TISHIO LA EBOLA WANANCHI WATAKIWA KUJIHADHARI

Na Hannah Mayige,  wa Chuo Kikuu Huria, OUT TISHIO la ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuuwa mamia ya watu Afrika Magharibi, umezua wasi...



Na Hannah Mayige,  wa Chuo Kikuu Huria, OUT
TISHIO la ugonjwa wa Ebola unaoendelea kuuwa mamia ya watu Afrika Magharibi, umezua wasiwasi  mkubwa   kwa nchi za Afrika  na  dunia nzima  kwa  ujumla na kutakiwa watanzania kuchukua tahadhari  kubwa kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini.
Lazima  Serikali na wananchi  wazingatie masharti na tahadhari inayotolewa kimataifa kuudhibiti ugonjwa na utayari wake wa kupambana nao.
Ugonjwa wa Ebola, umekuwa tishio kubwa kwa uhai na ustawi wa mataifa mbalimbali yakiwemo ya Afrika Mashariki ambako Tanzania ni mojawapo.
Mpaka  sasa, nchi zilizoathirika na ugonjwa  huo ni pamoja na Cameroon, Liberia na Nigeria  ambapo tayari  zaidi  ya  watu  1,000 wamepoteza maisha.
Eneo la Afrika mashariki,  kuna taarifa kuwa  hivi karibuni alipatikana mgonjwa  wa Ebola  katika  nchi ya  Rwanda na kwamba miaka ya nyuma milipuko iliwahi kutokea nchini Uganda. 
Ebola  ni ugonjwa  ambao  mpaka  sasa hauna tiba  wala chanjo,  ambapo  huambukiza  kwa njia  ya  hewa au majimaji  yatokayo mwilini kama mate , jasho,  damu na kwamba mgonjwa  akigusana  na    mtu  asiye na virusi  hivyo basi  anaambukizwa.
 Shirika la  Afya  Duniani (WHO) limetahadharisha nchi mbalimbali  hasa  Afrika kuchukua tahadhari  kubwa, mfano hivi karibuni ndege za shirika la Kenya  lilishauriwa kutoendelea  na safari zake za Afrika Magharibi  kwa kuhofia baadhi yaabiria wake kuhamisha virusi vya Ebola na kusambaza katika eneo la Afrika Mashariki.
Kenya ni mojawapo ya nchi za Afrika mashariki zenye safari nyingi za ndege kuelekea mataifa mbalimbali.
Kutokana na wito huo wa WHO, tayari  Korea imesitisha safari zake za ndege kwenda Kenya kwa tahadhari ya kudhibiti usambaaji wa Ebola.
Kwa kuwa ugonjwa  huo  unaambukiza kwa njia ya hewa pia na majimaji yatokayo mwilini hata madaktari  na wauguzi wanalazimika kuwa na mavazi maalum ambayo yanafunika  mwili  mzima, kwani   hawatakiwi kugusana kwa namna yeyote  ile.
Msimamizi wa  Vituo vya Afya mipakani Tanzania, Dk. Khalid Massa, anasema vifaa hivyo ni pamoja na magauni, aproni, buti, gloves na vifaa maalum vya kuziba pua na mdomo.
“Wahudumu wanatakiwa kuvaa vifaa hivyo kujikinga na maambukizi na tayari vifaa 20,000 vimepokelewa na kusambazwa katika maeneo yaliyoainishwa,” anasema Dk. Massa.

Dk. Massa, anasema kwa kushirikiana na maofisa uhamiaji wamejikita zaidi kuchunguza wasafiri wa ndege hasa wanaotokea Afrika Magharibi.
Naye, Mtaalamu wa Kudhibiti magonjwa ya mlipuko Dk. Vida Makundi, anawaasa wananchi kuripoti mapema katika vituo vya afya au kwa viongozi wa serikali za mitaaa endapo watakuwa na dalili   za ugonjwa huo.
Anazitaja dalili kubwa ambazo  zimeelezwa  na Shirika la Afya  duniani ni pamoja na kuumwa sana kichwa , kupata  homa  kali na hatimaye kutokwa  na damu katika  maeneo yenye  uwazi, kama vile  mdomoni, ngozi, masikioni na sehemu za siri.
Ebola imesababisha hofu na tafrani  kubwa kwa nchi hasa zinazoendelea  kwa  kuua watu bila kupata tiba ikiwa ni pamoja na madaktari  na udhoofisha  hali ya uchumi kutokana na shughuli nyingi za kusafiri na zinazokutanisha watu kusitishwa.
Shughuli za biashara za kimataifa pia  zinaendelea kutetereka kuogopa maambukizi  ya virusi vya Ebola hasa  wananchi katika nchi zenye  ugonjwa  huo kuogopana wenyewe  kwa wenyewe.
Mfano, huko Cameroun, kuna mtu alikutwa amekufa barabarani hakuna  mtu  aliyethubutu kumsogelea  mpakawalipokuja  madaktari ambao walivalia rasmi kuhakikisha   hakuna maambukizi mapya kwa watu wengine.
Hapa  Tanzania, tayari serikali kupitia viongozi  mbalimbali akiwemo  Makamu wa  Rais Mohamed Ali  Bilal , Waziri wa Afya Dk. Seif Rashid na baadhi ya wakuu wa mikoa ya Manyara, Dar es Salaam na  Mbeya  wamewataka wananchi kuwa waangalifu na wageni wasio wajua na kuwa tahadharisha  kwenda hospitali mara wanapoona wana dalili zisizo za kawaida au zinazoashiria  ugonjwa  wa Ebola.
Kulingana  na tamko la serikali , Ebola  bado haijaingia nchini lakini  usemi wa Kiswahili usemao ‘ ukiona mwenzako ananyolewa,  wewe  tia maji’.
Kwa  upande wa kutenga maeneo maalum ya kushughulikia wagonjwa wa Ebola, serikali imetenga maeneo mawili kwa Dare s Salaam, Temeke na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
 Waziri wa afya  DK. SeifRashid anasema tayari wauguzi na madaktari wanapatiwa elimu  kuhusiana  na kuudhibiti  ugonjwa wa  Ebola kabla  haujaingia  nchini, elimu hiyo  inatolewa katika  hospitali zote .
Nao, wananchi kwa nyakati tofauti wameendelea kumlilia mungu kwa mlipuko wa magonjwa hapa barani Afrika. “Mara ukimwi, mara Dengue mara Ebola yote hakuna tiba,” analalamika mmoja wa wananchi Kasian Komba mkazi wa Songea.
Kutokana na taarifa za baadhi ya wananchi wa Liberia kuvamia kituo kilichotengwa kuhudumia wagonjwa wa Ebola na kupora magodoro, vifaa na wagonjwa kutawanyika, ni taarifa mbaya na huenda imetokana na kukosa elimu ya ugonjwa huo.
Kwakuwa elimu ni muhimu,  ni vyema serikali hapa nchini ikatumia fursa hii kuelimisha umma kwa kutumia mikutano ya hadhara, Sanaa za maonesho, mabango, vyombo vya habari kama mitandao ya kijamii,  redio, televisheni, magazeti na vipeperushi ili jamii ipate uelewa.
Makala hii imeandikwa na Hannah Mayige, Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania – OUT.
Anapatikana kwa E-mail  hannahmayige@gmail.com

Related

OTHER NEWS 167618685589272694

Post a Comment

emo-but-icon

FOLLOW US

.

LISTEN / DOWNLOAD MUSIC HERE:

Total Pageviews

RECENT

Archive

item