haki kwa wananchi. 
 
MWANANCHI

Related

OTHER NEWS 9044676503013258556

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

item